Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, November 5, 2015

Baba wa Magufuli alitaka mwanaye awe Padri

Image result for magufuli
UMEWAHI kujiona ‘muasi’ wa ndoto za wazazi wako juu yako, wakitaka uwe hivi na wewe ukita uwe vile, kama umewahi basi hauko peke yako. Haya yalimkuta pia mgombea urais wa CCM Dk. John Magufuli, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 2015.

Kwa mujibu rafiki na jirani wa Baba wa Magufuli, mzee Benedict Byangosha (65), baba yake alitaka mwanaye huyo awe Padre.

“Nakumbuka wakati anasoma sekondari Dk. Magufuli alihama Seminari ya Katoke na kujiunga Shule ya Sekondari ya Lake iliyoko Mwanza, hatua ambayo Baba yake, mzee Joseph Magufuli aliipinga,” anaeleza.

“Mzee wake alitaka Dk. Magufuli awe Padre wa Kanisa Katoliki na mimi kama rafiki na kaka yake nilishiriki sana kumshawishi mzee Magufuli kuwa kulikuwa hakuna ubaya wowote kijana wake kusoma shule ya kawaida ya sekondari, alikubaliana na ushauri wangu,” anaongeza.

Byangosha (65) mkazi wa eneo la Mlimani katika Wilaya Chato mkoani Geita ana tabasamu pana usoni kwake wakati akimwelezea jirani yake na rafiki yake Dk. John Magufuli.
“Ni kweli Dk. Magufuli ni jirani na rafiki yangu tangu mwaka 1973 nilipohamia eneo hili, tumeishi pamoja kama ndugu pamoja na wanafamilia wake tukisaidiana na kushirikiana katika mambo ya kijamii ya shida na raha.”“Katika mila zetu tunaamini kuwa jirani ni mtu muhimu kuliko ndugu, kwa sababu unapopata tatizo mtu wa kwanza kutoa msaada ni jirani yako kuliko ndugu walioko mbali, hata katika vitabu vya dini imesisitizwa umuhimu wa mtu kumpenda jirani kuliko nafsi yake, na kwa msingi mimi na Dk. Magufuli tunaheshimiana na tunapendana,” anaeleza mzee Byangosha.Katika mahojiano na Raia Mwema yaliyofanyika nyumbani kwa mzee huyo, Jumapili iliyopita, anamwelezea Dk. Magufuli kama jirani mwema mwenye utu, ushirikiano na upendo wa kipekee.

Mzee Byangosha ni mtumishi wa serikali aliyestaafu karibuni, ametumikia nchi kama mwalimu kwa kufundisha katika shule mbalimbali katika mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza.

Jiografia ya eneo hili inaonyesha kuwa mji wa mzee Byangosha unapakana na nyumba ya Dk. Magufuli ambapo eneo kubwa lenye wastani wa ekari tatu kuna makazi ya wanafamilia wengine na nyumba ya biashara inayomilikiwa na mgombea huyo.
Nyumba hiyo iko pembezoni mwa barabara kuu ya Chato-Biharammlo-Bukoba mkabala na ofisi za Halmashauri ya Wilaya Chato.

“Najisikia fahari sana, tumekuwa karibu kwa muda mrefu hatujawahi kukwaruzana kwa namna yoyote, ni jirani mwema sana hata wakazi wengine wa eneo hili watakueleza,”
“Kwa jinsi tulivyoishi pamoja nimemfahamu Dk. Magufuli kama mtu mcheshi sana na anayependa matani na watu wa rika lake na si rahisi kugombana naye,” anafafanua mzee huyo.

Kwa mujibu wa mzee huyo, mgombea urais huyo wa CCM ni makini sana linapokuja suala la maendeleo ya binafsi au kijamii na huwa hana mzaha katika hilo.

Kuhusu hilo mzee huyo anaeleza; “Kwa mfano kabla ya kuwa mbunge mwaka 1995 wakati huo akiwa mwalimu tu, aliendesha harakati zake binafsi kuwahimiza wakazi wa eneo hili kujenga nyumba bora za bati na kuachana na nyumba za asili,”
“Aliwahi kuniasa kuwa nikitaka kujenga nyumba ya bati si lazima nipate fedha nyingi na kununua bati na matofali kwa mkupuo, bali natakiwa kununua malighafi za ujenzi kidogo kidogo kulingana na mapato na ninaweza kufanikisha ujenzi katika kipindi cha miaka mitano tu,”
“Alikuwa mtu jasiri sana na hakuwa mwoga, alisimamia alichokiamini na pia hakuwahi kujitenga na wenzake na pale tulipopata nafasi ya kukaa pamoja aliwashauri fursa na njia za kufikia maendeleo.”

Kuhusu matarajio yake iwapo Dk. Magufuli atashinda nafasi ya urais, mzee Byangosha anasema kuwa ana matumaini makubwa mgombea huyo atakuwa kiongozi bora na ataivusha Tanzania kutoka hatua moja kwenda nyingine.

