
Akizungumza na Nipashe Ofisa Sheria wa kituo hicho, Hussein Sengu, alisema waangalizi hao watakuwa wanatoa taarifa mara kwa mara juu ya matukio yanajitokeza katika kila eneo la nchi kuhusu kampeni zinazoendelea.
Kadhalika, alisema kama kituo kinachosimamia haki za binadamu, wamebaini kwamba kumeanza kujitokeza baadhi ya matukio kwenye kampeni za uchaguzi zinazoendelea.
Aidha, alisema kituo hicho kinalaani vikali vitendo vya mauaji ambavyo vimeanza kujitokeza vinavyosababishwa na kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa akitolea mfano wa tukio la mauaji lilitokea mkoani Mara hivi karibuni.Alisema ni vema wanasiasa na vyama vyao, wakazingatia maadili ya uchaguzi waliyojiwekea kwani bila kufanya hivyo ni kukiuka haki za binadamu.
“Kumeanza kujitokeza dosari za hapa na pale kwenye uchaguzi wa mwaka huu katika kampeni za vyama mbalimbali zinazoendelea nchi nzima. Watu wameanza kuuana, kutukanana badala ya kuzungumza sera zao. Ni vema wakazingatia maadili waliyojiwekea,” alisisitiza Sengu.
Aliongeza: “Lazima watambue kwamba uchaguzi ukimalizika, Tanzania lazima ibaki na maisha yataendelea.
Tunachokiomba wasiwadhuru watu kwa sababu ya kukosa uvumilivu wa kisiasa na katika hili, tunaomba vyombo husika viliangalie ili ikiwezekana wanasiasa au vyama vitakavyoonekana kuendeleza ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi, viondolewe katika uchaguzi.”
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment