
Ct Scan (Computerized Tomograph) kazi yake ni kuonyesha mahali penye ugonjwa mwilini. Ina wajibu wa kuonyesha ukubwa wa tatizo katika eneo fulani mwilini ambalo hatuwezi kuliona kwa macho. CT Scan itabainisha ukubwa wa tatizo na kuonyesha njia za kulitatua. Kwa mfano, itabainisha kama tatizo hilo linaweza kutibiwa kwa njia ya upasuaji au la. Kifaa hiki kinaweza kuona uvimbe kichwani, kwenye ubongo, pajani, tumboni na ukubwa wake.
Dar es Salaam. Agizo la Rais John Magufuli la kutaka mashine za uchunguzi wa magonjwa za CT Scan na MRI za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, limetekelezwa baada ya mashine moja ya MRI kuanza kufanya kazi saa tisa alasili jana.
Pia agizo la Rais Magufuli la kutaka mgonjwa Chacha Makenge, aliyekwama kutibiwa kwa kukosekana vipimo vinavyotokana na mashine hizo, jana alipelekwa hospitali za nje kupimwa na ameanza matibabu.
Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Muhimbili na kukutana na madudu mbalimbali ikiwamo wagonjwa kulala sakafuni na mashine za vipimo na uchunguzi za magonjwa mbalimbali zikiwa hazifanyi kazi kwa takriban miezi miwili.
Taarifa za kukamilika kwa matengenezo ya mashine ya MRI (pichani), zilielezwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, baada ya mafundi wa Kampuni ya Philips ambao ndiyo wenye zabuni ya kufanyia matengenezo vifaa hivyo, kukamilisha matengenezo ya kifaa hicho.
Kwa mujibu wa Aligaesha, kampuni hiyo ilianza matengenezo hayo baada ya kulipwa fedha zao jana mchana. “Walianza kuifanyia matengenezo mashine hiyo na saa tisa alasili ilitengemaa na kuanza kufanya kazi,” alisema. Alisema juhudi za kuitengeneza mashine ya CT Scan zinaendelea na maendeleo ya kazi hiyo yatatolewa leo saa nane mchana.
Kuhusu mgonjwa Chacha, kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Dk Othmani Kiloloma, alisema mgonjwa huyo, alipelekwa hospitali nje ya Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na tayari vimefanyika.
“Tamko akitoa Rais ni amri, asubuhi jana (juzi) alichukuliwa kwa gari ya wagonjwa akapelekwa hospitali ya nje ya hapa, na hivi ninavyokwambia ameshapimwa yanasubiriwa majibu ili aanze kutibiwa, ”alisema Dk Kiloloma.
Kiloloma alisema kuwa idadi ya wagonjwa katika Taasisi hiyo inaongezeka siku hadi siku, huku uwezo wake ni kuhudumia wagonjwa 150, lakini sasa wanahudumia wagonjwa 280 hadi 300.
“Rais aliona changamoto tuliyonayo, wagonjwa ni wengi kuliko wodi zilizopo, wanahitaji huduma huku wengine wakiingia kila siku, alifikia hatua ya kusema kama hali ndiyo hiyo madaktari ni watu wa kwanza kuingia peponi,” alisema Kiloloma.
Makenge akizungumzia kupata matibabu baada ya Rais kutoa agizo, alisema: “Ninashukuru kupata nafasi hiyo ya pekee, ingawa amenitibia kama msaada kwa sababu sikupata nafasi ya kumpigia kura na kumuajiri, kwa sababu ukimpigia mtu kura ili awe kiongozi unakuwa umemuajiri.”
Alisema ujumbe wake kwa Rais ni kuwa sekta ya afya ina changamoto nyingi, ikiwamo kuibuka kwa maradhi mbalimbali katika jamii, yanayotokana na saikolojia ya wananchi kukua na kujaribu kila kitu wakati mwingine hadi vyenye madhara.
Alifafanua kuwa mgonjwa mmoja anaweza kuwa na maradhi aina tatu yanayohitaji utabibu wa daktari bingwa, huku madaktari wakiwa wachache na wagonjwa wengi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mbando, alisema agizo la kutengeneza mashine mbovu kama lilivyotolewa na Rais, limeanza kutekelezwa na vifaa vya matengenezo vimeshafika kwenye Bohari ya Dawa.
“Mbali na kuanza matengenezo, nimeziagiza hospitali za Serikali nchi nzima kuhakikisha zinaandikia mashine mbovu kwa ajili ya matengenezo, lakini nimetoa angalizo kuwa baada ya hapo kila hospitali italazimika kutengeneza kutokana na mapato yatokanayo na mashine hizo,” alisema.
“Mashine zikiwa nzima watu wanahudumiwa na kuchangia kiasi kidogo cha fedha, hizo fedha zinazopatikana ndiyo zitumike kuzifanyia ukarabati, ” alisema Dk Mbando.
Awali Aligaesha, alisema kuwa taarifa kuhusu kuharibika kwa mashine hizo zilishatolewa miezi miwili iliyopita, lakini kampuni hiyo iligoma kufanya matengenezo kutokana na kuidai Serikali.
Alisema walikuwa wanaidai Serikali kupitia Wizara ya Afya ambao ndiyo waliingia mkataba na kampuni hiyo, hivyo hawakuwa tayari kufanya kazi na kuongeza deni.
“Siyo kwamba hakukuwa na taarifa za kuharibika mashine hizo, tulishatoa miezi mwili iliyopita, wenye zabuni ya kutengeneza ambao ni Kampuni ya Philips, hawakukubali kufanya matengenezo huku wakiwa wanadai f edha zao, sifahamu ni kiasi gani lakini tambua walikuwa wanadai, ” alisema Aligaesha.
Matengenezo ya mashine hizo yamefanyika baada ya Rais kuamuru hazina itoe kiasi cha Sh3 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya mashine zilizoharibika katika hospitali mbalimbali za Serikali nchini ikiwamo ya taifa ya Muhimbili.
No comments :
Post a Comment