Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 28, 2015

Njia ya kufikishwa ICC ni fupi!

Njia ya kufikishwa ICC ni fupi
Na Ahmed Rajab
MABADILIKO hayaepukiki. Ikiwa yatapatikana yote yale yanayohitajika kuibadili hali fulani ya mambo, hata ya nchi, basi hapana budi ila mabadiliko yatokee. Kwa hakika, tumezoea kujifanya kama tusioona lakini mabadiliko yanatokea siku zote katika jamii. Tena hutokea katika hali ambazo inakuwa taabu kwa mtu mmoja au hata kikundi cha watu kuweza kuyadhibiti mabadiliko hayo au kuyazuia yasitokee.

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakabiliwa na hayo hivi sasa. Wanajikaza kisabuni lakini wanafahamu vizuri kabisa kwamba wanakabiliwa na changamoto kubwa isiyowahi kamwe kuwakabili wao au viongozi waliowatangulia wa chama chao. Hakuna asiyeona jinsi chama hicho kilivyomeguka.Kumeguka huko ndiko kutakoleta mabadiliko Tanzania.

Kwa hivi sasa, chama cha CCM kimekuwa kama kishada kinachokwenda arijojo. Hakuna tena mtu yeyote wala kikundi cha watu wataoweza kukizuia chama hicho kisiendelee kumeguka au kuyazuia mabadiliko ya nchi yasitokee. Nionavyo ni kwamba umefika wakati ambapo nchi hii haiwezi kupata maendeleo inayoyahitaji ikiwa itaendelea kutawaliwa kama ilivyotawaliwa kwa muda wa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ili iweze kuendelea; lazima papatikane mabadiliko ya watawala na ya mfumo wa utawala.

Hali ya sasa ya kisiasa Tanzania na matukio yake ya hivi karibuni yanaashiria mabadiliko makubwa yatayotokea nchini humu. Mabadiliko hayo tayari yamekwishaanza kutia sura na tutakuwa tunajidanganya tukijidai kuyapuuza na kuyaona kuwa yasiyo na maana. Hiki “kimbunga cha Lowassa” si kidogo. Kina uwezo wa kuufungua ukurasa mpya wa historia ya Tanzania itapofika Oktoba 25.

Wako wanaojidanganya, wanaojaribu kila mara kumfananisha Edward Lowassa na Augustine Mrema. Kwa kufanya hivyo, wanakuwa wanajaribu kujenga dhana ya kwamba Lowassa, mithili ya Mrema, hana lake jambo. Wanakuwa wanajaribu kutwambia kwamba Mrema alikuwa na kishindo kama hicho cha Lowassa na hatimaye nguvu zake zilififia na zikapeperuka zisijulikane zilikokwenda. 

Mantiki ya watu kama hao imepindika vibaya sana na haiwezi kusimamia hoja ya kumkebehi Lowassa kwa kusema kwamba nguvu zake ni za upepo uvumao kwa nusu dakika.
Ilivyo ni kwamba Lowassa si Mrema wala Mrema si Lowassa. Kweli kila mmojawao aliwahi kuwa kigogo katika serikali ya Jamhuri ya Muunganowa Tanzania; na kweli wote wawili wamekihama chama kilichowalea cha CCM, lakini si kweli kwamba wawili hao ni sawa.

Huwezi hata kidogo kumlinganisha Mrema na Lowassa. Mrema hawezi kabisa kumfikia Lowassa. Si kwa haiba ya kisiasa, si kwa muono wa kisiasa, si kwa moyo wa kujiamini na wala si kwa uchapaji kazi.

Labda tunachoweza kukubaliana kuhusu wanasiasa hao wawili ni kwamba wao ni watu wenye itikadi moja ya kisiasa. Lakini hivyo ndivyo ilivyo kwa wanasiasa wote wa Tanzania ya leo. Hajatokea bado mwanasiasa mzito mwenye itikadi ya kisiasa iliyo tofauti naya wenzake. Wote wanaicheza ngoma ileile inayopigwa katika miji mikuu ya nchi za Magharibi.

Huo ndio uchungu ambao baadhi yetu tumekuwa tukilala nao na kuamka nao. Hatuna bado kiongozi mwenye falsafa mbadala wala sera mbadala.Wote wanazijenga sera zao juu ya misingi ya falsafa ya ulibirali mamboleo. Hali hii ndio moja ya sababu iliyoifanya Tanzania iwe imeiva kiasi hiki tayari kwa mabadiliko.

Ingawa mabadiliko hayo yataletwa na watu wenye itikadi moja na watawala wa leo, hata hivyo hiyo itakuwa ni hatua moja kubwa ya kuendelea mbele kuelekea mabadiliko halisi ya kimsingi. Mabadiliko yanayotukabili sasa ni muhimu sana kisaikolojia kwa sababu yatatuthibitishia kwamba “panaweza pakapatikana mabadiliko”.

Katika harakati za kuleta mabadiliko ni jambo muhimu sana kuweza kuufanya umma uamini kwamba kisichowezekana kinawezekana.

Miaka michache iliyopita, ni watu wachache waliokuwa wakiamini kwamba panaweza kupatikana watawala wengine badala ya wale watokao CCM. Hii leo umma unaimba nyimbo nyingine kabisa. Na wananchi wakishaona kwamba kweli pamepatikana mabadiliko ya viongozi na kwamba mageuzi yanawezekana, hapo ndipo mchuano halisi wa kisiasa utapoanza. Hapo ndipo patapotokea ukinzani wa dhati wa kiitikadi.

Hiyo ndiyo sababu kubwa inayowafanya wenye kuona mbele wawe tayari kumkumbatia Lowassa. Wanamuona kuwa ni daraja ya kuivuka kufikia kwenye mabadiliko. Mengine, kama wasemavyo, yatafuata baadaye.

Kama nilivyokwishagusia, ni dhahiri kwamba kwa sasa Watanzania wengi wamekwishang’amua kwamba hali ya mambo si lazima iendelee kuwa kama tuliyokuwa nayo kwa muda wa zaidi ya nusu karne. Wanatambua kwamba panawezekana pakawa na njia nyingine ya kufanya mambo, ya kujitawala, ya kuendeshea maisha yao na kujipatia ufanisi.

Ithibati ya niyasemayo ni huu mkondo wa uhamiaji kutoka CCM wa kwenda kuhamia kwenye kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Uhamiaji si wa wanachama wa kawaida tu wa CCM bali hata wa vigogo wa chama hicho. Kama nilivyokwishagusia siku za nyuma uhamiaji huo hautokuwa wa mkupuo mmoja lakini utakuwa wa polepole na utaendelea hadi karibu na tarehe ya upigaji kura.

Vigogo wengine wa CCM wataokihama chama chao bado wamekaa chonjo kwenye viti na mazulia ya CCM wakisubiri wakati muwafaka wa kukusanya virago vyao na kuhamia Ukawa. Wanapohamia huko wanakuwa wanahamia na kumbukumbu nyingi zitazozidi kusaidia papatikane mabadiliko ya uongozi wa taifa.

Tukishakubali kwamba kwa sababu mbalimbali mabadiliko hayana budi kutokea Tanzania, baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, wote wale wenye moyo wa kizalendo wanapaswa kujiandaa kwa jukumu la kusaidia kuyafanya mabadiliko hayo yawe ya maana. Wazalendo wanatakiwa wawe na jukumu la kuhakikisha kwamba mabadiliko yatayopatikana yatakuwa mabadiliko yenye sifa nzuri; ni muhimu kwamba wawe ni wao wataouongoza mkondo wa mabadiliko uelekee kutakoistawisha jamii.

Kuna hatari moja katika hali ya sasa.Ni hatari ya viongozi wenye kuona madaraka yanawaponyoka lakini wasio tayari kukubali kwamba zao zimekwisha. Aghalabu viongozi aina hiyo hupapatika na wanapopapatika huwa tayari kutumia njama zote na uovu wowote ilimradi waweze kuyang’ang’ania madaraka. Haya yamekwishatokea katika nchi mbalimbali duniani na hasa hutokea katika nyakati za uchaguzi.

Hofu ya machafuko na matumizi ya nguvu wakati wa uchaguzi iliibuka hivi karibuni tu huko Sri Lanka. Wiki iliyopita kulifanywa uchaguzi mkuu kwenye kisiwa hicho ambacho mara nyingi kilishuhudia mashambulizi katika chaguzi zilizopita.

Katika uchaguzi wa wiki iiyopita kuna kaulimbiu moja iliyotia fora katika kila sehemu ya kisiwa hicho. Ni ile iliyosema: “Hatutaki matumizi ya nguvu.”

Kaulimbiu hiyo ilizidi kuthibitisha jinsi wananchi hao walivyochoshwa na umwagaji wa damu na hali ya machafuko ya kisiasa yasiyokwisha. Ni lazima wapigakura wa Tanzania na vyombo vya dola viifanye kaulimbiu hiyo iwe yao pia.

Tusisahau kwamba kwa mujibu wa Mkataba wa Roma, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ina mamlaka kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyofanywa katika ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu yeyote anayechochea vitendo vya matumizi ya nguvu au anayeshiriki katika vitendo hivyo katika muktadha wa uchaguzi mkuu ujao anaweza akashtakiwa ama na mahakama ya Tanzania au na Mahakama ya ICC.

Wa mwanzo wenye kuwajibika ni wakuu wa nchi inayohusika. Vyombo vya kisheria vya nchi ndivyo vyenye kuwajibika kuwachunguza na kuwashitaki wote wanaotuhumiwa kwa makosa kama hayo ya jinai. Vikishindwa ndipo Mahakama ya ICC yanapoingia kati, yakalichukua jukumu hilo na kulitekeleza.

Na Mahakama hayo yanaweza yakawashitaki watu binafsi au vikundi vya watu vinavyowashambulia watu kwa sababu za kisiasa kama hizo za wakati wa uchaguzi na hata vyama vya siasa navyo vinaweza kuingia matatani.

Kwa Zanzibar, kwa mfano, vikundi viitwavyo “Janjaweed” na “Ubaya Ubaya” ni vikundi ambavyo kwa wepesi sana vinaweza vikafunguliwa mashitaka licha ya kwamba si vikundi vilivyosajiliwa rasmi. Hata hivyo, wenye kutuhumiwa kuhusika na harakati za vikundi hivyo wanajulikana. Hapo inakuwa kazi ya ICC kufanya uchunguzi wake ndani ya nchi kwa kuwasaili watuhumiwa, kukusanya ushahidi wa mashambulizi au mauaji.

Kwa Zanzibar, kazi hiyo haitokuwa ngumu kwa vile tayari upo ushahidi wa video wa mikutano ya kisiasa ambapo baadhi ya viongozi wanaonekana na kusikika wakitoa matamshi ya uchochezi, pia kuna video na picha watu walioshambuliwa kwa sababu za kisiasa na kuna maelezo ya walioathirika kwa mashambulizi ya aina hiyo.

Vyama vya siasa, asasi za kiraia, jumuiya zinazopigania haki za binadamu na hata watu binafsi wanaweza kuyaandikia Mahakama ya ICC na kuwatuhumu wanaofanya vitendo vya mashambulizi au mauaji kwa ajili ya siasa. Mahakama hayo yanawajibika kuanza kuchukua hatua mara tu baada ya mawasiliano hayo kufikishwa mbele yake. Si kazi kubwa kufikisha mashitaka ingawa mchakato wa kuwafanyia kesi watuhumiwa huenda ukachukua muda mrefu.

Mahakama ya ICC, kwa kawaida, huwashughulikia watu au vikundi vya watu wanaofanya vitendo vya utumizi wa nguvu kabla na wakati wa upigaji kura. Tangu ashike wadhifa wake wa kuwa Mshtaki Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda amekuwa akisisitiza kwamba ameazimia kuwapandisha kizimbani wote wanaotuhumiwa kwa vitendo vya uhalifu wa kijinai wakati wa uchaguzi.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/njia-ya-kufikishwa-icc-ni-fupi#sthash.kClaWWrH.dpuf

No comments :

Post a Comment