Wafuasi wa Ukawa katika uzinduzi wa Kampeni za Mgombea Urais #CHADEMA viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam leo. Picha na Mwananchi Digital
Dar. Baada ya kusubiri kwa takribani wiki moja, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wazindua kampeni zao jijini Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alimkabidhi Ilani ya Ukawa, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa.
Akiwanadi wagombea hao, Mbowe alisema wamemchagua Lowassa kupeperusha bendera ya Ukawa kwa kuwa wanaamini atawaunganisha Watanzania wa kada mbalimbali katika kuwaletea maendeleo.
Akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alitumia muda mwingi kumsafisha Lowassa, huku akitupa shutuma nyingi kwa serikali kuwa imekuwa na vitendo vingi vya ufisadi hata baada ya kujiuzulu kwa Lowassa.
Huku akishangiliwa, Sumaye alitolea ufafanuzi hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa dhidi ya Lowassa, ikiwepo suala la afya ya Lowassa, huku akibainisha kuwa viongozi wote waliotangulia walikuwa na shida za kiafya.
Akizungumza katika uzinduzi huo, mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema watahakikisha nchi inapata katiba inayokubaliwa na wananchi endapo watachaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema wataunda tume ya maridhiano kuwaunganisha Watanzania waliosambaratishwa na Itikadi mbaya za CCM huku akibainisha kuwa watajali maisha ya wanawake wa Tanzania waliosahauliwa na serikali ya CCM.
Mgombea urais Edward Lowassa alisema watatekeleza Ilani yao ya uchaguzi iliyotoa kipaumbele katika elimu ili kulifanya taifa liweze kupiga hatua kwa kasi.
Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kilimo, kuboresha huduma za afya, kuboresha miundombinu kwa kujenga reli ya kati na kufufua Shirika la ndege.
No comments :
Post a Comment