“Mimi ni mtu mzima sasa nina uzoefu katika utumishi wa umma, kwa upande wangu sitaki kuwa mnafiki kwamba natarajia kupata chochote kutoka kwake, lakini niseme kweli kuwa Dk. Magufuli atakuwa Rais wa mfano,” anasisitiza.

Jirani mwingine wa Dk. Magufuli ni Charles Saleh (54) ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya Chato katika Idara ya Misitu na pia ni mfanyabiashara, amemuelezea jirani yake kuwa mtu anayependa maendeleo.

Saleh anamiliki Hoteli ya Kyaka Resort, ambayo eneo lake limepakana na sehemu ya biashara ya Dk. Magufuli na nyumba za wanafamilia zilizojengwa jirani na hapo.

“Nilianza kufahamiana na Dk. Magufuli mwaka 2007 wakati nilipohamishwa kikazi nikitokea Shinyanga kama Afisa Misitu kuja wilaya mpya ya Chato,” anaeleza katika mahojiano yake na gazeti hili na kuongeza; “Chato ilikuwa wilaya mpya iliyoanzishwa mwaka 2006, hakukuwa na nyumba za kupanga na huduma nyingine zote muhimu za kijamii,”

Anaendelea kueleza; “Nakumbuka mwaka huo huo alikuja kama mbunge na tulifanya kikao cha pamoja kati yake na watumishi wa serikali na alitueleza kuwa tusimwangushe na tusiiangushe wilaya yake mpya.”

Saleh anaeleza kuwa Dk. Magufuli kwa wadhifa wake kama mbunge alijenga uhusiano wa karibu na watumishi wote wa serikali wa ngazi zote akifuatilia kwa karibu utendaji wao na mara nyingi hakusita kumpongeza anayefanya vizuri na pia hakusita ‘kumtolea uvivu’ mtumishi asiyewajibika.

“Hana tabia ya kumsema mtu pembeni, kama wewe ni mzembe atakuita na kukuonya ujirekebishe na pia alipenda sana kuwapongeza binafsi wale wanaofanya vizuri,” anaeleza.
Saleh anakumbuka kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuzaliwa kwa Wilaya ya Chato, mwaka 2010 ilishinda tuzo ya kuwa wilaya ya kwanza kitaifa kwa utunzaji wa mazingira na pia kata ya Kigongo ilishinda kuwa kata bora kitaifa.

“Kwa ngazi ya wilaya, Rais Kikwete alituzawadia shilingi milioni tano na kwa ngazi ya kata tulizawadiwa shilingi milioni tatu na mafaniko haya yalitokana na juhudi zangu za kuanzisha bustani ya miti kwa ushauri niliopewa na Dk. Magufuli,” anaeleza mtumishi huyo.

“Leo Chato imepaa kimaendeleo, kuna nyumba za kutosha za watumishi wa serikali, kuna nyumba za kulala wageni, kuna nyumba nyingi za kupanga na barabara za mji zimejengwa kiwango cha lami na kuna taa za barabarani ya kuongozea magari”.

“Haya ni maendeleo makubwa kwa wilaya yenye umri mdogo usiozidi miaka tisa na yote yamefanyika chini ya usimamizi wa Dk. Magufuli akiwa mbunge,” anaeleza mtumishi huyo.
Saleh anaeleza zaidi kuwa kama jirani yake wameshirikiana katika mambo mengi ya kijamii kama misiba, sherehe na hata ujenzi wa Kanisa, Kigango cha Mlimani.

“Ikitokea msiba wowote tunashirikiana pamoja uwe wa kifamilia au jirani yeyote na kama hatahudhuria basi atatuma rambirambi zake.”

“Hata waumini wa madhehebu mengine wamekuwa wanamwalika kwa nafasi yake kama waziri pamoja na mbunge kushiriki katika shughuli mbalimbali na hakuwahi kuwabagua hata siku moja,” anasema.

Anafafanua zaidi kuwa maendeleo ya Chato yanatokana na juhudi binafsi za Dk. Magufuli kama mbunge wake ambaye ndiye huwapa hamasa watumshi wa serikali kukopa na kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za kisasa na amekuwa akiwatoa hofu kuhusu hilo.
“Kwa kweli nafarijika sana kuwa jirani yangu ni mtu muungwana na mpenda watu, tumeishi vizuri kwa kuheshimiana pamoja na wanafamilia wake,” anaongeza.

Saleh anasema Dk. Magufuli akiwa Rais wa Tanzania ataendelea kuwa jirani yake kwa msingi huo tu na ana matumaini makubwa nchi itapiga hatua kubwa ya maendeleo.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/baba-wa-magufuli-alitaka-mwanaye-awe-padri#sthash.Uo1qLCPX.dpuf

No comments :

Post a Comment