Kampeni za Lowassa, ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema, zilikumbana na kikwazo baada ya juzi, Manispaa ya Ilala kudai kuwa imeshaipa CCM haki ya kutumia viwanja hivyo kwa siku hiyo.
CCM ilisema ilikodisha viwanja hivyo kwa siku tatu mfululizo kwa ajili ya kuendesha matamasha ya wasanii.
Lakini jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi alisema baada ya majadiliano baina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ofisi yake, walikubaliana kuwa mkutano huo ufanyike kesho kama ulivyopangwa, huku CCM ikibaki na siku mbili.
Mngulumi alisema viongozi wa CCM waliokuwa na haki ya kutumia uwanja huo wamekubali Chadema waendelee na uzinduzi wao kama walivyopanga.
“Tumekaa pamoja ili kuondoa maneno na tumezungumza na viongozi wa CCM ambao wameafiki kuiachia Chadema siku ya Jumamosi,” alisema Mngulumi.
“Awali, tuliwaomba Chadema wasogeze shughuli yao mbele, lakini wakasema ni lazima waifanye Agosti 29. Hatukuwa na lengo la kuwanyima uwanja ila tatizo lilikuwa kwamba CCM nao walikuwa wameomba.”
Kabla ya Manispaa ya Ilala kutoa tamko hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema chama chake kimesharuhusiwa kutumia viwanja hivyo, maarufu kwa mikutano ya kisiasa na kidini, kama kilivyoomba.
“Mkutano wetu wa uzinduzi wa kampeni upo palepale. Timu yetu tuliyoituma kuzungumza na vyombo husika leo (jana) asubuhi, imetuthibitishia kuwa kila kitu kinakwenda sawa na tumekubaliwa.”
Wakati Chadema ikiruhusiwa kutumia uwanja huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey alisema iwapo CCM wasingekubali kuachia eneo hilo, wangetumia Kifungu cha 40 cha Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ambacho kinaitaka NEC iitishe kikao cha wadau kujadili mgongano huo.
Alisema awali, vyama vyote vilikubaliana ratiba za kampeni zao na Chadema walishaonyesha kuwa wangezindua shughuli zao kwenye wilaya zote za mkoani Dar es Salaam, ingawa hawakutaja uwanja.
Alisema mgongano kama huo ulishatokea Kigoma na baada ya majadiliano, Chadema walikubali kuiachia CCM kuanza kufanya kampeni zake mkoani humo kutokana na NEC kutumia kanuni hiyo.
Hata hivyo, alisema ili kupata kiwanja cha kuzindulia kampeni, Chadema hawana budi kukubaliana na mamlaka za halmashauri husika kwa kuwa NEC haina uwezo huo ingawa kwa mujibu wa sheria, ni chama hicho pekee ambacho kilitakiwa kifanye kampeni zake Agosti 29 jijini Dar es Salaam.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo baadaye jana mchana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wanaotakiwa kutoa ufafanuzi ni uongozi wa mkoa au wilaya wa chama hicho.
Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa, Juma Simba aliwambia waandishi jana mchana kuwa wametumia busara kuwaachia Ukawa ili wazindue kampeni zao.
“Tumesikia malalamiko mengi ya viongozi wa Ukawa kwamba CCM inawahujumu, hii si kweli, tulichokifanya tulituma maombi na kuulipia uwanja wa Jangwani kwa ajili ya matamasha ya wasanii na kampeni za ubunge na udiwani,” alisema.
Alisema chama hicho kilituma maombi Manispaa ya Ilala tangu Agosti 21 na juzi kililipia Sh150,000 na kupewa kibali namba 00012339.
Simba alisema chama hicho hakiiogopi Ukawa kwa sababu ndicho kilichoruhusu mfumo wa vyama vingi nchini.
Msajili wa vyama
Wakati huohuo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amekemea tabia ya baadhi ya vyama kuchezeana faulu na kushutumiana kwenye vyombo vya habari katika kipindi hiki cha kampeni.
Alivitaka vyama vyenye malalamiko dhidi ya vingine kuyapeleka kwenye mamlaka husika na kusubiri uamuzi, badala ya kujibizana kwenye vyombo vya habari.
“Sizungumzii Chadema na CCM, nazungumzia vyama vyote. Kama vitafuata taratibu za uchaguzi zilizowekwa, shutuma hizi hazitakuwapo,” alisema.
Bavicha yatishia maandamano
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi amesema baraza hilo litaongoza maandamano ya vijana nchi nzima iwapo Serikali itaendelea kuminya demokrasia kwa vyama vya upinzani na kuzuia kila jambo analolifanya mgombea urais wa chama hicho, Lowassa.
No comments :
Post a Comment