Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, December 21, 2015

WALAJI WA NYAMA YA NG'OMBE DAR ES SALAAM HATARINI!

Ng'ombe waliodungwa sindano za kunenepeshwa wakipumzika kwenye malisho yao wilayani Shinyanga Vijijini. PICHA: SANULA ATHANAS
Walaji wa nyama ya ng’ombe katika Jiji la Dar es Salaam wako katika hatari kubwa ya kupata maradhi kama ya saratani na kushindwa kufanya kazi kwa figo na ini kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia kemikali zisizofaa katika kuwanenepesha wanyama hao kabla hawajafikishwa  sokoni, imefahamika.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa miezi kadhaa, ukihusisha ziara iliyoanzia kwenye baadhi ya maeneo wanakotolewa ng’ombe mkoani Shinyanga na pia jijini Dar es Salaam, umebaini kuwapo kwa wafanyabiashara wanaowanenepesha ng’ombe kwa kemikali mbalimbali zikiwamo zisizoruhusiwa na pia wengine huwalisha mbolea aina ya Urea kwa nia ya kujiingizia kipato kikubwa bila kujali afya za walaji wa kitoweo hicho.
Kadhalika, uchunguzi umebaini kuwa matumizi ya kemikali hatarishi kwa ajili ya kuwanenepesha ng’ombe kabla ya kuwafikisha jijini Dar es Salaam hushindwa kufahamika kirahisi kutokana na changamoto ya kukosekana kwa vifaa vya kutosha ili kuchunguza ng’ombe wote wanaoingia jijini Dar es Salaam kila uchao.
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ambako ndiko kuna machinjio ya Vingunguti na Ukonga, Dk. Audifas Sarimbo, alisema ofisi yake haina taarifa za kuwapo kwa ng’ombe wanaofikishwa sokoni baada ya kunenepeshwa kwa kemikali kama za mbolea aina ya Urea.
Kadhalika, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudencia Simwanza, alikiri kuwapo kwa dawa zilizodhinishwa nao (TFDA) kwa ajili ya kunenepesha mifugo, lakini zote za aina hiyo huwa na alama maalumu ikiwamo ya kuwa na namba inayoanzia na ‘TAN’ na kwamba kati yake, hakuna mbolea iliyoidhinishwa kwa kazi hiyo.
Ofisa Mifugo Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, Beda Chamatata, aliiambia Nipashe kuwa kuna tataizo kubwa la kuwapo kwa wafanyabiashara wanaonenepesha ng’ombe kwa njia haramu za kutumia dawa zisizofaa na kwamba sababu kubwa ni kuwapo kwa soko kubwa la kitoweo hicho jijini Dar es Salaam, hali inayowalazimu wengi wao kufanya kila wawezalo kwa nia ya kujiingizia fedha pasi na kujali afya za walaji.
     
TAARIFA KAMILI 
Nyama ya ng’ombe ni kitoweo maarufu katika jiji la Dar es Salaam. Kila uchao,  wakazi wa jiji hilo hula tani 120 za nyama (sawa na ng’ombe 1,200), kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Dk. John Mbogoma.

Licha ya kuchinja mifugo, Dk. Mbogoma aliiambia Nipashe jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuwa kila mwaka Tanzania husafirisha kiasi cha ng’ombe 300,000 kwenda Kenya ambao baada ya kuchinjwa, baadhi ya nyama hurejeshwa nchini na kuuzwa kwenye maduka makubwa, maarufu ‘super markets’.

Umaarufu wake, kupendwa kwake katika milo ya kaya aina zote jijini Dar es Salaam, husababisha mahitaji ya kitoweo cha nyama ya ng’ombe kuwa juu kila uchao.
Hali hiyo imevutia wajasiriamali wengi ambao wamewekeza katika biashara hiyo kwa kujua kwamba soko ni la uhakika.
Hata hivyo, changamoto iliyoibuka hivi karibuni ni kuwapo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaotaka faida ya haraka, wakitumia njia haramu za kunenepesha ng’ombe kwa kemikali, ambazo zinadaiwa kuleta matokeo ya haraka na kuwaongezea siha ng’ombe kabla ya kuwapeleka sokoni kwa nia ya kuwa na ng’ombe wa madaraja ya juu, wenye kilo nyingi (za minofu) na hatimaye faida kubwa.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kuanzia Machi, 2014, umebaini kuwa vitendo hivyo hufanyika zaidi kwenye maeneo ambako ng’ombe hupewa malisho maalum kwa ajili ya kuwaongeza siha kabla ya kuwasafirisha kwenda kwenye soko kubwa la kitoweo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Chamatata, mkoa wa Shinyanga, mwaka huu  unakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 1.2. Kati yao, 38,802 wamenenepeshwa na wanenepeshaji 189 wanaotambuliwa na serikali katika halmashauri za Kahama Mjini, Kishapu, Msalala, Shinyanga Vijijini, Shinyanga Mjini na Ushetu.
Akiwa kwenye mnada wa Tinde wilayani Shinyanga Vijijini Novemba 17 mwaka huu, mmoja wa wafanyabiashara wa ng’ombe ambaye hajapata leseni kwa miaka nane iliyopita (jina tunalo), aliliambia gazeti hili kuwa ng’ombe wake huwa anawadunga sindano zenye dawa za kunenepesha kabla ya kuwasafirisha kwenda Dar es Salaam.
“Tangu mwaka 2007, ninajishughulisha na biashara hii, wafanyabiashara wengi kwa sasa tunatumia sindano kunenepesha ng’ombe kwa sababu unenepeshaji wa asili wa kutegemea majani na pumba unachukua miezi saba hadi tisa ng’ombe kuwa kwenye hadhi ya kuuzika kwa bei katika soko la Dar es Salaam,” alisema mfanyabiashara huyo.
“Tunanunua ng’ombe (ambao hawajanenepeshwa) kwenye minada kwa laki na nusu (Sh. 150,000) hadi laki tatu na nusu (Sh. 350,000), kisha tunawaweka kwenye dozi maalum ya sindano kwa miezi mitatu wananenepa. Ukishamfikisha Dar es Salaam unapewa laki nane (Sh. 800,000), akiwa mkubwa zaidi unapewa hadi milioni moja na nusu (Sh. 1,500,000),” aliongeza.
Machi 25 mwaka jana, mfanyabishara mwingine wa ng’ombe alimwambia mwandishi kwenye mnada wa Mhunze wilayani Kishapu (mnada mkubwa zaidi wa ng’ombe mkoani Shinyanga) kuwa gharama kubwa za usafiri na vibali vya usafirishaji ndiyo chanzo cha wafanyabiashara wengi kutumia dawa na aina nyingine za kemikali kunenepesha mifugo yao kabla ya kuipeleka sokoni.
“Ukipeleka ng’ombe ambaye hajanenepeshwa, inakuwa hasara kwa sababu atanunuliwa kwa pesa kidogo na wakati mwingine unakosa mteja wa kumnunua,” alisema.
“Ili upeleke ng’ombe Dar es Salaam au Sirari (mpakani mwa Tanzania na Kenya), inabidi ugongewe mhuri na Ofisa Mifugo wa Wilaya, kuidhinisha jina na leseni ya mfanyabiashara na unalipia kibali Sh. 7,500 kwa kila ng’ombe.
 Wafanyabiashara wengi wa ng’ombe hatuna leseni, tunawalipa wenye leseni ‘laki mbili’ (Sh. 200,000) kwa safari moja. “Wenye magari nao tunawalipa Sh. 40,000 kwa kila ng’ombe kutoka huku Kanda ya Ziwa kwenda Dar. Vijana wanaowalinda ng’ombe safarini, tunawalipa ‘laki moja na nusu’ (Sh. 150,000) na wanakuwa wawili kwenye gari linalobeba ng’ombe 60 hadi 70. Gharama hizi ni kubwa, bila kuwanenepesha ng’ombe, inakuwa ngumu kupata faida,” alieleza mkazi huyo wa Kijiji cha Jibiso wilayani Igunga mkoani Tabora.
Wafanyabiashara hao wawili waliitaja minada mingine ambayo hununua ng’ombe kwa ajili ya kuwapeleka Dar es Salaam na kwenye mnada wa kimataifa wa ng’ombe wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara kuwa ni pamoja na Benako (Ngara), Lusonzo (Kahama), Ludahunga (Biharamulo), Katoro (Geita), Old Shinyanga (Shinyanga), Manzese (Kahama) na Bukombe (Geita).
Wafanyabiashara hao walieleza kuwa wamekuwa wakitumia kuanzia siku moja na nusu hadi siku mbili kusafirisha ng’ombe kwa magari kutoka Shinyanga hadi Dar es Salaam.
“Ukishafika kwenye geti la mnada wa Pugu, unakabidhi kibali chako kwa askari ambaye hukipeleka kwa Ofisa Mifugo wa halmashauri kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kukuruhusu kuingiza ng’ombe wako mnadani. Getini hakuna malipo kwa sababu unakuwa umeshalipia hapa Shinyanga,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Nipashe ilipotembelea maeneo ya malisho ya ng’ombe wa wafanyabiashara katika wilaya za Kahama, Shinyanga Vijijini na Kishapu hivi karibuni, ilibaini kuwa wengi wao wanadunga sindano za dawa za kunenepesha mifugo yao kabla ya kuipeleka sokoni.
Ilibainika kuwa ng’ombe waliodungwa sindano za dawa za kunenepesha, wanatumia muda mwingi kupumzika kwa kulala kwenye mazizi na maeneo wanakopewa malisho. Gazeti hili pia lilibaini kuwa dawa za kunenepesha mifugo (baadhi zikiwa hazina alama yoyote ya kuidhinishwa na mamlaka husika) zinauzwa kiholela kwenye minada na maduka ya dawa za kilimo na mifugo mkoani Shinyanga pasi na usimamizi wowote wa mamlaka za serikali.
Katika minada ya Tinde na Mhunze, mwandishi alikuta aina mbalimbali za dawa za mifugo zikiwamo za kuoshea aina ya Tix Fix, Paranex na Cybadip, za kuua minyoo kwa mifugo; Levamisole, Albendazole (ya maji) na Ivermectin Injection pamoja na za kunenepesha; OTC 20%, OTC 10%, Multivitamin Injection, Pen & Strep Injection na Diminasan Injection zikiuzwa na watu wanaojitambulisha kama wafanyabiashara wa dawa za mifugo.
Mwandishi pia alibaini kuwa wauzaji wa dawa za mifugo kwenye minada hiyo walikuwa hawazingatii taratibu za uhifadhi wa dawa.
Mfano, dawa ya kunenepesha aina ya Bavitamin (Multivitamine Injectable Solution) ambayo maelezo yake ya uhifadhi (storage) yanataka isiwekwe juani, ilikutwa na mwandishi ikiuzwa juani kwenye minada mbalimbali mkoani humo miezi miwili iliyopita.
Nipashe pia ilishuhudia dawa hiyo ikiuzwa kwa Sh. 4,000 kwenye moja ya maduka makubwa ya dawa za kilimo na mifugo mjini Shinyanga (Novemba 24 mwaka huu) ikiwa haina alama na namba zozote za usajili wa mamlaka inayohusika na dawa nchini.
Ilibainika vilevile kuwa baadhi ya dawa zinazotumiwa na wafanyabiashara mkoani humo kunenepesha ng’ombe, zina viambata vya kundi la Dexamethasone: Paradexa, Decason, Oradexason na Predexanol pamoja na viambata vya aina mbalimbali za vitamini ambavyo vimeshapigwa marufuku kutumika kunenepesha mifugo barani Ulaya baada ya kubainika kuwa na athari kubwa kwa walaji wa nyama.
Mwaka 2010, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zilisaini makubaliano ya kupiga marufuku nyama za mifugo iliyonenepeshwa kwa dawa zenye viambata hivyo.
Kadhalika, Sheria ya Malisho ya Wanyama ya mwaka 2010 inayotumika kwenye nchi zote wanachama wa EU, inazuia matumizi ya dawa, homoni za kuongeza ukuaji na kemikali za aina yoyote katika malisho ya wanyama. Yeyote anayepatikana na hatia ya kuikiuka, adhabu yake ni kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya euro 500 (Sh. milioni 1.2) au adhabu zote mbili.
SHERIA ZA TANZANIA
Sheria ya Malisho ya Wanyama ya mwaka 2010, iliyosainiwa na Rais wa Tanzania Mei 20, 2010, inakataza mifugo kunenepeshwa kwa kemikali na dawa hatarishi.
Kifungu Na. 13 cha sheria hiyo kinataja adhabu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kufanya kosa hilo kuwa ni faini isiyozidi shilingi milioni tatu au kifungo kisichozidi kipindi cha miaka miwili jela au adhabu zote kwa pamoja.
MATANGAZO YA DAWA
Licha ya sheria za Tanzania kukataza matangazo ya dawa, mabango ya dawa za kunenepesha mifugo yalikutwa na mwandishi ndani na nje ya maduka mbalimbali ya dawa za kilimo na mifugo mkoani Shinyanga.
Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003 inakataza mtu au taasisi kutangaza biashara ya dawa na huduma za matibabu.
Dawa nyingi za kunenepesha mifugo zilizokutwa na mwandishi kwenye maduka ya Kahama na Shinyanga mjini, zinatoka China na zilikuwa zinauzwa kuanzia Sh. 4,000 (za sindano) huku chache zikitoka Kenya, Uholanzi, Ufaransa na Ubelgiji, zikiuzwa kuanzia Sh. 5,000.
Baada ya kutembelea maduka mbalimbali ya dawa za kilimo na mifugo mkoani Shinyanga, Nipashe ilibaini kuwa wenye maduka siyo tu kwamba walikuwa wanauza dawa kwa wakulima na wafanyabiashara, bali pia walikuwa wanawashauri wateja wao namna ya kutumia dawa husika.
Manyesha James, muuzaji wa duka la dawa za kilimo na mifugo la Kings Chemist lililopo mjini Shinyanga, alisema dawa zinazonunuliwa kwa wingi kwenye duka hilo ni za kuoshea na kunenepesha mifugo.
“Dawa zinazonunuliwa sana na wafugaji ni za kuoshea, lakini kuna wafanyabiashara wanaopeleka ng’ombe Dar es Salaam na Kenya, hawa wananunua sana dawa kwa ajili ya kunenepesha,” alisema.
Manyesha alisema changamoto kubwa inayowakabili wakulima, wafugaji na wafanyabiashara ya ng’ombe mkoani Shinyanga ni ukosefu wa elimu.
“Wengi wao wanapofika hapa (dukani) wanakuwa wamekariri rangi za makopo ya dawa. Ukimpa dawa ile ile anayotaka, kama rangi ya kopo imebadilishwa, anakataa kununua dawa husika. Baadhi yao wanatumia dawa ya kuogesha mifugo kupulizia mimea,” alieleza zaidi Manyesha.
   
NG’OMBE WALISHWA UREA
Baadhi ya wauzaji wa maduka ya vifaa na dawa za kilimo na mifugo katika miji ya Kahama na Shinyanga waliieleza Nipashe kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa ng’ombe wamekuwa wakilisha mifugo yao pumba zilizochanganywa na mbolea ya kurutubisha mimea aina ya Urea ambayo hufahamika zaidi kama ‘46% Nitrogen MIN’.
“Kuna wafanyabiashara wa ng’ombe walikuwa wanakuja hapa wananunua dawa za kuoshea mifugo na Urea. Baada ya kuwauliza kuhusu matumizi ya Urea, walisema wanaichanganya kwenye pumba wanazowalisha ng’ombe wao.
“Pumba zinapaswa kuchanganywa na chumvi na siyo Urea, hii ni mbolea kwa ajili ya mimea, lakini inatumiwa isivyo. Hatuko salama kiafya, Mungu tu anaendelea kutulinda,” alisema Aboushir Salum, msimamizi wa duka la Kings Chemist.
“Sehemu kubwa ya dawa zetu zinatoka China na zinanunuliwa sana kutokana na bei yake kuwa nafuu. Nyingine zinatoka Uholanzi, Ufaransa na Belgium (Ubelgiji), aliongeza Salum”
ATHARI
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ulaji wa nyama ya ng’ombe walionenepeshwa kwa dawa, kemikali na mbolea za mimea, una athari kubwa kwa afya za walaji.

Dk. Abbas Ram, mtaalam wa magonjwa ya ngozi katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, alisema serikali inapaswa kudhibiti unenepeshaji huo haramu wa mifugo kwa manufaa ya Taifa.
“Ni vyema watu wakajikita kwenye vyakula vya asili kwa sababu vyakula vya kisasa na nyama za mifugo iliyokuzwa ndani ya muda mfupi kwa kutumia dawa ni hatari kwa afya zao. Serikali pia inatakiwa kudhibiti vyakula hivi vya kisasa,” alisema Ram.
Daktari mwingine wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Prudence Rwekaza, aliambia Nipashe hospitalini hapo Novemba 25 mwaka huu kuwa dawa zenye viambata vya vitamini na kemikali za unenepeshaji, wanazitumia wanapokuwa na mgonjwa mahututi na aliyedhoofika kimwili.
“Dawa hizi zenye mchanganyiko wa vitamini na kemikali za unenepeshaji tunazitumia pale tu tunapokuwa na mgonjwa ambaye amekonda sana na kudhoofika kiasi kwamba anahitaji kuongeza mwili kwa haraka, hasa wagonjwa wa ‘TB’ (Kifua Kikuu) na Ukimwi,” alisema Dk. Rwekaza na kueleza zaidi:
“Athari za dawa hizi zinaanzia kwenye ini maana ndiyo chujio la sumu mwilini, inafuata figo na baadaye moyo na mfumo wote wa damu. Ndiyo maana tunazitumia tu katika hali ya dharura kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa mwili wa binadamu.
“Zikishaingia mwilini, dawa hizo hutengeneza ‘fluid’ (kimiminika au gesi) inayosambaa kwa kasi na kusisimua homoni za ukuaji ndiyo maana mifugo hunenepa kwa haraka na kuwa na umbile kubwa.
“Kama ilivyo kwa kuku wa kisasa wanaokuzwa kwa wiki tatu, mlaji wa nyama ya ng’ombe aliyenenepeshwa kwa dawa na kemikali, anapata unene uliopita kiasi na wa ghafla. Pia anakuwa katika hatari ya kuugua kansa na kushindwa kufanya kazi kwa ini, figo na moyo.”
TAKWIMU HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI
Katika uchunguzi wake, mwandishi hakufanikiwa kupata takwimu zinazohusisha moja kwa moja vifo au maradhi yatokanayo na ulaji wa nyama ya ng’ombe walionenepeshwa kwa kemikali zisizofaa kama mbolea ya Urea.
Hata hivyo, ripoti ya mwaka 2012/13 ya Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyotolewa Machi 14, 2014, inaonyesha kuwa watu 1,720 walipokewa katika hospitali hiyo wakisumbuliwa na magonjwa yatokanayo na kushindwa kufanya kazi kwa ini na figo, ambayo yanatajwa kuwa ni baadhi ya madhara wanayoweza kuyapata watu wanaokula nyama ya ng’ombe walionenepeshwa kwa kemikali.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa wagonjwa 61 walifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kwenye hospitali hiyo (hakuna aliyefariki).
Aidha, ripoti ya mwaka 2011/12 ya hospitali hiyo iliyotolewa Machi 8, 2013, inaonyesha kuwa hospitali hiyo ilipokea wagonjwa wa moyo 97. Kati yao, sita walifariki wakati wakipatiwa matibabu.
MAOFISA MIFUGO SHINYANGA
Ashura Kaparata, Ofisa Mifugo Kata ya Tinde wilayani Shinyanga Vijijini, alisema serikali inapaswa kuhakikisha kunakuwa na ukaguzi wa kina katika uchinjaji wa mifugo nchini.
“Tunawashauri watu wasile mizoga, pia kuwe na ‘antemortem’ na ‘postmortem inspection’ (ukaguzi kabla na baada) ya kuchinja mifugo ili kuepuka magonjwa yatokanayo na ulaji nyama kama vile ‘rashes’ (vipele),” alisema Ashura.
Ofisa Mifugo Msaidizi Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Maduhu Limbu, alisema ofisi yake haikuwa na taarifa za unenepeshaji wa mifugo wilayani humo kwa njia ya kemikali na dawa.
“Hapa (Shinyanga Vijijini) hatuna taarifa za wafugaji wetu kunenepesha mifugo kwa kutumia dawa na kemikali. Tumekuwa tukiwashauri wafugaji kudunga sindano za minyoo, kukata kwato na pembe na kuogesha mifugo yao ili kuzuia magonjwa yanayoenezwa na kupe,” alisema Limbu.
Hata hivyo, takwimu za unenepeshaji wa mifugo mkoani Shinyanga zinaonyesha kuwa wilaya ya Shinyanga Vijijini ina wanenepeshaji 10 (wanaotambuliwa na serikali) ambao mwaka huu wamenenepesha ng’ombe 400. 
Unenepeshaji wa Ng’ombe Mkoa wa Shinyanga Mwaka 2015
Halmashauri   Wanenepeshaji   Ng’ombe
Ushetu DC              6                     4,238
Kahama TC           89                   28,000
Msalala DC             4                        314
Kishapu DC           50                     3,100
Shinyanga DC       10                        400
Shinyanga MC       30                     2,750
Jumla                 189                   38,802
Chanzo: Taarifa za Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga 2015
ONGEZEKO LA WATU
Ofisa Mifugo Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, Beda Chamatata, alisema Dar es Salaam si mahali salama kwa walaji nyama kutokana na jiji hilo kuwa na idadi kubwa ya watu kiasi cha kuwalazimu wafanyabiashara kutumia dawa kunenepesha ng’ombe ili kukidhi mahitaji ya nyama jijini humo.
Aidha, Chamatata alisema Dar es Salaam si mahali salama kwa walaji nyama kutokana na jiji hilo kutokuwa na machinjio ya kisasa.
“Hapa kwetu Shinyanga bado ni salama, tunakula kuku wa kienyeji na nyama ya ng’ombe ambao wamenenepesha kwa njia za asili za kulisha majani na pumba isipokuwa kwenye mji wa Kahama ambao kwa sasa unaongoza Shinyanga kwa kuwa na kuku wengi zaidi wa kisasa. Population (idadi ya watu) ni kubwa kiasi kwamba kuku wa kienyeji hawatoshi kulisha mji huo.
“Dar es Salaam ndiko kwenye matatizo, population ni kubwa. Si rahisi kulilisha jiji hilo nyama ya ng’ombe wanaochukua muda mrefu wa miezi saba kuwanenepesha. Wafanyabiashara wanatumia dawa za vitamini kupata matokeo ya haraka.
“Haya ndiyo madhara ya ongezeko la watu, itafikia kipindi ardhi tuliyonayo Tanzania haitatosha kwa shughuli za ufugaji. Hapo ndipo tutalazimika wote kula nyama za mifugo ambayo inakuzwa kwa muda mfupi kwa kutumia dawa,” alifafanua zaidi ofisa huyo.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, mkoa wa Dar es Salaam una idadi ya wakazi 4,364,541. Kati yao, wanaume ni 2,125,786 na wanawake ni 2,238,755.
Chamatata alisema ofisi yake haikuwa na taarifa za kuwapo kwa wafanyabiashara mkoani Shinyanga wanaotumia mbolea aina ya Urea na kemikali kunenepesha ng’ombe na mifugo mingine.
“Kama mna taarifa hizo mniletee tuzifanyie kazi,” Chamatata alisema huku akithibitisha kuwapo kwa changamoto ya wafugaji na wafanyabiashara mkoani humo kutumia dawa za minyoo na unenepeshaji bila kufuata taratibu za kitaalamu.
“Wafugaji wetu wengi hawana elimu, wakati mwingine hawafuati taratibu sahihi za matumizi ya dawa. Katika uchunguzi wetu mwaka huu (2015), kati ya wanenepeshaji wote 149 wa halmashauri nne za Kishapu na Kahama (Kahama ina halmashauri tatu - Ushetu, Kahama TC na Msalala), wawili tu ndiyo waliokuwa na elimu ya kidato cha nne. Wengi walikuwa na elimu ya darasa la saba na baadhi yao hawakupata elimu kabisa.”
NYAMA YA TANZANIA MARUFUKU KIMATAIFA
Kutokana na changamoto hiyo ya elimu, Chamatata alisema baadhi ya mifugo husafirishwa kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine ikiwa kwenye dozi ya dawa mbalimbali, hivyo kuhatarisha afya za walaji wa nyama itokanayo na mifugo hiyo.
“Mbaya zaidi, Dar es Salaam haina hata eneo moja la machinjio yanayokidhi vigezo. Ninaweza kusema hakuna machinjio kwenye jiji hilo...ndiyo maana nyama za mifugo inayochinjwa huko hairuhusiwi kuuzwa nje ya mipaka yetu,” Chamatata alisema.
“Hii ni mada ndefu, lakini kwa kifupi ni kwamba, Dar es Salaam na mikoa mingi Tanzania haina machinjio ya kisasa. Pia unenepeshaji wetu wa mifugo unaanzia kwenye ‘adult age’ (umri mkubwa), hatunenepeshi mifugo kuanzia umri mdogo.
“Tanzania ina machinjio ya kisasa Dodoma, Rukwa, Manyara, Arusha na Mtibwa mkoani Morogoro. Pamoja na kuwa na maeneo haya machache, Tanzania hairuhusiwi kuuza nyama katika maeneo mengi nje ya nchi kwa sababu bado mifugo yetu ina ‘FMD’ (magonjwa ya miguu na midomo), ‘CBPP’ (Homa ya Mapafu), Homa ya Bonde la Ufa na hatujafanikiwa kudhibiti magonjwa ya ngozi kwa mifugo.”
WIZARA YA AFYA
Baadhi ya maofisa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii walisema halmashauri na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wanapaswa kuwajibika kuhakikisha kunakuwa na usalama kwa walaji nyama nchini.
“Sisi tunahusika na sera. Tunashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kutoa mwongozo. Halmashauri na TFDA ndiyo wasimamizi wa utekelezaji wa sera husika. Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003 inaipa mamlaka TFDA kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka taratibu na kanuni za afya,” alisema Jacguiline Makupa, Ofisa Afya wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
TFDA WALONGA
Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwapo kwa wafanyabiashara wa mifugo wanaolisha ng’ombe mbolea aina ya Urea ili kuwanenepesha, ndipo Ofisa Uhusiano wa TFDA, Simwanza, aliposema hawana taarifa hizo.
“Hilo suala la Urea kutumika kunenepesha mifugo ndiyo kwanza tunalisikia. Zipo baadhi ya dawa za vitamani ambazo tumeziidhinisha kutumika kunenepesha mifugo. Kama kuna dawa umezikuta zinatumika huko mikoani zikiwa hazina alama na namba zetu za usajili, maana yake hatujaziidhinisha,” alisema Simwanza.
Kadhalika, aliongeza kuwa Sura Na. 219 ya Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2010, ambayo wengi hupenda kuiita Sheria Na. 1, ndiyo inaongoza kusimamia usalama wa vyakula, dawa na vipodozi. 
“Kwenye machinjio sisi (TFDA) tunawakilishwa na maofisa mifugo na mabwana afya wa halmashauri ambao wanapaswa kuhakikisha usalama wa nyama kabla haijawafikia walaji.” .
UKAGUZI KWENYE MACHINJIO DAR
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwenye machinjio mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ulibaini kuwapo kwa changamoto ya baadhi ya mifugo kuchinjwa na nyama kusambazwa kwa walaji pasi na ukaguzi wa kina wa maofisa wa afya jijini humo.
Aidha, gazeti hili pia lilibaini kuwa machinjio yanayotegemewa kwa kiasi kikubwa Dar es Salaam yaliyopo Vingunguti manispaa ya Ilala, yamekithiri kwa uchafu huku mifereji ya kupitisha damu ikiwa imeziba.
Pamoja na uchafu unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa miundombinu, ilibainika kuwa nyama ilikuwa inabebwa kichwani pasi na kuwapo kwa kifaa cha kuzuia isigusane na nywele wakati ikitolewa eneo la uchunaji ngozi kupelekwa mahali pa kupima uzito, kucharangwa ama kupakiwa kwenye vyombo vya usafiri.
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Ilala, Dk. Sarimbo, alisema wako katika mipango ya kuboresha huduma za machinjio ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watu wote wanaofanya biashara nje ya jengo la machinjio ya Vingunguti.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment