Dar es Salaam. Wakati matokeo ya ubunge katika jimbo la Kinondoni yakisubiriwa, umati vijana wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba (Ukawa) wamekusanyika nje ya kituo cha kujumlishia matokeo hayo huku wakiimba nyimbo kushinikiza yatangazwe.
Kwa zaidi ya masaa sita vijana hao walikuwa wakipiga kelele licha ya kikosi cha kutuliza ghasia cha jeshi la polisi (FFU) kutoa matangazo ya kuwatawanya.
Eneo lote la chuo kikuu huria lilizungukwa na ulinzi mkali wa askari, ili kupisha zoezi la kujumlisha matokeo uliokuwa katika ukumbi wa chuo hicho.
Kadri masaa yalivyokuwa yakiongezeka ndivyo umati mkubwa wa vijana hao uliongezeka bila hofu hali iliyokifanya kikosi cha FFU kujipanga, na kutoa tangazo la kutawanyika.
Hata hivyo hakuna aliyeondoka na badala yake vijana hao walikaa chini na kuendelea kuimba nyimbo zao za kutaka matokeo yatangazwe.
Miongoni mwa nyimbo walizokuwa wakiimba zilisema,“Tunataka matokeo kwa amani, tupeni matokeo vijana wa kindondoni hatulali mpaka kieleweke.”
Mpaka sasa hali ya viwanja vya Biafla si shwari na wakati wowote askari ambao wamejipanga na kuonyesha kitambaa chekundu wanaweza kufanya lolote huku kukiwa hakuna taarifa za saa ngapi, matokeo hayo yatatangazwa.
Wakizungumza na Mwananchi vijana hao walisema wanachotaka kupata ni matokeo kama ilivyo kwa majimbo mengine.
“Kwa nini iwe Kinondoni na sio sehemu nyingine, watoe matokeo haraka ili hali hii inayoendelea hivi sasa iishe,”alisema Amon Myela, mkazi wa Kinondoni.
No comments :
Post a Comment