Watu watatu wanaodaiwa kuwa maofisa wasaidizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), wamepata kichapo baada ya vurugu kubwa kuzuka katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, wakazi wa mji mdogo wa Himo walipowatilia shaka kisha kuwakamata wakidai kuwa wana masanduku matano ya kupigia kura, mali ya Nec.
Katika vurugu hizo, Polisi walilazimika kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kukabiliana na makundi ya wananchi waliokuwa wakitaka kuingia kwenye kituo kidogo cha Polisi Himo, baada ya kufunga barabara kuu ya Moshi Holili-Marangu ambayo inaziunganisha Tanzania na Kenya.
Hata hivyo, baada ya Polisi kuzima vurugu hizo, mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na mgombea ubunge wa TLP, Augustino Mrema walifika kituoni hapo kwa ajili ya kuwashuhudia watu hao na kujionea kile kilichodaiwa kuwa ni kura feki. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu jana kwamba, watu hao walikamatwa kati ya saa 3:30 na saa 4:00 juzi usiku wakati wakisafirisha masanduku hayo kwenda kwenye vituo vya kupigia kura.
“Uchunguzi wa awali wa Polisi, umebaini kwamba watu hao hawakuwa wezi wa kura kama ambavyo inadaiwa na wananchi, ila ni maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao walikuwa katika kazi ya kusambaza vifaa kwenye vituo vya kupigia kura vya Marangu-Kilema na Himo,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, kabla ya maofisa hao kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano, Polisi walilazimika kutumia nguvu kuwaokoa wasiendelee kushambuliwa na kujeruhiwa kwa kipigo na makundi ya wananchi hao waliokuwa wamewazingira.
Alisema baada ya kufanikiwa kuwanusuru, maofisa hao walifikishwa katika kituo cha Polisi-Himo wakiwa na vifaa hivyo na baadaye kuhojiwa ili kujiridhisha kama walikuwa ni maofisa wa NEC au la.
“Tuliendelea kuwashikilia kwa ajili ya mahojiano, lakini walipojitambulisha tulilazimika pia kumuita Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Vunjo, Fulgence Mponji, na aliwatambua kuwa ni maofisa wake,” alisema Kamanda Ngonyani na kuongeza kuwa baada ya hapo waliwaachia.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment