Manispaa ya Ilala imesema imezuia uzinduzi wa kampeni za Ukawa Jangwani kwa kuwa siku hiyo kutakuwa na shughuli nyingine ya CCM.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.
Siku chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzindua kampeni za mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli, katika viwanja vya Jangwani, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imezuia kuzinduliwa kwa kampeni za mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, katika viwanja hivyo.
Hatua hiyo imechukuliwa huku Ukawa wakisema wamehujumiwa ili wasizindue kampeni zao keshokutwa.
Manispaa hiyo imeeleza kuwa imechukua hatua hiyo kwa kuwa siku hiyo kutakuwa na shughuli nyingine ya CCM.
Lowassa ambaye anawakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya UDP, CUF na NCCR Magezi katika uchaguzi huo, amezuiliwa kuzindua kampeni katika viwanja hivyo kwa madai kuwa uwanja huo utatumiwa kwa shughuli nyingine na CCM.Mwenyekiti mweza wa Ukawa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia, alisema zuio hilo la kutumia uwanja huo limo kwenye barua waliyopelekewa na Manispaa hiyo juzi.
“Jambo la kushangaza ni kuwa, awali tuliomba kufanya kampeni zetu uwanja wa Taifa, lakini tukazuiliwa. Sasa tumeomba kuzindulia viwanja vya Jangwani walikofanyia wenzetu wa CCM, lakini pia tumenyimwa kwa madai kuwa kuna wenzetu wameshaomba kufanyia hapo mkutano, lakini Mgurugenzi wa Ilala ameshindwa kututajia ni chama gani kilicho omba,” alisema Mbatia.
Alisema uamuzi huo umewatatiza kwa sababu wanashindwa kuuelewa na kutafsiri kuwa ni matumizi mabaya ya dola dhidi ya CCM kwa kutumia viongozi na watendaji wake kuzuia kampeni za Ukawa.
Mbatia alisema kabla Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alikaririwa na vyombo vya habari akivitaka vyama vya siasa visivunje taratibu na sheria za uchaguzi.
Alisema pia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alitoa onyo kwa vyama vya siasa kufuata kanuni na taratibu za kampeni ili kuepuka uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu hadi uchaguzi utakapofanyika
.
“Jambo la kusikitisha na ambalo linatugawa Watanzania, chama dola CCM, kilivunja taratibu hizo kwa kuvuka muda wa kampeni hadi saa moja kasoro usiku badala ya kumaliza saa 12 jioni, pia siku ya uzinduzi, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alitumia lugha za matusi, lakini yote hayo yalifumbiwa macho na Nec,” alisema Mbatia.
Alisema kanuni na sheria hizo za uchaguzi pia zilivunjwa kwa kuongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete na kwamba hayo yote wakati yakifanyika Polisi na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki walikuwa katika viwanja hivyo.
MANISPAA YAZUNGUMZIA ZUIO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, alipoulizwa sababu za kuzuia Chadema kuzindua kampeni zake katika uwanja huo, hakuwa tayari kuzungumzia akidai yuko kikazi mkoani Arusha na kwamba Ofisa Utamaduni wa Manispaa hiyo anakaimu wadhifa wake.
Kwa upande wake,Ofisa wa Utamaduni huyo, Claud Mpelembwa, aliliambia Nipashe kuwa Chadema walipeleka maombi ya kutumia uwanja huo kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zake Jumatatu wiki hii na kuwajibu kuwa juzi (Jumanne) CCM wamelikwisha kuomba kufanyia mkutano Jumamosi.
“Hatujawanyima Chadema kutumia uwanja huu, bali tuliwaeleza tayari wameomba CCM tangu awali, isitoshe Chadema wao walichelewa kutuma maombi yao kwani walitoa taarifa Jumatatu ya wiki hii hivyo tuliwataka waombe siku nyingine,” alisema Mpelembwa.
Alifafanua kuwa kwa kawaida wanatoa siku mbili za maandalizi kwa watumiaji wa uwanja huo kwa ajili ya maandalizi na CCM watatumia Agosti 28 na 29 kufanya mkutano wao.
Mpelembwa alisema siku ambazo ziko wazi kutumiwa uwanja huo ni Septemba 3, 4, hivyo Chadema wanaweza kuomba kufanya uzinduzi kwa siku hizo.
“Jambo la kushangaza Chadema walipaswa kuja ofisi kupanga siku ambazo wanaweza kufanya mkutano wao ili tujadiliane, lakini wamekimbilia kwenye vyombo vya habari kulalamika,” alisema Mpelembwa.
UKAWA KUZINDUA KAMPENI JUMAMOSI
Mbatia alisisitiza kuwa licha ya kuzuiliwa bila ya sababu za msingi kuzindua kampeni katika uwanja huo, msimamo wao uko pale pale wa kampeni hizo kuwa kesho kutwa.
Alisema wakati viongozi wa Chadema wakiendelea kufuatialia suala hilo, wanatafuta njia mbadala ya kuzindua kampeni hizo kwa tarehe ile ile iliyoangwa awali.
“Ratiba yetu iko vile vile, tutazindua kampeni zetu Agosti 29 kama tulivyopanga, na tunatarajia kufanya kampeni za kistaarabu za amani na utulivu kwa kutanguliza kwanza mama Tanzania ambaye ni amani,” alisema Mbatia.
WALALAMIKA ZIARA ZA LOWASSA KUZUILIWA
Vilevile, Mbatia alionyesha kushangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kumzua Lowassa kuendelea na ziara alizoanza mwanzoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam, akisema ni kitasababisha uchaguzi mkuu usiwe uhuru na haki.
Alisema wakati kampeni zimezinduliwa, Jeshi la Polisi limemzuia Lowassa kuendelea na ziara za kukagua maeneo mbalimbali jijini humo na kero zinawakabili wananchi.
“Leo Lowassa alipaswa awe katika hospitali ashuhudie changamoto zilizopo, lakini polisi wamemzuia kwa madai hajatoa taarifa... walitaka atoe taarifa gani wakati kampeni zimeanza na pia wakati wanamzuia Mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, yeye alikuwa akifanya ziara katika hospitali mkoani Kilimanjaro?” alihoji Mbatia.
Alionya kuwa endapo Jeshi la Polisi litaendelea kutumiwa na CCM, litambue halitaweza kuzuia nguvu ya umma ambayo inashuhudia vitendo hivyo.
WAMHADHARISHA JAJI LUBUVA
Ukawa umetoa hadhari kwa Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, kutokana na kile ulichodai ni ukimya wake bila ya kutoa tamko kutokana na uvunjwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi unaoendelea dhidi ya umoja huo na wagombea wake.
“Kama Jaji Lubuva atashindwa kuenea kwenye kiti chake basi atambue kuwa historia itamhukumu na nguvu ya umma haitaweza kuzuiliwa pindi itakapoamua kuvunja ukimya,” alisema.
WAPINGA MIONGOZO YA WATENDAJI
Mbatia pia alielezea kupinga maagizo yanayotolewa na viongozi, wakiwamo wakuu wa mikoa, wakurugenzi na wakuu wa wilaya kwa madai kuwa ni watendaji wa CCM.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakitoa makatazo ambayo hayazingatiwi na chama hicho tawala.
“Wakati huu wa kampeni, Jaji Lubuva anapaswa atambue kuwa maagizo yote ya uchaguzi tutayafuata kutoka kwake na kama atatumia viongozi hawa hatutafuata kwani hawa ni watumishi wa CCM,” alisisitiza.
NEC YAJIBU TUHUMA
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Kailima Kombwey, alipoulizwa jana saa 10:59 jioni, alijibu kuwa wanaendelea kufuatilia ili uwanja upatikane kwa ajili ya kuzindua kampeni za Chadema.
Akizungumzia kuhusu malalamiko yaliyotolewa na Ukawa ya kuzuiliwa kwa Lowassa kufanya ziara, alisema hawezi kujibu kwa sababu suala hilo liko mikononi mwa polisi.
Agosti 18, mwaka huu, Idara ya Habari (Maelezo) iliiandikia Chadema barua ya kuzuia kufanya uzinduzi wa kampeni zake zilizokuwa zifanyike Agosti 22 mwaka huu katika uwanja wa Taifa kwa maelezo kuwa uwanja huo ni kwa ajili ya matumizi ya michezo pekee.
Agosti 13 mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, kupitia kamanda wake, Fulgence Ngonyani, lilizuia msafara uliokuwa ukimsindikiza Lowassa kwenye mazishi ya aliyekuwa mwasisi wa CCM, Marehemu Peter Kisumo, kwa maelezo kuwa msafara huo ulikuwa na watu wengi.
Aidha, Agosti 19, Jeshi la Polisi lilitoa zuio kwa vyama vya siasa kurejesha fomu na makundi ya wafuasi wanaowaunga mkono kwa madai ya uvunjifu wa amani kunakotokana na malalamiko yaliyotolewa na wananchi.
Kadhalika, Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), jana ilitoa tangazo katika vyombo vya habari kuzuia matumizi ya helikopta kwenye maeneo ya hadhara na mikusanyiko ya watu.
Taarifa hiyo ilitaja vigezo vinavyotakiwa kufuatwa ni pamoja na cheti cha ndege kwa usalama wa kuruka, taratibu za usalama wa uendeshaji na usalama wa eneo la kutua na kurukia helikopta.
Vingine ni ni usimamizi wa chombo kikiwa ardhini, usalama wa umma, kuchukua, kuangusha vitu ardhini, kupeperusha mabango angani na kutoa taarifa ya matukio.
KUZINDUA KONGAMANO LA BAWACHA
Wakati akikumbana na changamoto hizo, Lowassa ameibuka na mkakati mpya na leo atazindua kongamano la kampeni la Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, alisema jana kuwa wengine watakaozungumza katika kongamano hilo ni mke wa mgombea huyo, Regina, mke wa mgombea mwenza na viongozi wengine wa Ukawa.
Alisema kati ya mambo ambayo Lowassa atayazungumza na wanawake hao, ni kuhusiana na mambo atakayoyapa kipaumbele kama atachaguliwa zikiwamo changamoto wanazokabiliana nazo wanawake katika sekta ya afya.
Pia, kupambana na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu hususani kwa watoto wa kike.
Kadhalika, alisema wake wa wagombea nao watapata fursa ya kueleza malengo mbalimbali waliyonayo ikiwa Ukawa itashinda.
Kwa mujibu wa Mdee, wanawake wenye ulemavu, wachuuzi, wauzaji sokoni, mama lishe, wagonga kokoto, wauza baa, waandishi wa habari, viongozi Bawacha, wabunge na mabalozi wanawake kutoka nchi mbalimbali wamealikwa.
Aliongeza kuwa kongamano hilo litasaidia wanawake hao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa kuwa wao ni wapiga kura wakubwa.
Alisema pamoja na mambo mengine, kongamano hilo linatarajiwa kuimarisha mtandao utakaosaidia kampeni za uchaguzi.
Mdee aliongeza kuwa Bawacha imeunda timu 10 ambazo zitatawanyika katika kanda 10 za Chadema kuzungumza na wanawake kuhusu uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema timu hizo zitaongozwa na wabunge wanawake na wanawake ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu.
SOURCE: NIPASHE
No comments :
Post a Comment