Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, December 22, 2015

Wizara ya Fedha yatoa ufafanuzi mawaziri wa Cuf waliojiuzulu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud
Wizara ya Fedha Zanzibar imesema haiwezi kusitisha malipo ya mishahara na marupurupu ya mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo kutoka Cuf bila wahusika kuandika barua za kuthibitishwa kufutwa uteuzi wao pamoja na kulipwa bila ya kufanyakazi tangu Novemba Mwaka huu.
Mawaziri wa Cuf wametangaza kujivua nyadhifa zao tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka huu.
Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khamis Mussa, alisema wizara haijapokea barua ya kufutwa kwa uteuzi wa mawaziri hao, ndiyo maana wanaendelea kuwalipa stahiki zao zote kama kawaida kupitia benki kila mwezi.
“Anayeteua mawaziri na mwenye mamlaka ya kufuta uteuzi ni Rais. Sisi kama watendaji hatuwezi kusitisha malipo ya waziri bila ya kuwa na maandishi ya kufutwa uteuzi wao,” alisema.
Alisema mvutano kuhusu mawaziri kulipwa mishahara na marupurupu bila ya kufanyakazi ni wa kisiasa zaidi na sio wa kiutendaji.
Mussa alisema mtumishi wa serikali anasimamiwa na Sheria ya Utumishi wa Umma tofauti na viongozi wa kuteuliwa, hivyo hakuna mtu mwenye uwezo wa kufuta uteuzi wake zaidi ya aliyemteua kushika wadhifa husika.
“Mambo haya yapo kisiasa zaidi ndiyo maana hatutaki kuyazungumza kama watendaji wa serikali kwa sababu yapo nje ya uwezo wetu,” alisema Mussa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, alisema mtu mwenye uwezo wa kufuta na kufanya uteuzi wa mawaziri ni Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba.
Alisema pamoja na mawaziri wa Cuf kudai wamejivua nyadhifa zao, lakini bado wanaendelea kupokea stahiki zao na hakuna aliyeandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake pamoja na kukabidhi mali za serikali kwa utaratibu uliowekwa yakiwamo magari.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment