dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 20, 2015

Lowassa amvaa Mwakyembe, Magufuli akomaa Kanda ya Ziwa.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amemvaa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa kuwataka wananchi wa Jimbo la Kyela wasithubutu kumchagua huku mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli akiendeleza mapambano kwenye maeneo ya Kanda ya Ziwa kuhakikisha kuwa anavuna kura nyingi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili wiki hii.
 
Akihutubia maelfu ya watu kwenye viwanja vya Takoshiri, wilayani Kyela jana, Lowassa anayewakilisha pia ushirikiano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF), alisema wananchi wa Kyela wana bahati mbaya ya kuchagua wabunge wasiowasaidia na hivyo,  adhabu inayostahili kwa mbunge wa sasa Dk. Mwakyembe, ni kuhakikisha kwamba wanamnyima kura na kumchagua Abraham Mwanyamaki anayepeperusha bendera ya Ukawa.
 
Hata hivyo, Lowassa hakumtaja Mwakyembe moja kwa moja, ingawa waziri huyo wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiye mbunge aliyemaliza muda wake na sasa anagombea tena kupitia CCM kutetea kiti chake.“Nawaambieni wana Kyela huyu (Mwanyamaki) ni mbunge mzuri, nyie mna bahati mbaya ya kuchagua wabunge wenye matatizo,” alisema na kuongeza:
 
“Naomba mumpe adhabu Oktoba 25, mwaka huu kwa kumchagua Mwanyamaki... naombeni mniletee huyu mtu bungeni.”
 
Akizungumzia kuhusu bodaboda na wafanyabiashara, alisema ataunda benki ya kuwashughulikia wafanyabiashara ndogo ndogo ili wasibughudhiwe mitaani.
 
 
MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema uchaguzi wa mwaka huu ni kuhusu mabadiliko, hivyo ni lazima washirikiane kwa pamoja kuiondoa CCM madarakani.
 
“Watanzania wote tunatakiwa kupiga kura na kuzilinda ili tushangilie ushindi kwa pamoja,” alisema.
 
Kuhusu CCM, alisema chama hicho kimetengeneza kura za bandia na wanakusudia kuziingiza kwenye vituo vya kupigia kura na kuwarubuni mawakala.
 
Alitaja mbinu nyingine ambayo CCM wamepanga kuitumia ni kutengeneza wasimamizi wa kimataifa feki ili waweze kuingia ndani ya vituo vya kura na kuweka kura haramu.
 
“Tunawaonya CCM na wale waangalizi ambao watapewa vitambulisho feki wasije wakafanya mchezo huo ambao utahatarisha amani ya nchi,” alisema.
 
KAULI YA CCM
Hata hivyo, msemaji wa Kamati ya kampeni za CCM, January Makamba, alipotafutwa jana kuelezea tuhuma za Mbowe, alisema tuhuma hizo siyo za kweli bali wapinzani wanatapatapa na kutafuta sababu pale watakaposhindwa.
 
Alisema waangalizi hawawezi kutumika kwa sababu wanafahamika na ofisi zao zinajulikana, hivyo CCM haiwezi kuwalaghai na kuwatumia.
 
KINGUNGE
Aliyekuwa mwasisi wa CCM, kingunge Ngombale-Mwiru, alisema ameachana na CCM kwa sababu chama hicho kwa sasa si kile ambacho walikiasisi mwaka 1977.
 
“Viongozi wake wa sasa wamekifanya mali yao binafsi, wanavunja katiba na taratibu... yote kwa kumuogopa Lowassa, eti wamzuie asifike Ikulu,” alisema na kuongeza:
 
“Ikulu si yao...kwenda Ikulu lazima ubebwe na watu, kama huna watu huwezi kufika Ikulu, walijaribu kumfungia ndani ya CCM, lakini Lowassa ikabidi aitafute haki yake nje ya CCM.”
 
OLE MEDEYE
Aliyekuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Dk. Goodluck Ole-Medeye, alisema alikataa kugombea ubunge mwaka huu kwa sababu alitaka kupita Tanzania nzima ili kuwaeleza Watanzania kilichopo ndani ya CCM.
 
“CCM haiwezi kutuvusha kwa sababu inatawaliwa na rushwa na ufisadi...wamekuwa ni wabinafsi,”
alisema.
 
Aliwataka wananchi wa Kyela kumkataa Mwakyembe ili asipate tena ubunge.
 
Wakati huo huo, Lowassa aliwaahidi  wananchi wa Tunduma kumaliza msongamano wa malori na kuliboresha eneo la Tunduma ili  kuliingizia Taifa mapato mengi.
 
Lowassa ambaye mkutano wake ulihudhuriwa na umati, alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais, atahakikisha anamaliza msongamano wa malori na liboresha eneo hilo ndani ya siku 21.
 
Aidha, alisema atahakikisha boda hiyo inafanyakazi kwa saa 24 badala ya 12 kama ilivyo sasa.
 
“Haiwezekani boda kubwa (mpaka) kama hii iwe inafanyakazi kwa saa 12 badala ya saa 24, nikiingia madarakani nitatatua matatizo yote,” alisema.
 
Aidha, alisema mpaka huo kwa mwaka unaingiza Sh. bilioni 34, na kwamba atahakikisha unaingiza zaidi ili Watanzania wanufaike.
 
Kuhusu suala la maji, afya na miundombinu, alisema atahakikisha anaunda kamati mikakati itakayoshughulikia masuala hayo.
 
Mbali na Kyela na Tunduma, Lowassa jana pia alihutubia  mikutano ya kampeni  maeneo ya Ileje, Busokelo, Makete na Tukuyu.
 
MAGUFULI
Naye mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, amejitabiria ushindi wa tsunami  katika na amerudia kauli yake kwamba wagombea wenzake ni sawa na wapambe wa  harusi.
 
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Ihumilo, Mkoa wa Geita wakati wa mwendelezo wa  kampeni za lala salama.
 
Mgombea huyo alisema ana imani ya kupata ushindi mkubwa kutokana na wananchi wa mikoa mbalimbali alikopita kuonyesha kumuunga mkono kwa kiasi kikubwa.
 
“Ndugu zangu nimepita mikoa mbalimbali na kote nilikopita wameniahidi ushindi wa tsunami na nyinyi hapa Geita naamini mtafanya kama wenzenu, mimi naahidi kufunga mianya yote ya rushwa na mafisadi wameshaanza kuweweseka,” alisema Dk. Magufuli.
 
 Aidha, mgombea huyo aliahidi kuwa rafiki mkubwa wa wavuvi  kwa kuwapa mikopo na zana bora za uvuni na aliwataka kuwapuuza watu wanaoeneza uvumi kwamba akiingia madarakani watakatazwa kwenda kuvua.
 
Alisema yeye anachopinga ni  uvuvi haramu kwa wale wanaotumia sumu wakati wa kuvua, hali ambayo imekuwa ikiua mazalia ya samaki na kusababisha idadi yao kupungua siku hadi siku.
 
Alisema serikali yake itasaidia kuinua sekta ya uvuvi  kwa kujenga viwanda vya samaki ili kuongeza ajira kwa vijana kwani viwanda hivyo vitakuwa vikiuza samaki kwa wingi nje ya nchi na kuingiza fedha za kigeni.
 
“Wavuvi msitishwe na mtu yeyote, mimi ni rafiki yenu na nitawasaidia, ingawa naomba kura, lakini narudia kuwakataza wanaovua kwa kutumia theodan, maana mnaua mazalia ya samaki na uvuvi haramu ndio umesababisha samaki kuadimika,” alisema.
 
Kuhusu pamba, alisema siku za karibuni bei yake imeporomoka na kuahidi kuwa akiingia madarakani atawawezesha wakulima wa zao hilo kulima kisasa kwa kuwapa pembejeo na dawa za kilimo.
 
Alisema kushuka kwa bei ya zao hilo kumesababishwa na kukosekana kwa viwanda vya kusindika pamba, hivyo akiingia Ikulu kupaumbele chake cha kwanza kitakuwa kuanzisha viwanda.
 
Dk. Magufuli alisema kulikuwa na viwanda ambavyo vilikufa kwa kukosa waendedhaji, hivyo aliahidi kuvifufua na kuanzisha vipya.
 
APATA MAPOKEZI MAKUBWA
Dk. John Magufuli, jana aliendelea kuutikisa Mkoa wa Mwanza kutokana idadi kubwa ya wananchi wanaojitokeza kumsikiliza kwenye mikutano yake.
 
Mgombea huyo amekuwa akipata mapokezi makubwa kwenye majimbo mbalimbali ya mkoa huo ambao alifanya mikutano yake ya kampeni.
 
Msafara wa Dk. Magufuli ulikuwa ukisimamishwa mara kwa mara na mamia ya wananchi wanaovamia  barabara wakitaka azungumze nao kwenye maeneo mbalimbali alikopita akielekea kwenye mikutano yake.
 
Jana mgombea huyo alisimamishwa zaidi ya mara kumi  kuanzia Mwanza Mabatini, Stand ya Nyakato, Igoma, Kisesa, Nyanguge, Kahangara, Lugeye, Ilungu  ambako alizungumza na wananchi wa maeneo hayo akiwa njiani kuelekea kwenye mkutano mkubwa wilayani  Magu.
 
AKERWA NA MITUMBA
Dk. Magufuli alieleza kukerwa watanzania kuvaa mitumba.
 
Wakati akizungumza na wakazi wa Jimbo la Magu na kuwahakikishia kuwa iwapo atashinda, serikali yake italijali zao la pamba na ataweka mazingira mazuri yatakayowezesha lipande bei.
 
Alisema haipendezi Watanzania kuendelea kuvaa mitumba wakati wanaweza kuendeleza zao la pamba na kuzalisha nguo za kuvaa wenyewe na kuuza nje ya nchi kuingiza fedha za kigeni.
 
Alisema kwa kuwa serikali yake itakuwa ya viwanda na atajenga viwanda vingi kwa ajili ya kuongeza thamani ya zao hilo badala ya kuuza malighafi  nje ya nchi.
 
“Haiwezekani Tanzania yenye katani na pamba ikaendelea kuagaiza mitumba kutoka nje…yaani sisi tunawauzia pamba wanatengeneza nguo wanazivaaa ndipo wanatuletea. Lazima tubadilike tutumie pamba yetu kutengeneza nguo tuwauzie wao,” alisema. 
 
Alisema serikali yake itatoa dawa za pamba na pembejeo kwa wakati ili kuinua kilimo cha zao hilo na wakulima wauze kwa bei ya faida hali itakayowahamasisha wananchi wengi kulima zao hilo.
 
Aidha, alisema anajua wakazi wengi wa Kanda ya Ziwa ni wafugaji, hivyo ataanzisha viwanda vya mifugo na samaki ili wafugaji wanufaike na mifugo yao kwa kuuza kwa bei ya juu.
 
“Nilipokuwa Waziri wa Mifugo, samaki waliongezeka sana kwa sababu tulipambana na uvuvi….wananchi tuache kuua mazalia ya samaki ili waongezeke watusaidie kwenye uchumi wetu,” alisema Dk. Magufuli.
 
Ukiwa njiani kuelekea Jimbo la Kwimba, msafara wa Dk. Magufuli ulizuiwa mara nane  na wananchi wa vijiji mbalimbali wakitaka kuzungumza na mgombea huyo.
 
Msafara wa Magufuli ulisimamishwa kwenye vijiji vya Kabila, Maligisu, Kadesh, Kalalo, Sumve mjini, uwanja wa Ngudu, Nyamirama na Mngumarwa ambako alisimama na kuzungumza na wananchi.
 
Akizungumza na wananchi wa Kwimba kwenye viwanja vya Ngudu, mgombea alisema anataka kuwa rais awe anatuma mawaziri kutekeleza miradi mbalimbali kama alivyokuwa anatumwa.
 
Dk. Magufuli alisema kama yeye aliweza kufanyakazi kubwa na inayoonekana ya kusimamia barabara akiwa anatumwa, hawezi kushindwa kufanya hivyo akiwa rais.
 
Alisema serikali yake itapunguza bei ya vifaa vya ujenzi kama nondo, bati, misumari na saruji ili kuwawezesh wananchi wengi kumudu kuvinunua na kujenga nyumba bora.
 
“Siwezi kuja hapa kuwadanyanganya kama wengine waliopita hapa kwamba nitamaliza nyumba za tembe ndani ya siku 100…hizo ni ndoto za mchana kwa sababu huyo anayesema hivyo hata kule anakotoka hizo nyumba hajazimaliza…mimi nitawezesha kushuka kwa bei ya vifaa vya ujenzi,” alisema Dk. Magufuli.
 
 MGOGORO MISUNGWI
Dk. Magufuli alisema migogoro ndani ya chama hicho wilaya ya Misungwi ndiyo imechelewesha maendeleo ya wilaya hiyo na aliwaagiza viongozi hao kuacha tofauti zao.
 
Alisema migogoro hiyo imekuwa ikidhoofisha chama hicho na kutoa mwanya kwa wapinzani kuitukana serikali kwamba haijafanya lolote.
 
“Msimkaribishe shetani, nataka muwe wamoja na kuanzia leo nataka mwende mkafanyiane kampeni  mbunge wafanyie kampeni madiwani na madiwani mumfanyie kampeni mgombea ubunge, mgawanyiko na malumbano yenu haiwezi kuisaidia Misungwi,” alisema.
 
Aidha, Dk. Magufuli alisema ameamua kusema ukweli kuhusu malumbano ya viongozi hao kwa kuwa yeye ni mtu wa kazi tu na hapendi kuona viongozi wakishindia malumbano badala ya kutatua kero za wananchi.
 
“Najua kuna wengine hapa mchana CCM usiku upinzani sasa hayo hayatawasaidia …muwe kitu kimoja kuhakikisha CCM inashinda, iwekeni Misungwi mbele na muachane kabisa na malumbano,” alisema Dk. Magufuli.
 
Vile vile, mgombea huyo alisema kuna mzee mmoja ambaye ameamua kuondoka CCM na kuisema vibaya kwamba haijafanya lolote wakati amezeekea kwenye chama.
 
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Abdalah Bulembo, alisema kuondoka kwa Kingunge Ngombare Mwiru hakuwezi kukitikisa chama hicho.
 
Alisema chama hicho kina hazina kubwa ya wazee ambao hawajawahi kuhama kwenye chama hicho na walio hai wameendelea kuwa washauri wazuri.
 
Imeandikwa na Jacqueline Massano, Kyela na Joseph Mwendapole, Geita na Gwamaka Alipipi, Dar.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment