NA EDITOR
28th August 2015
CCM ilifanya uzinduzi wa kampeni zake katika viwanja vya Jangwani, Ilala jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea mikoani kutangaza sera zake kwa wananchi ambao Oktoba 25, mwaka huu watakuwa na dhamana ya kuamua kwa kupiga kura.
Hata hivyo, awali kabla ya CCM kufanya uzinduzi wake, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa); Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, viliomba kibali cha kufanyia uzinduzi wa kampeni katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Lakini Idara ya Habari Maelezo, Agosti 18, mwaka huu ilikiandikia Chadema barua ikitoa zuio kwa maelezo kuwa kiwanja hicho ni kwa ajili ya michezo tu, jambo ambalo lilizua maswali mengi kwani mara kadhaa uwanja huo umekuwa ukitumika kwa matukio mbalimbali ikiwamo mikesha ya mikutano ya injili.
Lakini Idara ya Habari Maelezo, Agosti 18, mwaka huu ilikiandikia Chadema barua ikitoa zuio kwa maelezo kuwa kiwanja hicho ni kwa ajili ya michezo tu, jambo ambalo lilizua maswali mengi kwani mara kadhaa uwanja huo umekuwa ukitumika kwa matukio mbalimbali ikiwamo mikesha ya mikutano ya injili.
Hatua hiyo iliwafanya Ukawa, Agosti 22, mwaka huu kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuomba kibali cha kufanyia uzinduzi wao wa kampeni katika viwanja vya Jangwani wakiamini kuwa, eneo hilo linaweza kutosha kubeba umati unaohitaji kusikiliza sera zao kama ilivyokuwa kwa CCM.
Hata hivyo, ofisi ya mkurugenzi wa manispaa hiyo, Agosti 25, ilimjibu katibu mkuu wa Chadema kuwa maombi ya kutumia uwanja huo hayakupewa nafasi kwa kuwa utakuwa na matumizi kwa muombaji mwingine, ambaye alidaiwa kuwa ni CCM. Hatua iliyowafanya Ukawa kufikisha malalamiko yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kabla ya jana kuruhusiwa rasmi kutumia viwanja hivyo.
Tunatambua kuwa eneo hilo ni la serikali na kipindi hiki hakuna shughuli inayopaswa kupewa kipaumbe katika viwanja hivyo na vingine mikoani kama kampeni za urais kwa vyama vyote. Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba CCM ambayo imemsimamisha Dk. John Magufuli katika nafasi ya urais, huku Ukawa wakimsimamisha Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa, wawili hao wanaushawishi mkubwa wa kuvuta umati mkubwa, hivyo kuhitajika eneo kubwa na la wazi ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kama vifo kutokana na msongamano mkubwa wa watu.
Kumekuwapo pia na taarifa kuwa CCM imepanga kuwaminya Ukawa kwa kutumia kigezo chake cha kuwa madarakani na kumiliki viwanja vingi, hivyo kuhakikisha wapinzani wanakosa viwanja vya kufanyia kampeni watakapoanza kuelekea mikoani.
Tunasema hilo halikubaliki kwa kuwa kwa kufanya hujuma mbaya kama hizo, ni kucheza na maisha ya watu, kwani ushawishi wa Lowassa kama mkutano wake wa kampeni utafanyika katika eneo finyu ni wazi kuna hatari ya vifo vitakavyosababishwa na msongamano wa watu.
Viwanja hivyo ni mali ya Watanzania wote kwani vilijengwa kabla ya kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi, hivyo CCM haina budi kutambua kuwa, wananchi wanahitaji kujitokeza kwa wingi katika kampeni hizo ili Oktoba 25 waweze kufanya uamuzi sahihi.
Kadhalika Nec inapaswa kutenda haki kwa kusimamia mchakato huo ili kuwawezesha wananchi kuweza kupima sera za wagombea wa vyama vyote, wakati huo huo Jeshi la Polisi nchini nalo likitekeleza wajibu wao wa kuwalinda wananchi na kutoegemea upande wowote.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment