Juu: Mzee Vijisent (Chenge) na Prof Tibaijuka ambae kila mmoja alipewa TShs 1.6 billion kutoka Escrow Account!
Ufisadi na rushwa ni agenda kuu kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao, Oktoba 25 mwaka huu, kwa vyama vya Upinzani na kwa chama tawala CCM, vikidai ni janga la Taifa.
Tatizo ni kwamba, wale wanaopaswa kupambana na janga hilo, wao wenyewe mikono yao imechafuka kwa damu ya rushwa. Utamaduni wa kuwajibika na kuwajibishana umetoweka; huku vigogo watuhumiwa wakiendelea kudunda madarakani kwa kulindwa na kufichiwa maovu.
Katika kinyang’anyiro kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, tunaona kila chama na kila mgombea urais anarudia wimbo ule ule na kwa wasikilizaji wale wale kwa kupepesa macho akielewa hiyo ni danganya toto, kwamba baada ya uchaguzi itakuwa mdundo ule ule.
Mbaya zaidi, wagombea wote wamekulia na kushika madaraka kwenye mfumo huo wenye kuatamia rushwa, wao kama sehemu ya kundi dogo lenye kuneemeka na mfumo huo. Leo ujasiri wa kutokomeza rushwa watautoa wapi wakati ni washiriki na wanufaika wakuu tangu mwanzo? Kama si unafiki na ulaghai, ni nini?
Rushwa na ufisadi mkubwa vilianza na Serikali ya Awamu ya pili [1985 – 1995] kufuatia kupigwa ngwara Azimio la Arusha kwa Azimio la Zanzibar [1992] kwa kutukuza sera za soko huria, uwekezaji na ubinafsishaji usiojali, ufisadi mkubwa wa kwanza ukiwa ni ule wa Mkataba wa uwekezaji katika Sekta ya umeme, kati ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd [IPTL] na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) katika mkataba wa maelewano (MoU) uliofikiwa mapema mwaka 1994.
Chini ya Mkataba huo wa kilaghai, serikali imebebeshwa mzigo wa kulipa Sh. 5.6bn/= kwa mwezi kama “capacity charges” kwa mitambo mkweche ya IPTL, mbali na gharama za umeme zilizoongezwa kilaghai maradufu, tena kwa umeme wa kusuasua.
Na ingawa Mahakama ya Kimataifa ya Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ya mjini London, ilibaini kuwa ongezeko hilo halikuwa halali na haramu, na kwamba TANESCO ilistahili kurejeshewa; kinyume chake, fedha za tozo hilo haramu (zaidi ya bilioni 320/=) ambazo zilifunguliwa Akaunti maalum “IPTL Tegeta Escrow Account”, zimelipwa kifisadi kwa IPTL hao hao na kuzua ghadhabu ya Bunge na umma kwa ujumla, na kufanya mawaziri wawili waandamizi na mwanasheria mkuu wa serikali kujiuzulu mwaka huu vigogo huku wengine kuendelea kuchunguzwa na Tume ya Maadili.
Ufisadi mwingine ni ule wa uwekezaji wa Benki ya kigeni Meridian Biao, iliyodhaminiwa na Benki Kuu (BOT); kwamba, mwaka 1995 ilipowapora wateja wake zaidi ya 54bn/= na kutoroka, serikali ililazimika kulipa kwa fedha za umma.
Hatujasahau kuporwa kilaghai na mfanyabiashara mmoja zaidi ya 150bn/= za “Mpango wa Kununua Madeni (Debt Conversion Programme) mwaka 1994, ambapo kesi dhidi yake inaelekea kufutwa kimya kimya, baada ya mtuhumiwa, mwenye uraia wa nchi mbili kuruka dhamana.
Ufisadi mwingine mkubwani ule wa BOT [EPA] ambapo 133bn/= ziliporwa, kisha ya Rada (70bn/=), ujenzi wa majengo pacha ya BOT (600bn/=), Richmond, Meremeta; na bila kusahau mikataba mibovu lukuki iliyoingiwa, yenye kupora fedha na rasilimali za Taifa.
Kashfa ya Richmond ilisababisha kujiuzulu kwa kuwajibika, aliyekuwa waziri mkuu wakati huo, Edward Ngoyayi Lowassa, mwaka 2008 akidai kufanya hivyo ili kulinda chama na heshima ya nchi; na hivyo kufanya vigogo wengine waliokuwa nyuma ya kashfa hiyo kusalimika kwa mmoja huyo kukubali kufa ili wengine wapone. La Meremeta litaelezwa kipekee hivi punde kwa sababu ya uzito wake.
Ufisadi ulivamia pia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Wafanyakazi wanyonge wa nchi hii. Mfano mmoja; mwaka 2005, mfanyabiashara mmoja mashuhuri alikopeshwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii 9bn/= kwa ajili ya kukarabati maghala. Baada ya kufanya hivyo aliuzia Mfuko maghala hayo hayo kwa 47bn/=.Vivyo hivyo, aliuuzia mwingine maghala matatu kwa bei ya 39bn/=, zaidi ya mara tatu ya thamani halisi. Ufisadi aina hii kwa mifuko hiyo, ambayo sasa ni hoi bin taabani kifedha, haujakoma.
Ufisadi huu, ukiwamo ule wa Tegeta Escrow Account, umefanyika mikononi mwa wengi wa wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi hivi leo, ambapo baadhi ya watiani wa urais walioshindwa kuvuka ngazi ya uteuzi na kugeukia ubunge, wametajwa kupokea milungula, lakini bado vyama vyao vimewapitisha kana kwamba ni watu safi!
Ufisadi ulikithiri kufikia kutumia jina la “Usalama wa Taifa” katika kuficha maovu, uporaji na kwa wahujumu uchumi wa Taifa kulindwa wasiguswe kwa kisingizio hicho, kama ilivyotokea kwa mradi wa Meremeta, Deep Green na Tangold, tutakavyoona hivi punde.
Kuna mfanano mkubwa wa ukwapuaji fedha katika mazingira yanayojirudia nchini, kati ya kashfa ya Akaunti ya Escrow ya IPTL, Tegeta, EPA na kashfa ya Meremeta. Na ingawa Bunge lilikwishaagiza hesabu za Kampuni hiyo ziwasilishwe kwa CAG zikaguliwe, bado kuna “mgomo” kwa upande wa Serikali kiasi kwamba, aliyekuwa CAG wakati huo, Ludovick Utoh, amestaafu akilalamika kutopelekewa hesabu hizo, kuonyesha kwamba kuna “Hiroshima” inayoweza kwenda na wengi na hivyo lazima kuwe na kulindana.
Kisingizio cha awali kilikuwa kwamba, “Meremeta” ulikuwa mradi wenye kuhusisha mambo ya “Usalama wa Taifa”, na hivyo eti kwamba uendeshaji wake usingewekwa hadharani.
Kwa kioja hiki ilidaiwa kuwa, Kampuni ya Meremeta iliandikishwa na kusajiliwa nchini Uingereza (Kisiwa cha Isle of Man), Agosti 9, 1999 kwa nambari ya Usajili 3424504. Lakini katika hali inayokanganya, Serikali inadai, Meremeta ni ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 50, na Kampuni ya Trinnex ya Afrika Kusini inayomiliki asilimia 50 za hisa, lakini bila kutaja nambari ya Usajili.
Tunaelezwa, madhumuni ya Meremeta yalikuwa ni kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo nchini pamoja na kuwasaidia zana za kufanyia kazi. Mkanganyiko unaongezeka pale tunapoambiwa kwamba, makampuni mengine mawili – The London Law Service Ltd na The London Law Secretarial Ltd, nayo ni wanahisa wa Meremeta.
Ni kwa vipi kampuni inayomilikiwa na serikali kwa asilimia 50 na yenye kuhusisha mambo ya Usalama wa Taifa, isajiliwe katika nchi ya kigeni, London, Uingereza?
Kati ya mwaka 2003 na 2005 Meremeta, tofauti na madhumuni ya kuanzishwa kwake, ilijiingiza katika uchimbaji wa dhahabu moja kwa moja huko Buhemba, Musoma, na kuibuka na madhumuni mapya ya kusaidia kiwanda cha magari cha Kijeshi, Nyumbu, kilichopo Mkoa wa Pwani; wakati haikuwa kweli. Tunajua, kati ya mwaka 2003 na 2005, Kiwanda cha Nyumbu kilipangiwa kutumia 950m/= kwa ajili ya kutengeneza magari 21 tu ya Kijeshi kwa wastani wa 45.2m/= kwa kila gari na hakukuwa na fedha yoyote kutoka Meremeta wala mahali pengine.
Kile tu kwamba “Mradi” wa Meremeta ulijengwa mahali ambapo zamani ilikuwa Kambi ya Jeshi, hakifanyi uwe Mradi wa Jeshi kuweza kuhusishwa na Usalama wa Taifa. Na hili liliwekwa wazi na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wakati huo, Profesa Philemon Sarungi, katika hotuba yake ya bajeti ya 2004/2005 aliposema: “Mradi wa Buhemba umejengwa kwenye eneo ambalo zamani ilikuwa Kambi ya Jeshi; shughuli za uchimbaji na uzalishaji zinasimamiwa na Idara ya Madini”, alitamka.
Ukweli ni kwamba, Mgodi wa Buhemba ulijengwa na Kampuni ya WBHO[Pty] Ltd ya Afrika Kusini, kwa niaba ya Meremeta na Triennex (Pty), kwa rand milioni 240 (dola 56m) na ujenzi huo ulikamilika mwaka 2000. Ulizihusisha pia kampuni za kigeni za Jefferies and Green na Time Mining, zote za Afrika Kusini.
Mmoja wa wanahisa wakubwa wa Time Mining alikuwa Anna Muganda, mke wa aliyekuwa Gavana wa BOT, Daudi Balali, ambaye (Balali) ndiye aliyeileta kampuni hiyo nchini kusimamia na kuendesha Mgodi wa Meremeta kwa niaba ya “Serikali” ya Tanzania.
Kioja kingine ni kwamba, wengi wa watumishi wa nje (expatriates) wa Kampuni ya Alex Stewarts ya mjini Washington, iliyoletwa nchini na Balali kukagua mauzo ya dhahabu ya makampuni nchi za nje, ndio hao hao waliokuwa watumishi pia wa Kampuni ya Anna Muganda, Time Mining. Hapo, Usalama wa Taifa unaingiaje? Na Daudi Balali alikuwa na mamlaka gani kuajiri kampuni binafsi ya Alex Stewarts kukagua mauzo ya dhahabu ya Serikali; na kwa manufaa ya nani?
Ikumbukwe kuwa, mawaziri wawili waandamizi wa serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin William Mkapa, waziri wa fedha, Basil Pesambili Mramba na waziri wa nishati na madini, Daniel Yona; wamehukumiwa kifungo kwa kosa la kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni tata hiyo ya Alex Stewarts kwa Meremeta, lakini bila Serikali kutaka kutaja maovu ya waovu waliohusika na mradi huo. Mramba na Yona wametolewa kafara “kufunika kombe mwanaharamu apite” ili wengine wapone.
Meremeta ilipokomba dhahabu yote huko Buhemba, Buhemba Kusini, Nyamongo na Magunga, mwaka 2006 ilijitangaza kuendesha shughuli kwa hasara; ikaundwa “Tume” ya Serikali kuchunguza matatizo ya Kampuni hiyo!. Waliokuwa kwenye “Tume” ni Daudi Balali – gavana wa BOT na Mwenyekiti wa Tume; Gray Mgonja (katibu mkuu, wizara ya fedha] na Patrick Rutabanzibwa (Katibu Mkuu, Nishati na Madini).
Wengine walikuwa ni Vincent Mrisho (katibu mkuu, ulinzi na JKT), Andrew Chenge (mwanasheria mkuu wa serikali na Michael Garner, kama mshauri wa Tume na Mshauri pia wa Benki ya Nedbank, yenye uhusiano wa kikazi na Kampuni ya Nedcor Trade Services iliyochota 155bn/= kutoka BOT katika mazingira ya kutatanisha.
Tume hiyo ilipendekeza kutambua kwa kuridhia, Meremeta kusitisha tangu mwaka 2003 shughuli zilizotajwa katika madhumuni ya kuanzishwa kwake, na badala yake ikaridhia shughuli mpya ya uchimbaji na umiliki wa migodi tangu mwaka huo na kuendelea.
Tume pia ilipendekeza kuanzishwa kwa kampuni mpya ya kusimamia na kuendesha Mgodi wa Buhemba kwa kumilikiwa na Serikali asilimia mia. Na kwa uzito wa mapendekezo ya Tume hiyo ya Balali, Meremeta ilifilisiwa; mali na madeni yake yakarithishwa Serikali kupitia Kampuni mpya iliyoundwa, TANGOLD.
Ingawa inadaiwa Meremeta ilifungwa rasmi mwaka 2006 nchini Uingereza, lakini shughuli zake hazikukoma nchini mwetu. Hapa kuna utata: Kumbukumbu zinaonesha “Tangold” ilianzishwa na kusajiliwa kwenye Visiwa vya Mauritius, Aprili 4, 2005 na kupewa Leseni ya Biashara Aprili 8, 2005 kama Kampuni binafsi.
Wakati huo huo, kumbukumbu nyingine zinaonyesha “Tangold” ilifungua Akaunti ya Benki, Namba 011103024852, Tawi la Corporate la NBC, Dar Es Salaam, Januari 1, 2003; kabla hata Tume ya Balali haijaundwa, licha ya kwamba siku hiyo ilikuwa ya Mapumziko ya Sikukuu ya Mwaka mpya ambapo Benki hazifanyi kazi.
Taarifa nyingine zinaonyesha, “Tangold” ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa nchini Mauritius na kupewa Leseni ya Biashara nchini Tanzania, Februari 20, 2005 kama Tawi la Kampuni ya kigeni, na kuanza kupatiwa fedha na BOT, Agosti 1, 2005 kwa huduma zisizojulikana.
Hii ni kusema kwamba, “Tangold” ilikuwapo nchini tangu Januari 2003 kabla ya kuanzishwa kwake nchini Mauritius mwaka 2005. Kama hivyo ndivyo, kwa nini Tume ya Balali ilipendekeza kuanzishwa kampuni ambayo tayari ilikuwepo? Je, kuna tofauti kati ya “Tangold” iliyofungua Akaunti Benki, Januari 1, 2003 na kuanza kuchota fedha; na “Tangold” iliyosajiliwa Mauritius Aprili 4, 2005 kurithi Meremeta?
Kituko kingine ni kile cha baadhi ya Wajumbe wa Tume ya Balali iliyochunguza matatizo ya Meremeta, kuteuliwa (kujigeuza?) kuwa Wajumbe wa Bodi ya “Tangold”. Hao walikuwa ni mabwana Daudi Balali, Gray S. Mgonja, Andrew Chenge, Patrick J.W. Rutabanzibwa na Vincent Mrisho.
Inawezekana kwa mtazamo huo, hao ndio walikuwa “Serikali” yenyewe yenye kumiliki asilimia kwa mia ya hisa!
Lakini ibara ya 7 ya Katiba ya Tangold ilimaanisha kuwa na wamiliki binafsi [na si Serikali] na kwamba, “Wenye hisa kwenye kampuni wanaweza kurithisha hisa zao kwa ndugu zao”. Ni ndugu wapi hao wa Serikali wanaoweza kurithishwa hisa za Serikali? Je, Serikali ina ndugu binafsi?
Kwa kifupi, sakata la ufisadi huu, toka kuundwa kwa Meremeta hadi kufilisika kwa “Tangold”, kuliligharimu Taifa fedha za wavuja jasho zaidi ya 526bn/=, zikiwamo155bn/= zilizochotwa moja kwa moja na Kampuni ya Nedcor Trade Service kutoka BOT. Serikali ya awamu ya Tatu, ilifanya malipo hayo kimya kimya, Oktoba 2005, mwezi mmoja tu kabla ya kuondoka madarakani.
Mwananchi wa kawaida amechoshwa na ngonjera za ulaghai huu wa kujirudia. Na ili kurejesha imani ya wananchi na Wafadhili wema kwa Serikali na mfumo wa utawala, anahitajika Rais jasiri atakayefufua na kuzishughulikia kashfa hizi, na wananchi waone dhahiri kwamba kweli anakerwa na uozohuo. Ni nani Rais aina hiyo ajaye?
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tunataka-rais-jasiri-atakayefufua-kashfa-za-ufisadi-huu#sthash.kBXhg0y9.dpuf
No comments :
Post a Comment