25th October 2015.
Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni fursa ambayo ilisubiriwa na Watanzania kwa hamu ili kuwapata viongozi wa awamu ya tano kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani.
Viongozi watakaopatikana baada ya uchaguzi huu ndio watakaoliongoza taifa hili la Tanzania kwa miaka mitano ijayo, kabla ya kufanyika uchaguzi mwingine unaotarajiwa mwaka 2020.
Uongozi tunaouchagua leo utakuwa wa awamu ya tano tangu nchi hii ijipatie uhuru wake mwaka 1961.
Tofauti na chaguzi zilizopita, uchaguzi wa mwaka huu una mwitikio mkubwa wa wananchi kuanzia uandikishaji katika Daftari la Mpigakura.
Uchaguzi wa mwaka huu pia umekuwa na changamoto kubwa kutokana na ushindani kuwa mkubwa hasa kati ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Changamoto nyingine ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, vyama vya upinzani vinne kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais anayepambana na mgombea wa chama tawala.
Vyama hivyo ni Chadema, Chama cha NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (Cuf) na Chama cha National League for Democrasy (NLD).
Ushabiki wa wapambe wa wagombea hao umefanya mikutano mingi ya kampeni za wagombea hasa wa urais kuwa na idadi kubwa ya wananchi huku kila upande ukitamba kuvuna wapigakura wengi.
Historia nyingine iliyojiandika katika uchaguzi huu ni ya chama kipya cha siasa cha ACT-Wazalendo, kumsimamisha mgombea pekee wa urais mwanamke, anayepambana na wanaume saba.
Wagombea wengine wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mackmilian Lyimo (TLP), Fahmi Dovutwa (UPDP), Hashim Rungwe (Chaumma), Janken Kasambala (NRA) na Lutasola Yemba (ADC).
Wananchi wamepata fursa ya kumsikiliza kila mgombea na sera zake na kila mmoja atakuwa amefanya maamuzi yake ya kumchagua kiongozi anayeona anafaa kuiongoza Tanzania.
Sababu nyingine zilizohamasisha msisimko wa kisiasa mwaka huu ni pamoja na maamuzi ya baadhi ya viongozi waandamizi wastaafu wa serikali na chama cha CCM, kuhamia vyama vya upinzani.
Idadi ya waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje imeongezeka katika uchaguzi wa mwaka huu ili wawe mashahidi wa kuieleza dunia uchaguzi unavyofanyika nchini kwetu.
Katika kipindi chote cha kampeni, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali wamekuwa wakiomba na kuwahimiza wananchi wote kudumisha utulivu na amani, wakati wa kipindi cha kampeni, kupiga kura, kuhesabu kura na wakati wa kutangaza matokeo.
Ni wajibu wetu kuhakikisha wote tunafuata taratibu na sheria zilizowekwa na mamlaka husika kuepusha mitafaruku.
Tunaamini kila mwananchi ameshafanya maamuzi ya nani atampa kura yake, na baada ya kukamilisha mchakato wa kupiga kura kila aliyehusika atakuwa na shauku ya kutaka kujua matokeo ya washindi, inawezekana hicho kikawa kipindi kigumu kuliko wakati mwingine wowote.
Juzi, Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na waangalizi wa kimataifa Ikulu, jijini Dar es Salaam, aliwahakikishia kuwa uchaguzi huu utakuwa na amani na utulivu kupita chaguzi zote zilizopita.
Waangalizi walifika Ikulu kujitambulisha kwa Rais kuwa wapo nchini kwa ajili ya kuangalia uchaguzi unavyokwenda kwa kuzingatia amani na utulivu.
Tunaamini kuwa tofauti zilizojengeka miongoni mwa wafuasi wa vyama mbalimbali wakati wa kipindi chote cha kampeni hadi leo siku ya kupiga kura, ni masuala ya mpito.
Historia na maadili yetu yanabaki kutuweka katika undugu, umoja na mshikamano wa kitaifa, tukiamini kuwa kipaumbele cha matarajio ya wananchi ni namna ya kujinusuru kiuchumi na kuendeleza jamii katika nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku.
Tunawasihi wananchi kudumisha amani na mshikamano wakati wa kipindi hiki tunachosubiri kuwapata viongozi katika ngazi za urais, ubunge na udiwani ili taifa letu liendelee kuwa moja na na lenye mshikamano.
Tukumbuke kuwa yeyote atakayetangazwa kuwa mshindi, ndiye atakayekuwa rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi yoyote ile.
Pia inatupasa kujua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo tuendelee kudumisha amani, upendo na umoja.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment