Wakati Magufuli alikuwa mkoani humo katika mkutano wa kufunga kampeni zake za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Lowassa alikuwa jijini Dar es Salaam alipohitimisha katika viwanja vya Jangwani.
Wagombea hao wamekuwa na ushindani mkubwa katika kampeni zao na kuufanya uchaguzi wa leo kuwa wenye kutegemea uamuzi mgumu.
Wakati wawili hao wakielekea Monduli na Chato, taarifa kutoka ACT-Wazalendo zilieleza kuwa mgombea wake, Anna Mghwira atapigia kura mkoani Singida.
Kwa upande wake, mgombea urais kwa tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP) Macmillan Lyimo, atakuwa Njia Panda ya Himo mkoani Kilimanjaro.
WAGOMBEA WATATU ‘KUBANANA’ DAR
Wagombea watatu Fahmi Dovutwa (UPDP), Hashim Rungwe (Chaumma) na Chifu Litayosa Yemba (ADC), watapiga kura kwenye vituo tofauti jijini Dar es Salaam.
Dovutwa atapiga kura katika kituo cha Kagera kilicho karibu na ofisi ya UPDP wakati Rungwe, atakuwa kwenye kituo cha Shule ya Msingi ya Ushindi iliyopo Mikocheni B na Chifu Yemba atapigia maeneo ya Buguruni.
DK SHEIN, MAALIM SEIF KUBAKI UNGUJA
Wagombea urais wa Zanzibar wenye ushindani wa karibu, Dk. Ali Mohammed Shein (CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) watapiga kura zao kisiwani Unguja.
Wote wawili wanaiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini wakiwa na asili ya kutokea kisiwani Pemba.
Taarifa kutoka Zanzibar zimeeleza kuwa Dk Shein atapiga kura kwenye Skuli ya Kibele wilaya ya Kusini Unguja wakati Maalim Seif atakuwa kwenye kituo cha Skuli ya Garagara wilaya ya Magharibi A, Unguja.
Wagombea wengine na skuli zenye vituo watakavyopiga kura kwenye mabano ni Issa Mohammed Zonga wa SAU (Kijitoupele), Juma Ali Khatib wa TADEA (Kiembe Samaki).
Wengine ni Khamis Iddi Lila wa ACT Wazalendo (Kilimani), Kassim Bakar wa Jahazi Asilia (Karakana), Mohammed Masoud Rashid wa CHAUMMA (kituo cha Salama Holi Bwawani).
Pia wapo Said Soud Said wa AFP (Wawi-Pemba), Tabu Mussa Juma wa Demokrasia Makini(skuli ya biashara iliyopo Mombasa), Ali Khatib Juma wa CCK (Kijitoupele) na Hamad Rashid Mohammed wa ADC (Wawi-Pemba).
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment