dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, November 29, 2015

Kwa kasi hii mianya ya rushwa itakwisha

NA MHARIRI

29th November 2015.

Maoni ya Katuni
Ni dhahiri kuwa Watanzania wameanza kukubali dhamira njema ya uongozi wa awamu hii ya tano ya Rais Magufuli ya kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kwa nguvu zote.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa na wengi, Rais Dk. John Magufuli, amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade na kumteua Philip Mpango, kukaimu nafasi hiyo mara moja.

Uamuzi huo ulitangazwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa TRA kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 80.

Bade alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kufuatia kuwapo kwa upotevu huo wa fedha uliotokana na wafanyabiashara kukwepa kulipia ushuru makontena zaidi ya 300 yaliyoingizwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Tunaamini kuwa taarifa za ubadhirifu wa viongozi katika usimamiaji na uhakiki wa mizigo inayoingia bandarini hapo bila kulipa kodi Ikulu ilikuwa inajua, na inaonekana ni mtandao wa muda mrefu. 

Tunaamini yapo mashirika na taasisi nyingine za umma ambako ufisadi umejiimarisha kwa kipindi kirefu, ndio maana Rais Magufuli alitangaza wakati anazindua Bunge la 11 Dodoma kuwa serikali yake inaanza kutekeleza kwa vitendo vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.

Awali Waziri Mkuu, Majaliwa alitoa maagizo kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Lusekelo Mwaseba, watoe ushirikano kwa polisi kufuatia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kurejeshwa serikalini.

Tunaamini serikali haikuchukua maamuzi ya kufanya ziara ya ghafla ndani ya Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa kukurupuka tu, ilifanya uchunguzi wa kina na kubaini fedha za serikali kupotea katika mazingira ya ubadhirifu na ufisadi mkubwa. Ndio maana Katibu Mkuu Kiongozi alikwenda na orodha ndefu ya majina ya wakwepa kodi.

Kama alivyoahidi Rais Magufuli Bungeni, kwamba watuhumiwa wote watakaobainika kujihusisha na hujuma za fedha na mali ya umma, watawajibishwa na pia kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani, hilo tayari limeshawakumba watumishi waandamizi wa TPA na TRA.

Majaliwa aliwataja baadhi ya maofisa waliosimamishwa kazi kuwa ni pamoja na Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habib Mponezya, ambao aliagiza wakamatwe na kuisadia polisi wakati hati zao za kusafiria zikishikiliwa na mali walizo nazo zikaguliwe.

Udanganyifu unaofanywa na viongozi wenye dhamana ya kukusanya mapato ya serikali ni suala ambalo awamu ya uongozi huu haiwezi kuvumilia, hatua mbalimbali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka maadili ya uongozi wa umma.

Tunaamini kuwa mtikisiko uliotokea ndani ya Mamlaka ya Bandari na TRA ni mwendelezo wa dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila sekta ya umma inafanya kazi kwa matarajio yaliyowekwa, kwamba uwajibikaji unakuwa dira kuu ya kaulimbiu ya ‘Hapa ni Kazi Tu’.

Ni imani yetu kuwa uzembe, wizi na aina zote na ubadhirifu na ufisadi wa mali ya umma utakoma ili serikali iweze kukusanya mapato makubwa yatakayoiletea nchi mabadiliko ya kweli ya maendeleo kwa wananchi.

Tunaamini kila mpenda maendeleo ya Tanzania atatoa ushirikiano wa kufichua maeneo yanayoendelea kuhujumu uchumi wa taifa hili.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment