Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, August 5, 2015

Njia alizopita Lowassa kufika Chadema

Na Ahmed Rajab
EDWARD Lowassa, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Tanzania na mmoja wa vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameibuka kuwa ndiye atayeshika bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwania urais wa Tanzania.

Kwa kuchukua hatua hiyo, yeye ndiye chaguo la vyama vya upinzani vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwa mgombea wa urais wa kupambana na Dk.John Magufuli wa CCM.


Safari iliyomfikisha Lowassa Chadema ilikuwa ndefu. Ilianza miezi michache iliyopita ilipodhihirika kwamba wale wenye kuihodhi nchi hawamtaki awe Rais. Kwa hivyo, kulikwishaandaliwa njama za kumzuia asiwe mgombea wa urais wa CCM.


Kuna siku ambapo maelezo ya safari hiyo yataandikwa kwa ukamilifu.


Maelezo hayo yatapowadhihishwa yataonyesha wazi njia walizozipita Lowassa na viongozi wa Chadema, walifikia wapi na walikubaliana nini. Kwa sasa, na itoshe tukisema kwamba mashauriano yalikuwa magumu na yalikuwa ya “nipe, nikupe.”


Lowassa alisailiwa kinagaubaga kuhusu shutuma mbalimbali anazoshutumiwa.


Waliporidhika na majibu yake, viongozi kadhaa wa Chadema walibidi wapige moyo konde wakubali kumkumbatia. Halikuwa jambo rahisi.

Wala sio wote waliomkubali.Lowassa ni mtu waliozoea kumshambulia kwa tuhuma za ufisadi.Kwa namna alivyokuwa akipakwa matope ungedhani kwamba hata harita zisingaliweza kumsafisha.

Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Chadema walitumia hekima, busara na mantiki walipokuwa wakimpima.


Walihoji kwamba lengo lao kuu na la awali ni kuing’oa CCM madarakani. Kwa hivyo, ni muhimu kuunganisha nguvu zote zinazoweza kuunganishwa ili CCM iangushwe.


Duru za waliokuwa karibu na mashauriano hayo zinasema kwamba hatimaye viongozi hao walikubaliana kwamba Lowassa ahamie Chadema. 

Aidha, walikubaliana kwamba atapewa fursa ya kuwa mgombea wa urais atakayeungwa mkono na vyama vilivyo katika Ukawa.

Kuna viongozi wachache wa vyama vingine vilivyo katika Ukawa ambao mpaka sasa wanaona taabu kumkubali na kufanya kazi naye Lowassa.Lakini,kwa jumla, wengi wa viongozi wa vyama hivyo wameungana na Chadema kumkubali.


Walipokuwa wakimpima viongozi wenzake wa upinzani walivutiwa na rekodi yake ya utendaji kazi. Hakuna aliyetia dosari sifa alizojipatia katika uendeshaji wa wizara alizowahi kuzishika. 


Anatambulika kwamba yeye ni mchapakazi na ni kiongozi mwenye kufuatilia jambo mpaka mwisho wake.

Kwa upande wake, miongoni mwa mingine, Lowassa ameahidi kuunga mkono muswada wa Katiba uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, mswada huo ni wa ile iitwayo “Katiba ya wananchi” ambayo CCM imeikataa.


Suala la kupambana kidhati na ulaji rushwa na ufisadi, kwa jumla, ni jambo jingine litalopewa kipaumbele na serikali itakayoundwa na Ukawa pale CCM itaposhindwa, kama inavyotarajiwa. Lowassa mwenyewe ameahidi kwamba hatouvumilia ufisadi.
Kwa mujibu wa hesabu zilivyo mpaka sasa, inaelekea kwamba kwa mara ya mwanzo Muungano wa Tanzania utakuwa na serikali ya mchanganyiko wa vyama itayoongozwa na Chadema.


Walio karibu na Lowassa wanasema kwamba kuna wabunge wasiopungua 83 watakaohama CCM na kumuunga mkono waziri huyo mkuu wa zamani.


Wabunge hao pamoja na wanachama wengine wa CCM wataomfuata Lowassa hawatoihama CCM kwa mkupuo mmoja. Wataiacha mkono kwa vikundi vikundi, toka sasa hadi Oktoba, ili wazidi kuwahamasisha Watanzania.

Athari za hatua ya Lowassa ya kujiunga na Chadema zimekwishaanza kuonekana. Hulisikii jina la Magufuli likizungumzwa sana kama linavyozungumzwa la Lowassa.


Jina la Lowassa ni zito katika siasa za Tanzania. Kwa kuhamia upinzani limehamasisha na kuzifanya siasa za Tanzania zizidi kuwa zi moto na tamu. Nadhani, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania,sasa kuna uwezekano mkubwa wa CCM kushindwa katika uchaguzi na Tanzania kuwa na Rais asiye wa kutoka chama hicho.


Tukio hilo, likitokea, litakuwa mithili ya zilzala katika siasa za Tanzania.Hilo, lakini, litawezekana endapo tu vyama vya upinzani vitapoendelea kushikamana.
Jambo litaloweza kuviletea mtafaruku kwa sasa ni hilo chaguo la Lowassa kuwa awe mgombea wa Chadema, na kwa hivyo wa Ukawa, katika uchaguzi wa urais.


Tatizo ni jinsi Lowassa alivyokuwa akihusishwa na ufisadi. Kuna mengi yaliyosemwa na yanayosemwa kumhusu bwana huyu. Pengine shutuma anazovurumishiwa zina ukweli.


Lakini kama kweli zina ukweli, hata kama ni chembe tu ya ukweli, kunazuka swali la kwanini asichukuliwe hatua za kisheria? Au kwanini wakati wa uhai wake Mwalimu Julius Nyerere, anayetajwa mara kwa mara, kwamba alikuwa akimpinga Lowassa asimfukuzishe kwenye chama? Kwanini aliachia aendelee kuwa kiongozi katika chama na serikali?


Swali jingine linaloulizwa ni kuwa je, tangu Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu ufisadi serikalini umepungua au umeongezeka?


Tutakuwa ni watu wenye fikra finyu endapo tutawaamini waliokuwa viongozi wenzake ndani ya CCM wanapomlaumu yeye peke yake kwa ufisadi.
Kuna mambo matatu ya kimsingi ambayo Tanzania inayahitajia, kwa viwango tofauti, ili iweze kustawi na kuendelea.Haya ni mambo yenye umuhimu mkubwa si kwa maendeleo tu bali hata kwa heshima ya taifa hili mbele ya macho ya walimwengu.


Mambo hayo matatu ni: demokrasia na ukuaji wake; busara ya watawala na watawaliwa; na uhalali wa watawala na wapinzani.


Hayo ni mambo ya thamani. Yanahitaji kuzingatiwa kwa makini katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.


Kuna wengi wenye kulalamika kwamba Tanzania, na hususani Zanzibar, haina demokrasia ya kweli.Zipo sababu zinazoifanya demokrasia ishindwe kushika mizizi kama ipasavyo katika jamii ya Watanzania.
Sababu moja ni kwamba imekuwa ikichimbwa kwa vitimbi vya watawala wasio na busara, hasa wakati wa uchaguzi, na zaidi visiwani Zanzibar.


Tangu mfumo wa siasa za ushindani wa vyama vingi urejelewe tena 1992 hakuna uchaguzi mkuu uliofanywa nchini humu bila ya kuzuka vituko vya aina kwa aina.


Kura zimekuwa zikiibiwa, watu wakipigwa na wengine kufika hadi ya kuuliwa na vyombo vya dola.
Yote hayo yamefanywa ili watu fulani waweze kuendelea kutawala kwa sababu wanaamini kwamba ni wao peke yao wenye haki hiyo.


La kushangaza ni kwamba baadhi ya yale yanayofanywa na chama kinachotawala dhidi ya wapinzani wake hufanywa pia ndani ya chama hicho chenyewe. Bado hawajauana lakini katika chaguzi za ndani ya chama hicho wamekuwa wakiibiana kura, wakipigana, kutandikana bakora na kuumizana.


Yametokea hayo mwishoni mwa wiki iliyopita Bara, kwa mfano, katika jimbo la Iramba, mkoani Singida ambako wana CCM wamekuwa wakilalamika ya kuwa kwenye kura za maoni kumetokea wizi wa waziwazi.


Yametokea hayo pia katika sehemu mbalimbali za Unguja, ikiwa pamoja na jimbo jipya la Mahonda. Huko, katika mchuano wa kura za maoni za kumtafuta mgombea wa uwakilishi Balozi Seif Idi, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, alishindwa na kijana mwenye umaarufu mkubwa katika jimbo hilo.Ikabidi uchaguzi huo ubatilishwe na urejelewe tena siku ya pili.


Uvumi ulioenea ni kwamba kijana huyo ambaye kwa umaarufu anaitwa Alwattan alisimamishwa ampinge Balozi na wazee wa eneo la Donge lililoingizwa katika jimbo hilo.


Wazee hao wananukuliwa wakisema kwamba wataendelea kumpinga Balozi mpaka awarejeshee mtoto wao Sheikh Msellem Ali ambaye ni mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Uamsho, waliowekwa korokoroni Bara.


Balozi alishindwa licha ya shutuma kwamba upande wake ulifumwa na kura za bandia.


Ikiwa wenyewe kwa wenyewe wanafanyiana hivi, jee mahasimu wao watawafanyia nini? Hii ni dalili iliyo wazi ya kwamba kuna mtikisiko mkubwa ndani ya CCM uliosababishwa na Lowassa.


Siku zote viongozi wake wakuu wakichukulia kwamba mambo yao yatajiendea tu watakavyo wao.


Leo hali imebadilika. Wanakabiliwa na upinzani mkali nje ya chama ukiongozwa na Lowassa na ndani ya chama ukiongozwa na wahisani wa Lowassa. Matokeo yake ni kwamba viongozi hao wa CCM wamebabaika na wanatapatapa.


Hatari iliyopo ni kwamba katika kutapatapa kwao wanaweza wakaiweka kando busara na wakachochea matumizi ya nguvu na uvunjwaji wa amani.


Badala ya kuwa waungwana na watamaduni wakaingia katika kundi la wahuni wa kuchochea fujo kama tunazozishuhudia siku mbili hizi Burundi au zile zilizosababisha mauaji Rwanda au Cote d’Ivoire.


Hatutochoka kukumbushana kwamba siku hizi ulimwengu umebadilika na hauvumilii tena mauaji yanayofanywa kwa sababu za kisiasa. Wenye dhamana ya vitendo kama hivyo huishia mjini Hague kwenye Mahakama ya Jinai ya Kimataifa aliko Laurent Gbagbo, Rais wa zamani wa Cote d’Ivoire.


Au hukamatwa na kufunguliwa kesi humu humu Afrika kama ile inayomkabili Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre, huko Senegal.


Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeutambua umuhimu wa usalama na amani wakati uchaguzi. Kwa hivyo, imekuwa ikiandaa mikutano maalumu katika sehemu mbalimbali za Bara kuzungumzia suala hilo.


Taasisi hiyo ilipanga iwe na mkutano wa aina hiyo kwenye hoteli ya Bwawani, Unguja, Jumapili iliyopita uliokuwa uongozwe na Joseph Butiku, mmoja wa viongozi wa Taasisi hiyo na aliyewahi kuwa katibu wa Mwalimu Nyerere.


Bahati mbaya Jumamosi Butiku aliarifiwa na Balozi Idi kwamba serikali ya Zanzibar haitoruhusu mkutano huo ufanyike kwa madai ya kwamba waliopangwa wazungumze walikuwa “wapinzani” na hiki ni kipindi cha kampeni za uchaguzi.


Kwa ufupi, kilichotokea ni kwamba serikali ya Zanzibar iliupiga marufuku mkutano uliokuwa na dhamira ya kuzungumzia jambo la maana — la usalama na amani wakati wa uchaguzi.


Hatua hiyo isiyoeleweka ni mfano wa mambo yanayoifanya demokrasia ipate taabu kushika mizizi nchini. Demokrasia ina madosari yake. Lakini ni kheri tuwe na madosari ya kidemokrasia kushinda kuwa na madosari ya utawala wa kimabavu, kwani mfumo ulio mbadala wa utawala wa kidemokrasia ni udikteta.
 

- See more at: http://raiamwema.co.tz/njia-alizopita-lowassa-kufika-chadema#sthash.VFvuZ5Zz.dpuf

No comments :

Post a Comment