dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, November 19, 2015

Mali za waliookolewa zilirithiwa

Thobias Oluoti (Kulia) akiwa wodini jana akimuuguza kaka yake Onyiwa Moris aliyelazwa katika Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama baada ya kuokolewa katika machimbo ya Nyangarata. Picha na Shija Felician
Kahama. Hakuna msiba usiokuwa na mwenziwe. Msiba wa kwanza uliowapata wachimbaji watano wa madini katika machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama, Shinyanga ulikuwa wa kufukiwa na kifusi na kuishi shimoni kwa shida kwa siku 41, lakini msiba wa pili baada ya kuokolewa ni kukuta mali walizokuwa wanamiliki zimerithiwa.
Waliokumbwa na ‘msiba’ wa pili ni Onyiwa Morris na Chacha Wambura. Mali za Joseph Bulule zimenusurika lakini hakuna taarifa kuhusu mali za Amos Mhangwa na Msafiri Gerald.
Taarifa iliyotolewa jana na mganga mfawidhi wa hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Joseph Ngowi zimesema waathirika hao wote wako katika hali nzuri.
“Waathirika wote watano; Joseph Bulule, Chacha Wambura, Amos Mhangwa, Onyiwa Moris na Msafiri Gerald hawana magonjwa yoyote, wanahitaji lishe ili kurudisha nguvu zilizokuwa zimepotea baada ya siku saba tutawapa ruhusa ya kurudi majumbani kwao,” alisema Ngowi. “Kati ya hao, Onyiwa bado hajaanza kusimama lakini wengine wote wanasimama na wanaweza kutembea wenyewe bila kuwa na msaada wowote.”

Mali za waathirika
Akizungumza na Mwananchi jana mjini Kahama, Thobias Oluoti ambaye ni mdogo wake Onyiwa alisema baada ya tukio la kufukiwa kwa kifusi kaka yake na wenzake watano walikwenda nyumbani kwao Tarime na kuweka msiba.
Oluoti alisema kilichosababisha watangaze msiba ni kauli ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga kwamba haukuwapo uwezekano wa kuwaokoa wakiwa hai kwa vile hakukuwa na vifaa. “Baada ya kauli ile tulichukua nguo zake zote tukaenda kijijini ambapo tuliweka matanga kwa siku saba, na baada ya hapo, kwa mujibu wa mila na desturi zatu, tulianua matanga na kugawana mali za “marehemu” zikiwamo ng’ombe, mashamba na nguo,” alisema Oluoti.
Hata hivyo, tukio la kufukuliwa kwa kaka yake akiwa hai liliwashtua. “Nilipigiwa simu na mdogo wangu, mimi nikadhani huenda aliugua malaria au aliingiwa na mtandao wa kishetani wa freemanson. Tuliingiwa na hofu, nikamzuia mdogo wangu asiende mahali popote hadi nimpe maelekezo mengine,” alisema.
Mbali ya kuingiwa na hofu na kumzuia mdogo wake asiende sehemu yoyote, alimtaka afuatilie kwa makini simu iliyopigwa na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Tingwa na baada ya kupata uhakika ndipo alipopigiwa tena simu na mdogo wake.
“Aliponipigia simu aliniambia kwamba kaka Onyiwa ameokolewa akiwa hai na alinitaka niamini hivyo, ndipo nilipofunga safari kuja kwanza mimi mwenyewe kuthibitisha katika hospitali kujionea,” alisimulia. Oluoti alisema juhudi za kumwona Onyiwa hospitalini zilitatizika kwani alizuiwa na shemeji yake kwa madai hatakiwi kumwona mpaka atengenezewe masuala ya imani ya matambiko ya kwao.
Kutokana na shauku aliyokuwa nayo kumwona kaka yake na ukweli masuala ya mila na matambiko yamepitwa na wakati, Oluoti aligoma kwa madai wao ni Wakristo waumini wa dhehebu la Sabato hivyo aliingia wodini akamwona kaka yake akiwa amedhoofika ambapo alianguka kilio.
Bhoke Mwita ambaye ni mke wa Wambura alisema baada ya Serikali kutangaza kwamba haukuwapo uwezekano wa kuwatoa watu hao wakiwa hai waliamua kuhamisha makazi kutoka Nyangalata hadi Kahama ambako waliweka matanga. Baada ya hapo msiba ulihamia Tarime huku ndugu zake wakichukua nguo za mume wake na kwenda nazo huko ambako baada ya siku saba walianua matanga na kugawana mali zake.
Marco Bulule ambaye ni kaka wa Joseph Bulule alisema mali zake zilinusurika kurithiwa baada ya televisheni moja kutangaza kuwa watu waliofukiwa na vifusi bado walikuwa hai ndani ya mashimo na walikuwa wanawasiliana na wenzao wa nje kwa njia ya simu. Hiyo ilikuwa siku ya saba tangu wafunikwe na kifusi.
Bulule alisema ndugu wote waliokuwa kwenye msiba Bunda walisikia taarifa hiyo na ndipo kwaya ya kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) iliombwa kubadili nyimbo badala ya kuimba za kuomboleza ikaanza kuimba za kuwaomba Mungu awanusuru.
Taarifa hiyo iliwafanya waahirishe kufanya matanga na yeye alikaa hapo kwa siku 30 mpaka Novemba 5 alipoondoka kwenda nyumbani kwake Katoro, Geita. Bulule anasema siku ya tukio la kuokolewa kwa watu hao alipigiwa simu ambayo hakuiamini kwa kuwa zilipita siku nyingi watu hao wakiwa ndani ya mashimo.
Katika hatua nyingine Bulule alisema ingawa mdogo wake amenusurika kifo, kaka zake wawili walishakufa huko Tarime kutokana na tukio kama hilo la kufukiwa na kifusi. “Maisha yetu sisi ni uchimbaji madini,” alifafanua.
Wachimbaji hao watano ni kati ya sita waliofukiwa na kifusi Oktoba 5 na wameishi chini ya ardhi kwa siku 41 hadi walipookolewa Novemba 15 na kulazwa Hospitali ya Mji Kahama. Mchimbaji madini wa sita alifariki siku 15 kabla ya kuokolewa.

No comments :

Post a Comment