Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati akijinadi yeye na wagombea udiwani na ubunge wa CCM mkoani hapa ili wachaguliwe katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli alikuwa akijinadi na wagombea hao kwa nyakati tofauti katika mji wa Mbalizi na wilayani Songwe eneo la Mkwajuni, Makongolosi wilaya ya Chunya.
Magufuli ambaye jana alikuwa katika siku ya nne ya kujinadi kwa wananchi na kuomba kura tangu kufunguliwa kwa pazia la kampeni mikoani, alisema tangu kuanza kwa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM wa urais ndani ya chama hicho, hakutumia fedha bali alikwenda kimya kimya makao yao makuu kuchukua fomu na kuzirejesha.
Alisema kwa mantiki hiyo, hana cha kulipa kwa sababu hadaiwi na mtu yeyote.
Magufuli alisisitiza kuwa anachofahamu ni kwamba deni kubwa alilonalo ni kuwatumikia Watazania na kuwaletea maendeleo ili wazidi kuwa na maisha bora.“Nilichukua fomu kimya kimya na kurudisha kimya kimya, natembea na barabara ili shida zenu ziwe shida zangu, ili nikiingia Ikulu nizishughulikie kwa haraka,” alisema.
Magufuli alisema anaamini kuwa kuteuliwa kwake na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro hicho kuna makusudi ya Mwenyezi Mungu ili afanye kazi.
“Sikutoa rushwa kwa kuwa ni dhambi na adui wa haki... niliacha mchakato huo wa kumpata rais ndani ya CCM ufanywe na Mungu,” alisema.
AOMBA POWER
Dk. Magufuli alisema wale wanaosalimia kwa kutumia salamu na kauli mbiu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Peoples Power, wampe ‘power’ aende Ikulu kuharakisha maendeleo ya watanzania.
“Nipeni wabunge na madiwani wa CCM nikafanye kazi, tutafanyakazi bila kinyongo, hatutawabagua, hapa ni kazi tu,” aliahidi.
Alisema maendeleo hayana chama, kabila wala rangi, hivyo amepanga kufanya kazi na makundi yote bila kubagua na kuomba kura kwa wananchi wote bila ya kujali vyama vyao vya siasa.
“Hakuna anayezaliwa kutoka tumboni mwa mama yake akiwa na kadi ya chama fulani, bali wanavikuta, hivyo msidangaywe na vyama, kinachotakiwa ni maendeleo,” alisema.
WALIMU VUMILIENI
Akizungumzia kuhusu madai ya walimu nchini, alisema kada hiyo siyo wito bali ni kazi, fedha na kuwafundisha wanafunzi kwenye shule walizopangiwa na serikali.
Alisema baada ya kuingia Ikulu, kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuwalipa madeni wanaoyoidai serikali.
Magufuli aliwataka walimu kuwa wavumilivu na kuwaomba kumchagua kwa kura nyingi katika uchaguzi huo.
“Sitawaangusha, nitamtanguliza Mungu na kila mmoja katika sala zake aniombee nisijeanza kwa kiburi, kujiona, kusahau ahadi, niwe mtumishi wa watu, nikapendwe kwa utumishi na siyo bora utumishi,” alisema.
AWATANGAZIA KIAMA MAJANGILI
Aidha, Magufuli alitangaza kiama dhidi ya majangili wanaoshirikiana na askari wanyamapori kupora rasilimali za meno ya tembo na pembe za ndovu huku akishangazwa na kitendo cha askari wanyapori kulipwa mishahara vizuri na wenye silaha kwa kushindwa kuwalinda tembo kwenye hifadhi za wanyamapori nchini na kuuawa na meno yao kukatwa na kusafirishwa nchi za nje.
Alionya kuwa serikali yake haitakubali vitendo hivyo viendelee.
WAKURUGENZI
Pia, Magufuli alisema serikali yake itapiga marufuku wakurugenzi wa halmashauri nchini kutembelea magari ya kifahari na kukaa kwenye majengo mazuri wakati wanafunzi wakisoma wakiwa wamekaa chini madarasani.
Alitangaza kuwa elimu itakuwa ikitolewa bure kwenye shule za serikali na kuboresha mazingira ya kusomea.
Magufuli alionya kuwa watakaoshindwa kwenda na kasi yake katika kutumikia wananchi, watakazimika kuachia madaraka.
MAADHIMISHO MARUFUKU
Kadhalika, alisema katika serikali yake itakuwa ni marufuku kufanyika maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa kuwa yana lengo la waandaji kulipana posho na kuvaa sare za fulana na kofia huku wananchi wakiteseka kwa kukosa maji safi na salama.
AWALIPUA WAPINZANI
Katika hatua nyingine, awalirushia kombora wapinzani, akiwataka wananchi wasiwachague kwa madai kuwa watasababishia mateso.
Alisema kwa sasa Tanzania inaelekea kwenye neema ya maliasili kama ya gesi, madini na wanyamapori, ndipo wapinzani wanajitokeza kuwalaghai watanzania kuwa wataleta mabadiliko makubwa.
AIAGIZA TANROADS
Katika hatua nyingine, Magufuli ameendelea kutumia wadhifa wake wa uwaziri wa Ujenzi kwa kumwagiza Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Mbeya, kujenga barabara ya kilomita moja mjini Mbalizi na kutangaza zabuni ya kilomita nne za barabara mjini Makongolosi ndani ya wiki moja.
Pia, amemwagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads, kupeleka fedha za ujenzi na upanuzi wa barabara hizo ndani ya wiki moja.
Akihutubia mikutano ya hadhara mjini Mbalizi na Makongolisi, alimpandisha jukwani Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Abass Kandoro na kumtaka ampelekee maagizo hayo Meneja wa Tanroads wa mkoa huo aliyemtaja kwa jina la Lyakurwa.
“Mimi bado ni Waziri wa barabara, ukifika ofisini mweleze Lyakurwa barabara hii ianze kujengwa, leo (jana) nampigia Chief Executive (Mtendaji Mkuu) wa Tanroads alete fedha haraka, wiki hii nataka kuona kazi inaanza...natamani ningekuwa rais nianze kazi leo niguse na sekta nyingine,” aliagiza.
Akiwa katika katika mji wa Makongolosi, alimuita jukwaani Kandoro na iagiza Tanroads kutangaza zabuni ya kilomita nne za barabara za mjini Makongolosi.
“Mimi napenda mambo yaende harakaharaka, uwaziri wa ujenzi bado ninao, tukitoka hapa RC mwambie Meneja wa Tanroads atangaze zabuni ya kilomita nne mjini Masongolosi zianze kujegwa na fedha nitatoa, nataka muone kuwa nasema na kutekeleza,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment