Mgombea urais kupitia Chadema , Edward Lowassa akishuka katika basi la daladala .Picha na Edwin Mujwahuzi
Tunaweza kuendelea kwa kufanya mambo ambayo waliotunzunguka wanayaona si ya kawaida? Maana yake tunaweza kuendelea bila kukubalika katika ulimwengu wa leo? Wale wasiotupenda wanasema kuna mambo ambayo yanatendeka katika Taifa letu tu na wala hayatendeki nchi nyingine.
Kwa mfano, tukienda dukani, tunaomba kununua kwa pesa zetu, lakini unamwambia mwenye duka “naomba kununua sabuni”. Nchi jirani ya Kenya wanasema “nataka sabuni”. Kuna mengi, nikiandika nitajaza ukurasa mzima.
Acha nitolee mfano hili la leo la “Lowassa ni yule yule na mambo yake ni yaleyale”. Hili litafafanua vizuri hoja yangu. Wakati Edward Lowassa, akiwa CCM, niliandika makala juu yake. Nakumbuka wakati huo wana-CCM walichukizwa na makala yangu na baadhi kuniandikia ujumbe mwingi wa matusi na kunishutumu kwa kununuliwa na vyama vya upinzani. Nilishutumiwa kwa kuandika uongo na uzushi!
Matusi yalikuwa mengi, nikafikiri labda nilikosea sehemu. Nililazimika kuchimba zaidi juu ya matukio ya Lowassa. Niliongea na watu waliomfahamu kwa karibu. Nilipekua huku na kule na kusoma yaliyoandikwa na wenzangu nje na ndani ya nchi juu ya Lowassa, lakini matokeo yalikuwa ni yaleyale na mambo yaleyale. Nilikuwa sijakosea chochote.
Nilijaribu kuwaelewa hawa ndugu zangu wa CCM, maana kila mtu makini ni lazima akitetee chama chake na watu wake. Heshima inapanda zaidi pale mtu anapotetea ya ukweli zaidi ya ushabiki na ulevi wa madaraka. Lakini mtu akitetea kwa vile anakitetea chama na yale uongo, unakuwa ushabiki zaidi ya uzalendo ambao ninajaribu kuelezea.
Vyama vya upinzani vilinipongeza kwa makala yangu hasa kwa kuandika ukweli bila woga na kunipongeza kwa kupiga simu na kuandika ujumbe wa shukrani.
Vyama vya upinzani vilionyesha kumchukia Lowassa na kufikiri kwamba labda huyu ndiye kikwazo cha wao kuchukua madaraka!
Makala yangu haikuwa sifa kwa Lowassa, hivyo kwa vyama vya upinzani ilikuwa ni silaha tosha ya kuiwajibisha CCM. Na hasa imani kwamba Lowassa alikuwa na wafuasi wengi ndani ya chama hicho. Nguvu zake za kutengeneza mtandao wa ushindi mwaka 2005, zilikuwa zinaonekana wazi.
Hivyo kwa upinzani, kuonyesha kasoro zake, walipokea kwa mikono miwili. Katika safu hii, wiki iliyopita, niliandika kuhusu Lowassa, kwa kutumia maneno yaleyale kama niliyoyaandika miaka ya nyuma kidogo. Niliirudia bila kupunguza wala kuongeza neno lolote lile.
Kwa vile sasa amehamia Ukawa, basi CCM walikuwa wa kwanza kunishukuru kwa kuandika bila woga na kuandika ukweli mtupu.
Hawakukumbuka tena jinsi walivyonitukana nilipoandika juu yake. Uzushi wangu na uongo wangu sasa umegeuka kuwa ukweli na ukweli mtupu! Inashangaza kidogo na kuacha maswali mengi! Tutahukumiwa na historia.
Zamu hii ilikuwa ni ya vyama vya upinzani kunitukana matusi ya nguoni. Nimegundua umuhimu wa sheria mpya ya mtandao. Maana kuna watu wanatukana matusi kabisa ya nguoni.
Kumbe ukitaka usalama ndani ya nchi hii usimseme Lowassa. Kama unakataa jaribu uone! Kusema kweli sms nilizozipata zilivunja rekodi ya idadi kubwa niliyowahi kupata hadi sasa katika maisha yangu.
Miaka michache iliyopitia walinipongeza kwa kumwandika Lowassa, na kunipongeza kwa kuandika ukweli bila kuogopa. Lakini leo hii wananitukana maana Lowassa, amejiunga nao.
Tumeandika mambo yaleyale, bila kupindisha wala kubadilisha. Wao wanampokea Lowassa wanayemtaka.
Akiwa upande wao anakuwa mtu safi, akiwa upande mwingine anakuwa mtu mbaya. Nani mnafiki hapa?
Lowassa, yuleyule na mambo yaleyale, anakuwa na sura mbili katika jamii. Na kusema ukweli sura hizi mbili si ndugu! Maana Lowassa, alipokuwa CCM, ukimwandika, wana-CCM walimtetea kwa nguvu zote. Lakini Lowassa nje ya CCM, anakuwa makapi.
Tunaandika juu ya Lowassa, mambo yaleyale bila kutoa neno hata moja. Lakini maneno hayo yanakuwa mazuri kwa Lowassa wa CCM na kuwa mabaya kwa Lowassa wa Ukawa. Inachekesha, inashangaza na labda ni kurogwa!
Kwa upande wa vyama vya upinzani Lowassa wa CCM ni mbaya, lakini Lowassa wa Ukawa ni shujaa na rais mtarajiwa. Huyu aliyeitwa fisadi, huyu aliyeitwa ana uchu wa madaraka, leo hii huyu ni mkombozi. Wanasema hakuna rafiki au adui wa kudumu katika siasa. Lakini je, hata kwa mambo ya msingi kama haya?
Sura mbili za mtu yuleyule, mambo yaleyale, huku anakuwa mzuri, huku mbaya? Akihama chama kimoja na kujiunga na kingine anakuwa mbaya na kuwa mzuri kwa wakati mmoja?
Je, hizi siyo siasa za unafiki? Wanasiasa wameacha kuangalia na kuitambua dira ya Taifa letu.
Wanatanguliza vyeo na madaraka. Wanasiasa wanafumbia macho mahitaji muhimu ya kuleta mabadiliko katika Taifa letu. Wanafumbia macho mahitaji ya kuliendeleza Taifa letu na kuliingiza kwenye ulimwengu mpya wa sayansi na teknolojia.
Tunapoingia kwenye uchaguzi mkuu kwa kuongozwa na unafiki, chuki na uchu wa madaraka hatuwezi kupiga hatua yoyote ile. Tutabaki kwenye matusi, vijembe na mipasho huku muda unakimbia na miaka inayoyoma. Tukizinduka tutakuwa tunaogelea kwenye ukoloni mamboleo.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment