
Kituo cha Kulea Watoto Yatima na Wanaoishi katika Mazingira Hatarishi (Swacco) kilichoko Mwenge Mshindo Manipaa Songea Mjini, kimemwangukia mke wa Rais, Mama Janet Magufuli, awe mlezi wa kituo hicho.
Mkurugenzi wa Swacco, Regina Chinguku, amesema Mama Magufuli kuwa ni mmoja wa wanawake wachache waliojitokeza kwa miaka 10 iliyopita kusaidia kwa hali na mali kituo hicho.
Wanawake wengine waliotajwa kutoa msaada wa hali na mali katika kituo hicho kuwa ni Daktari Bingwa wa Hospitali ya Seliani iliyoko Ngaramtoni jijini Arusha, Dk. Neema Loi Sabaya.
Chinguku alisema wanamuomba Mama Magufuli awe mlezi kufuatia kifo cha Flora Komba, aliyekuwa mlezi na mwanzilishi wa kituo hicho.
“Mwanzilishi marehemu Flora Komba, ndiye aliyejenga nyumba moja kati ya nane zinazohitajika katika kituo hicho,” alisema Chinguku.
Alisema baada ya kufariki dunia kwa mlezi huyo, uendeshaji wa kituo hicho umekuwa mgumu.Kwa mujibu wa Chikungu, mwanzilishi wa kituo hicho alitaka majengo yote manane yajengwe ili kuwapa fursa watoto yatima na wanaoishi katika mzingira hatarishi, waishi ndani ya kituo hicho.
Alisema kwa sasa kituo hicho kina jengo moja tu, jambo linalolazimu watoto wengi yatima kuishi nje ya kituo.
Alipoulizwa kwa njia ya simu kutoa maoni yake kuhusu uendeshaji endelevu wa kituo hicho, Dk. Loi alisema kuwa serikali kwa sasa ichukue wajibu wake wa kusaidiana na wanawake walijitokeza kuendesha kituo hicho.
Dk. Loi alisema kuwa majirani na watu wengine wanaozunguka kituo hicho wasifumbie macho wajibu huo wa kusaidiana na Mkurugenzi wa Kituo hicho.
Baadhi ya watoto wanaoishi katika kituo hicho walisema watoto yatima wanaoishi nje ya kituo hicho wananyanyaswa na kuteswa na ndugu wanaoishi nao.
Mmoja wa watoto wanaoishi kituoni hapo, Amanu Saidi, alidai kuwa dada yake kwa sasa anaishi nje ya kituo hicho na amefaulu darasa la saba, lakini shangazi yao amesema hatampeleka sekondari kwa sababu hana uwezo wa kununua sare za shule na madaftari.
Aidha, wasichana mapacha, Marieta Turuka na Jane Turuka, wakizungumza huku wakibubujika na majozi, walidai hawajui pa kwenda baada ya kumaliza mitihani yao ya kidato cha nne Novemba, mwaka huu kutokana na baba yao kuwafukuza nyumbani miaka saba iliyopita huko Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma.
Wasichana hao walipata fursa ya kusoma elimu ya sekondari kwa ufadhili wa Swacco na kulelewa nyumbani kwa Mkurugenzi wa shirika hilo kwa zaidi ya miaka saba sasa.
Swacco liliwagharimia wasichana hao ada ya Sh. 900,000 kwa kila mwaka mbali ya sare na vifaa vya shule katika shule binafsi ya Sekondari Ruhuwiko ya mjini Songea.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment