Nyumba iliyoteketea kwa moto na kuua watu tisa wa familia moja huko Buguruni, Jijini Dar es Salaam
Jiji la Dar es Salaam linaomboleza moja ya misiba mikubwa baada ya watu tisa wa familia moja kuteketea kwa moto ulioibuka usiku kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hitilafu ya moto.
Juhudi zao kutaka kujiokoa na majirani kuwaokoa zilishindikana kutokana na moto kuwa mkali, lakini pia milango ya chuma kushindwa kufunguka baada ya kutanuka kutokana na moto huo.
Hali kadhalika, kufuli lililokuwa kwenye mlango wa mbele halikuweza kufunguka kutokana na moto huo. Na watu hao walipoona juhudi zote zimeshindikana, walikwenda kwenye chumba kimoja alichokuwa akilala bibi yao na wakashikana mikono kusubiri mauti yao.
Ni msiba ambao umetikisa siyo tu Jiji la Dar es Salaam, bali nchi nzima, lakini likiacha mambo mengi ambayo Taifa linatakiwa lijifunze katika kuboresha makazi ili kuweka maisha yetu kuwa salama zaidi.
Kwa sasa, Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa ujenzi holela ambao hauzingatii miundombinu ya usafiri, majitaka, maji safi, uunganishaji umeme, miundombinu ya zimamoto, na suala la kujihami na matukio kama moto ndani ya nyumba.
Nyumba nyingi zimefanana majengo, zikiwa zimewekewa milango ya chuma sehemu ya mbele na nyuma, bila ya kuwa na milango ya dharura iwapo kunatokea tatizo kama hili la hitilafu ya umeme.
Wengi hujenga bila ya kushirikisha wasanifu wa majengo kwa ajili ya ushauri kuhusu mambo mbalimbali kama hili la usalama. Kibaya zaidi, mamlaka zinazohusika na makazi ya watu, huwa hazifuatilii ujenzi wa majengo ya makazi, licha ya kuwapo sheria inayowapa mamlaka ya kusimamisha ujenzi au kuruhusu uendelee iwapo unakidhi masharti yaliyowekwa.
Hali hii inazidi kuyaweka maisha ya wakazi wa Dar es Salaam katika hali ya hatari, hasa ikizingatiwa pia kuwa hakuna miundombinu ya zimamoto, hakuna njia za kupita kufikia kila nyumba na pia wananchi hawapewi elimu ya kujikinga na majanga.
Ujenzi huo, pia unaliweka Jiji la Dar es Salaam katika hali rahisi ya kukumbwa na magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu, ambacho safari hii kimeibuka tena jijini humu kukiwa hakuna mvua kama ilivyokuwa nyakati nyingine.
Ujenzi huu pia hulifanya jiji hili kupata mafuriko kirahisi kwa kuwa ujenzi hauzingatii miundombinu ya majitaka na hivyo mvua kidogo zinaponyesha, maji hujaa kirahisi kwa kuwa hayapati njia ya kufuata mkondo wake kirahisi. Mamlaka husikazinashuhudia ujenzi huu holela, lakini hazitimizi wajibu wake na badala yake Dar limegeuka kuwa ni mkusanyiko wa mitaa isiyo na mpangilio maalum, mithili ya vijiji vya kienyeji. Hii ni hatari kwa maisha ya wakazi wa jiji hili.
Pamoja na ukweli kwamba wadau wote wana wajibu wa kuhakikisha ujenzi unafuata mpangilio na ramani ya Jiji la Dar es Salaam, mamlaka husika hazina budi kuhakikisha hakuna mtu anayejenga ovyo. Ni vizuri mamlaka zikahakikisha wote wanaotaka kujenga, wanafuata mpangilio wa jiji ambao unaonyesha mambo yote ya kuzingatia.
Wadau wengine kama Kikosi cha Zimamoto, hawana budi kuhakikisha kuwa ujenzi wa nyumba za makazi unazingatia usalama wa wenye nyumba kwa kuwa na tahadhari dhidi ya moto na mambo mengine yanayohatarisha usalama wao.
Kama askari wa Kikosi cha Zimamoto wanaweza kutanda barabara zote jijini Dar es Salaam kukamata magari yasiyo na mitungi ya kuzimia moto, wanashindwaje kuweka mkakati wa kupita kila mtaa kutoa elimu ya kujikinga na majanga?
Tuna imani kuwa mambo hayo yakizingatiwa, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa athari zitokanazo na majanga ambayo yanazuilika.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment