
Geita. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Makame Mbarawa ametoa miezi minne kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka wa Mji wa Geita kuhakikisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria unawafikia wakazi wa mji huo.
Mji wa Geita unakabiliwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa muda mrefu sasa.
Waziri Mbarawa alitoa agizo hilo juzi alipofanya ziara ya kukagua mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria unaojengwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Dhahabu ya Geita (GGM) kwa gharama ya Sh13 bilioni.
Akiwa kwenye kituo cha mradi huo kilichojengwa ndani ya Mgodi wa Geita, alisema mradi huo unapaswa kuwafikia wakazi wasiopungua 4,000 ifikapo Aprili 2016.
Agizo hilo lilitokana na waziri huyo kutoridhishwa na maelezo ya Mkurugenzi huyo baada ya kuona mradi unasua sua huku wananchi wakiteseka na huduma ya maji.
Akisisitiza kauli yake Mbarawa alisema kuna watu wengi wanataka maji lakini hawajafikiwa na mradi huo na kuhoji kwa nini wateja hao 4,000 wasitafutiwe njia mbadala ili wayapate kwa haraka zaidi.
Katika maelezo yake Chagu, alidai mradi huo una uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 200 kwa saa, lakini inakadiriwa kukidhi mahitaji ya maji kwa wakazi wa Geita kwa asilimia 24. Kwa sasa kuna asilimia tatu tu ya maji yanayozalishwa na mamlaka hiyo.
Alisema mahitaji ya maji kwa Mji wa Geita ni lita 15,000 kwa siku na kuna asilimia 10 zinatoka kwenye vyanzo vingine vya maji.
Chagu alisema mradi huo umeanza kutoa huduma kwa majaribio Novemba na bado kuna matatizo madogo ya mkandarasi. Alisema wanatakiwa kujenga kilomita 35 za mtandao wa maji, lakini mahitaji ni kilomita 89, lakini kutokana na upungufu wa fedha, mamlaka inakusudia kuanza na kilomita 35.
Alidai wateja waliopo ni 510, lakini waliounganishwa kwenye mtandao mpya ni 12 tu huku matarajio yakiwa ni kuwafikia wateja 6,000 miradi yote miwili itakapokamilika.
Alisema mradi wa kwanza unatarajia kukamilika Agosti, 2016 na mradi wa pili Aprili, 2017 na wateja 4,625 wataunganishwa kwenye mradi huo.
Akitoa taarifa ya maji ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwassa alisema kutokana na ongezeko la ukuaji wa miji ya Geita na Chato, mahitaji ya maji nayo yanaongezeka kwa wakazi wa miji hiyo.
Waziri Mbarawa alikagua miradi ya maji kwenye wilaya za Chato, Geita na Nyang’hwale ambayo ipo kwenye mradi wa Nyamtukuza na Mbogwe.
No comments :
Post a Comment