By Angetile Osiah
Dar es Salaam. Leo Watanzania watatumia haki yao ya kikatiba kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, wabunge wa Bunge la Muungano, madiwani na wawakilishi kwa upande wa visiwani baada ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne kuhitimisha kipindi chake cha pili cha miaka mitano.
Ni siku ambayo inahitimisha kampeni ya takriban siku 64 za wagombea wa nafasi mbalimbali kujinadi kwa wananchi ili wapewe dhamana ya kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo.
Ni siku ambayo Watanzania watakuwa wakipiga kura kwa mara ya tano kwenye Uchaguzi Mkuu tangu mwaka 1995 baada ya Serikali kurejesha siasa za ushindani mwaka 1992.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, vyama nane vimesimamisha wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiongozwa na John Magufuli, anayegombea kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa (Chadema), Anna Mghwira (ACT Wazalendo) na Macmillan Lyimo wa TLP.
Wengine ni Hashim Rungwe wa Chaumma, Chifu Litasola Yemba (ADC), Fahmi Dovutwa (UPDP) na Junken Kasambala wa NRA.
Rekodi za Uchaguzi wa 2015
Mghwira, ambaye pia ni mwenyekiti wa ACT Wazalendo anakuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania, kuwa mgombea urais ambaye amepitishwa na chama chake na baadaye Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), akitokea chama ambacho kina umri usiozidi miaka miwili.
Pia, Samia Suluhu amekuwa mgombea mwenza wa kwanza wa kike kusimamishwa na chama kwenye Uchaguzi Mkuu na hivyo iwapo CCM itashinda, atakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Rekodi nyingine ni kwa Lowassa ambaye amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza kuihama CCM na kujiunga na upinzani na baadaye kupewa fursa ya kugombea urais, wakati Frederick Sumaye amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza aliyemaliza kipindi chake cha miaka kumi madarakani, kuhama chama tawala na kujiunga na upinzani.
Mawaziri wakuu waliopita, Dk Salim Ahmed Salim, John Malecela na Mizengo Pinda waliwahi kuingia kwenye mbio za urais wakaishia kwenye ngazi ya chama.
Pia kwa mara ya kwanza, vyama vinne vya upinzani-Chadema, NLD, CUF na NCCR Mageuzi, vimeingia kwenye uchaguzi vikiwa vimefikia makubaliano ya kimaandishi ya kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao si chama na haujasajiliwa.
Vyama hivyo viliunganisha nguvu mwanzoni mwa mwaka jana wakati wa Bunge la Katiba. Vyama hivyo vilipinga mwenendo wa Bunge hilo vikisema kuwa liliacha kujadili Rasimu ya katiba iliyopendekezwa na wananchi na kuwasilishwa kwenye chombo hicho na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Vilipinga kitendo cha Bunge hilo kubadili mapendekezo ya muundo wa Muungano, ambayo yalikuwa kwenye sura ya kwanza na ya sita zilizoanza kujadiliwa na vikaamua kususia mikutano na kuunda rasmi umoja huo, ambao ulihusisha kushirikiana katika uchaguzi.
Vifo vya wagombea
Pia mwaka huu, idadi ya wagombea ubunge waliofariki tangu kuanza kwa kampeni imekuwa ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote.
Uchaguzi katika majimbo sita hautahusisha wagombea ubunge baada ya wagombea watatu wa CCM, mmoja wa Chadema, ACT Wazalendo na NLD kufariki.
Mawaziri wawili wa Serikali inayomaliza muda wake, Celina Kombani, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma) na mbunge anayemaliza muda wake Ulanga Mashariki, na Abdallah Kigoda, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na mbunge wa Handeni ni kati ya wagombea sita waliopoteza maisha katika kipindi cha kampeni.
Wengine ni mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, aliyekuwa akigombea ubunge wa Jimbo la Masasi, Mohamed Mtoi wa Chadema aliyekuwa akigombea Jimbo la Lushoto, Estomih Mallah wa ACT Wazalendo aliyekuwa akigombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Deo Filikunjombe wa CCM ambaye alikuwa akitetea kiti chake Jimbo la Ludewa.
Kampeni za mwaka huu pia zimeshuhudia kifo cha mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, aliyefariki katika ajali ya gari iliyotokea Morogoro na kufanya uchaguzi huu uwe wa kwanza kupoteza wenyeviti wawili wa vyama vya siasa.
Kampeni za uchaguzi
NEC ilipuliza kipenga cha kuanza kwa uchaguzi ilipotangaza kuwa kampeni zianze Agosti 22 na CCM ikawa ya kwanza kuzindua Agosti 23 ilipofanya mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam. Siku sita baadaye, Chadema kwa kushirikiana na NLD, CUF na NCCR Mageuzi chini ya Ukawa wakazindua kampeni kwenye viwanja hivyo kwa kufanya mkutano uliohudhuriwa pia na maelfu ya watu.
Mikutano hiyo miwili ya vyama pinzani ndio iliyojenga sura ya mikutano mingine yote iliyofuata ya kipindi cha kampeni kutokana na kila chama kufanya jitihada ili kijaze watu wengi, maarufu kama nyomi.
“Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na mwamko na msisimko mkubwa kwa sababu wananchi wengi sasa wanafahamu wajibu wa Serikali kwao na wamechoshwa na namna Serikali inavyoendeshwa kwa maslahi ya wachache,” alisema Profesa Mpangala.
“Kwanza mshindi wa ngazi ya urais bado hajulikani. Lakini ni wazi kwamba wapinzani watapata viti vingi mwaka huu kwenye nafasi za ubunge na udiwani.”
Msomi huyo alisisitiza haja ya vyombo husika kutenda haki ili kuliepusha Taifa na vurugu.
Wakati uwingi wa watu kwenye mikutano ya kampeni umezua hofu kuwa upande mmoja unaweza usikubali matokeo iwapo utashindwa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda anasema haoni vurugu zikitokea.
“Hatuwezi kusema hakutakuwa na amani baada ya uchaguzi, lakini mazingira ya siku hiyo yataamua amani iwepo au isiwepo. Najua uchaguzi wa mwaka huu una msisimko mkubwa, na matarajio makubwa,” alisema na kuvitaka vyombo vya usalama kuhakikisha nchi inabaki katika hali ya usalama..
“Watanzania ni watu wastaarabu, hawataruhusu nchi yao iingie kwenye machafuko,” alisema Mbunda.
ACT-Wazalendo, kilichoanzishwa mwaka jana, kilifuatia kwa kuzindua kampeni zake kwenye Uwanja wa Mwembeyanga pia jijini Dar es Salaam, wakati TLP ilifanya uzinduzi wake Vunjo, ambako mwenyekiti wake, Augustine Mrema anawania ubunge na baadaye kuzindua tena kampeni kwenye Uwanja wa Mwembeyanga.
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kilizindua kampeni zake kwenye Uwanja wa Bakhresa, Manzese jijini Dar es Salaam. Vyama vingine vya ADC Maendeleo na UPDP vimekuwa vikidai kufanya kampeni kwa kufuata watu, lakini havijaitisha mikutano ya hadhara na vimekuwa havionekani sana.
Sera za vyama
Pamoja na uhasimu baina ya vyama viwili-CCM na Chadema- wagombea wote walijikuta wakijinadi kwa hoja za kutaka kufanya mabadiliko, kuongeza ajira, kuondoa kodi za kero kwa wakulima, kujenga mazingira bora ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao, kufufua na kujenga viwanda, kuongeza ufanisi kwa watendaji wa serikalini na kuboresha huduma za afya.
Pia walizungumzia ujenzi wa miundombinu ya usafiri, kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) na kuboresha elimu kwa kuwajengea walimu mazingira bora na pia kwa kutoa elimu bure kuanzia chekechekea ingawa walitofautiana wataishia kiwango gani.
Hoja kubwa iliyotoka kwa wananchi wakati wote wa kipindi cha kampeni ilikuwa ni kilio cha maji safi ambacho kilitolewa karibu kila sehemu ambayo wagombea urais walipita, na wote waliahidi kuitafutia ufumbuzi wakitoa mfano wa jinsi maji ya Ziwa Victoria yanavyosaidia baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Hoja za wachambuzi wa masuala ya kisiasa zilikuwa ni jinsi gani wagombea hao watapata fedha za kutekeleza ahadi zao. Lakini wote walieleza kuwa watahakikisha wanatumia rasilimali zilizopo kupata fedha za kuendesha miradi hiyo ya kutekeleza ahadi zao, hasa gesi.
Karibu wote walisema watabana mianya ya rushwa na ufisadi, kupunguza matumizi ya Serikali, kuziba mianya inayopoteza mapato ya Serikali, kama kodi na kuongeza uzalishaji viwandani, kwenye kilimo na uvuvi.
Ukiacha matatizo machache yaliyotokea sehemu chache, kampeni za mwaka huu zimekuwa za amani na za kistaarabu kutokana na mashabiki kujikita zaidi kushabikia wagombea wao badala ya kupambana na wafuasi wa vyama pinzani.
Ni kwa nadra sana kulitokea mapambano baina ya polisi na wananchi, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita.
Vyama 22 vyashiriki
Mwaka huu, jumla ya vyama 22 vinashiriki kwenye Uchaguzi Mkuu, kati yao vinane vimesimamisha wagombea urais na vilivyobaki vimesimamisha wagombea ubunge na udiwani. Mwaka 2010, ni vyama 19 tu vilivyoshiriki uchaguzi.
Kwa mujibu wa NEC, vyama vinavyoshiriki uchaguzi mwaka huu ni CCM, CUF, Chadema, UMD, NCCR- Mageuzi, NLD, UPDP, NRA na Tadea.
Vingine ni TLP, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau, AFP, CCK, ADC, Chaumma na ACT-Wazalendo.
Wapiga kura na majimbo
Katika mwaka ambao kumekuwa na hamasa kubwa ya wananchi kushiriki uchaguzi, Jumla ya wapigakura milioni 22.75 wameandikishwa kupiga kura mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya watu milioni mbili waliojiandikisha mwaka 2010. Katika uchaguzi uliopita, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 20,137, 303, lakini waliojitokeza siku ya uchaguzi walikuwa milioni 8.6 tu.
Mwaka huu, jumla ya makada 1,218 wa vyama mbalimbali wamejitokeza kugombea ubunge Bara na Visiwani, kati yao wanawake ni 233 na wanaume 985, wakati watu 10,879 wamejitokeza kuwania udiwani, kati yao wanawake wakiwa 679. Wagombea hao wa ubunge watakuwa wakichuana kuwania majimbo 264, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuongeza majimbo 26 mwaka huu.
Kati ya majimbo yaliyoongezwa, 20 yaliongezwa kutokana na kuanzishwa halmashauri mpya wakati mengine sita yalianzishwa kwa kigezo cha idadi ya watu, kwa mujibu wa mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva.
Zanzibar wachagua Rais, wawakilishi
Visiwani Zanzibar, wananchi watakuwa wakipiga kura kwa mara ya pili tangu kufikia maridhiano yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.
Maridhiano hayo yalifikiwa baada ya chama kikuu cha upinzani cha CUF kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na 2005, ya awali yakiwa yamesababisha machafuko makubwa. Machafuko hayo yalisababisha baadhi ya Wazanzibari kukimbilia Shimoni, Mombassa nchini Kenya kusubiri hali ya hewa itulie.
Mwaka huu, jumla ya vyama 14 vimesimamisha wagombea urais wa Zanzibar kati ya 15 vilivyochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Waliopitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni Dk Ali Mohamed Shein anayewakilisha CCM kutetea kiti hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad wa CUF, ambaye amekuwa akiweka upinzani mkali tangu siasa za ushindani zirejeshwe nchini.
Wagombea wengine ni Khamis Iddi Lila wa ACT-Wazalendo, Juma Ali Khatib (Ada-Tadea), Hamad Rashid Mohammed (ADC), Said Soud Said (AFP), Ali Khatib Ali (CCK) na Mohammed Masoud Rashid (Chaumma).
Wagombea urais wengine ni Tabu Mussa Juma (Demokrasia Makini), Abdallah Kombo Khamis (DP), Kassim Bakari Ali (Jahazi Asilia), Seif Ali Iddi (NRA), Issa Mohammed Zonga (SAU) na Hafidh Hassan Suleiman (TLP)
Wakati wananchi nchi nzima itakuwa ikichagua wagombea urais, wabunge na madiwani, Wazanzibari watakuwa na kazi zaidi ya kuchagua Rais wa Zanzibar na wawakilishi, kazi ambayo itasimamiwa na ZEC.
Jumla ya vyama 15 vimesimamisha wagombea 181 wa nafasi ya uwakilishi. Kati ya wagombea hao, 23 ambao ni sawa na asilimia 12.7 ni wanawake na waliosalia 158 (asilimia 87.3) ni wanaume.
Kwa mujibu wa ZEC, uteuzi wa wagombea umeongezeka kwa
asilimia 100 kwa uchaguzi wa Rais, asilimia 22.3 kwa uchaguzi wa wawakilishi na umepungua kwa asilimia 9.8 kwa uchaguzi wa madiwani ukilinganisha na mwaka 2010.
Wakazi 503,860 wamejiandikisha kupiga kura mwaka huu na watatumia haki hiyo ya kikatiba kwenye vituo 1,580, kila kituo kikiwa kimepangiwa wapigakura 350, kwa mujibu wa ZEC.
/Mwananchi.

No comments :
Post a Comment