Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, David Misime.
Dodoma. Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata mkazi wa Chang’ombe Emmanuel William (35) kwa tuhuma za kupiga nyimbo za mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Chadema, Edward Lowassa kwa kutumia simu ya mkononi wakati akiwa kwenye foleni ya wapiga kura.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, David Misime, alisema mpiga kura huyo alikamatwa katika kituo cha kupigia kura cha Chang’ombe mjini hapa Jumapili.
Pia Misime alisema wamewakamata watu watatu katika kituo cha kupigia kura cha Mbabala wakigawa vipeperushi vya aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Benson Kigaila.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Emmanuel Pascal (20), Samwel Joseph
(50) na Amos Lugonya (29).
Katika tukio jingine Misime alisema waliwakamata watu watatu katika kituo cha kupigia kura cha Emaus waliokuwa wamelewa na wakifanya fujo kwenye kituo hicho.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Kizitto Kabwe (36), Masonga Baraka (40) na Benedict Mbijima (35).
Misime pia alisema katika kituo cha Hamvu, Chamwino walikamatwa wakazi wawili wa Chang’ombe wakifanya fujo katika kituo cha kupigia kura cha Hamvu.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Tumaini Frank na Seleman Ally.
Kamanda huyo alisema mafaili ya watuhumiwa hao wote yamepelekwa kwa wakili wa serikali kwa ajili ya kuandaa mashtaka.
Hata hivyo, Misime alisema pamoja na kukamatwa kwa watu hao hali ni shwari mkoani hapa na watu walishiriki na kupokea matokeo ya uchaguzi kwa amani bila bughudha yoyote.
No comments :
Post a Comment