
Rais Jakaya Kikwete akihutubia Bunge la Kitaifa la Kenya na lile la Seneti jijini Nairobi jana. Picha na NMG
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameliambia Bunge la Kenya kuwa ana uhakika mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli atashinda na kwamba ataimarisha zaidi ushirikiano baina ya Tanzania na Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati akilihutubia bunge la pamoja la kitaifa na lile na seneti na kusisitiza kuwa amebakiza siku 18 tu kabla ya kumaliza kipindi chake cha pili cha urais kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Rais Kikwete alisema, “Nitaondoka madarakani nikiwa na furaha kwa kuacha uhusiano mzuri baina ya Kenya na Tanzania, kuliko wakati wote katika historia.
“Ninawahakikishia hata mimi baada ya kuondoka sera (ushirikiano) hiyo haitabadilika, labda tupate mtu mpumbavu na wa ajabu, lakini watu wa aina hiyo wapo wachache kwetu.
“Kama akipata mgombea wa chama changu (Magufuli) na nina uhakika atapata, mambo yatakuwa mazuri zaidi.
“Amenituma na ataelezea msimamo wake kuhusu EAC na kuhusu uhusiano na Kenya baadaye leo (jana) kwenye mkutano wake wa kampeni mjini Arusha. Lakini amesema niwahakikishieni Mungu akimsaidia akashinda, atadumisha na kuendeleza uhusiano uliopo kati ya nchi zetu mbili ili uwe mzuri zaidi.”
Katika hotuba yake aliyoitoa kwa Kiingereza na Kiswahili na kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha KBC, Rais Kikwete alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili na Afrika Mashariki kwa jumla.
“Tunaamini kama nchi zetu za Afrika Mashariki hazitashirikiana, uwezo wetu wa kushindana katika masoko ya kanda na dunia utakuwa mdogo sana.
“Kwa hiyo, sisi wakati wote tutaunga mkono ajenda ya utangamano wa EAC na tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba ajenda hiyo inatekelezwa kama vile tulivyokubaliana.
Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema ni faraja kuona Kenya ina moyo huo huo.
“EAC ndiyo chombo chetu na sote tukisadie kiweze kustawi na kufanikiwa. Sisi Tanzania ni waumini wa utengamano wa kikanda, kwetu sisi ni sera na ni jambo la msingi,”alisema.
Rais Kikwete ambaye alikuwa Kenya kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais, Uhuru Kenyatta alisema nchi hiyo imewekeza zaidi Tanzania.
No comments :
Post a Comment