
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilisema Jeshi la Polisi limefuatilia kwa kina na kumkamata mtuhumiwa huyo Oktoba 2, mwaka huu mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, taratibu za kumhoji mtuhumiwa huyo zinafanywa na Jeshi la Polisi pamoja na upelelezi wa kina kuhusiana na suala hilo.
Septemba 26, mwaka huu, wizara hiyo iliwaita waandishi wa habari kukanusha uzushi huo uliokuwa unaenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Mwamunyange amenusurika kifo baada ya kulishwa chakula chenye sumu.
Aidha, Wizara na Jeshi kwa ujumla, liliahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika kumsaka mtu huyo aliyeeneza uzushi huo kama hataonyesha ustaarabu wa kuomba radhi.“Baada ya kuendelea kupokea simu mbalimbali kutoka kwa baadhi yenu mkitaka kujua maendeleo ya kumsaka `kanjanja, huyo, tumeona ni busara kuwafahamisha hatua iliyofikiwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, amesema afya ya Jenerali Mwamunyage ni nzuri.
Hata hivyo, Mwambene alikataa kueleza mahali alipo Jenerali Mwamunyange kwa sasa.
“Jenerali Mwamunyange hajapewa sumu kama ilivyodaiwa kwenye mitandao ya jamii, naomba wananchi wazipuuze taarifa hizo,” alisema.
Aidha, Mwambene alisisitiza kuwa taarifa zilizoenea kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, amefariki dunia, siyo za kweli bali anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu.
Alisema serikali itavichukulia hatua za kisheria vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii viliyohusika kueneza taarifa hizo na kukiuka sheria ya uandishi wa habari.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment