Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, January 22, 2016

Namna Nyerere ‘alivyomzidi kete’ Karume!



MWALIMU Julius Kambarage Nyerere aliyatambua Mapinduzi ya Zanzibar Januari 16, 1964, siku tano baada ya kutokea, wakati Kenya na Uganda zilifanya hivyo saa 24 na 36 tu, kwa mfululizo huo, baada ya kufanyika.

Hii ni baada ya Abeid Amani Karume (Rais), Abdullah Kassim Hanga (Makamu wa Rais) na Abdulrahman Mohamed Babu (Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje) kwenda Dar es Salaam kuonana na Nyerere kumsihi ayatambue pamoja na kuomba msaada wa askari kwenda kutuliza hali, ombi ambalo lilikubaliwa. Siku mbili baadaye, askari polisi 300 wa Tanganyika walipelekwa Zanzibar.

Wakati huohuo, Wakomunisti waliendelea kutamba visiwani ambapo inasemekana Mwanamapinduzi wa Cuba mwenye asili ya Argentina, Ernesto Che Guevara alitembelea Zanzibar kwa siri kutathmini hali baada ya Mapinduzi.

Vituko hivi vilizidi kuzitia kiwewe Marekani na Uingereza. Ili kujiweka karibu na matukio visiwani humo, Marekani ilifungua ubalozi mdogo na kumhamishia Zanzibar mmoja wa majasusi nguli wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Frank Carlucci, akitokea Ureno kudhibiti matukio na kutoa taarifa Washington juu ya kilichokuwa kikiendelea kila nchi.

Kabla ya kupelekwa Ureno, Carlucci alishiriki kwenye ghasia za Congo (sasa DRC) zilizopelekea kuuawa kikatili kwa Waziri Mkuu wa kwanza, Patrice Emery Lumumba kwa mipango ya CIA.

Huko Ureno, alijulikana kwa ukatili wake dhidi ya wanaharakati wa Kikomunisti akapewa jina “The Hangman of Portugal” (Mnyonga Watu wa Ureno). Na baada ya Zanzibar, alipanda cheo kufikia kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa CIA, wakati Jimmy Carter akiwa Rais wa Marekani.

Tatizo kwa nchi za Magharibi kuhusu Zanzibar, halikuwa juu ya kupinduliwa kwa Serikali ya ZNP/ZPPP iliyosimikwa madarakani na Waingereza; bali tatizo lilikuwa juu ya ushawishi wa Wakomunisti eneo hili la Afrika, wakala wao mkubwa akiwa Abdulrahman Babu (Umma Party) na Abdullah Kassim Hanga (ASP).

Hofu ya nchi hizo ilikuwa kwamba, Zanzibar ya Kikomunisti ingetumika kama kituo cha hujuma na operesheni dhidi ya maslahi ya nchi hizo, pamoja na Tanganyika, kuanzia Kenya hadi Rasi ya Tumaini Jema (Cape of Good Hope – Afrika Kusini); na pia kwamba kungeruhusu Wakomunisti wa Kichina (Chicomms) na Wacuba, kuhamishia uwanja wao wa mafunzo kwenye ardhi ya Afrika na kueneza mfano (model) wa kuigwa wa mbinu za kimapinduzi bara zima.

Kenya, Uganda na Tanganyika kwa upande wake, hazikutaka kuona Taifa la Kikomunisti mlangoni pao; na lililowaumiza kichwa zaidi ni hofu ya nchi zao kuingizwa kwenye ulingo wa vita baridi kati ya Magharibi na Mashariki.

Mtizamo wa Nyerere


Nyerere aliona kwamba, tatizo la Zanzibar ya Kikomunisti lingemalizwa kwa njia ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) ambamo Zanzibar (na Wakomunisti wake) ingemezwa ndani ya tumbo isiweze kufurukuta.

Wazo la Nyerere lilidakwa haraka haraka na Marekani kuwa ndilo suluhisho pekee la mgogoro huo, huku wakiamini kwamba, Jomo Kenyatta (Kenya) na Milton Obote (Uganda) wasingepinga wakifahamika kuwa marafiki wema wa Uingereza na Marekani. Isitoshe, Uingereza ilisaidia kuzima maasi ya Majeshi ya nchi hizi tatu yaliyotokea kwa mpigo, siku na saa hiyo hiyo na kwa staili moja dhidi ya Serikali za viongozi hao, Januari 20, 1964; yakazimwa na Majeshi ya Uingereza kwa staili na mbinu zinazofanana.

Kwa kuridhika na mkakati huo, Nyerere sasa alipewa jukumu la kuratibu uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki kuzima “kirusi” cha Zanzibar.

Mwanzoni, Kenyatta na Obote walionesha utayari wa kuunda Shirikisho na hivyo kuwapa matumaini Nyerere, Marekani na Uingereza. Kwa kujawa matumaini hayo, mwanzoni mwa Machi 1964, Nyerere alimwita Karume Ikulu Dar es Salaam, kukamilisha kazi ya kuuza wazo la kuunda Shirikisho la nchi nne – Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar; akamwambia, “Nimeuza wazo hili kwa Kenyatta na Obote, kwamba, sisi Tanganyika tuko tayari kuungana pale Kenya na Uganda watakapokuwa tayari”.

Nyerere akaendelea kumshawishi Karume, akisema: “Na sasa nakuambia na wewe, Sheikh (Karume), kwamba mtakapokuwa tayari Zanzibar, sisi Tanganyika (na Kenya na Uganda) tuko tayari”.
Karume alidakiza, akasema: “Kitu gani hiki kuwa tayari! Sisi tuko tayari moja kwa moja; ita waandishi wa habari sasa hivi tuwatangazie”.

Kauli za viongozi hawa wawili juu ya Muungano, zimepotoshwa mara nyingi kwa maslahi ya kisiasa Visiwani na Tanzania Bara kuonekana kwamba, Nyerere na Karume walikuwa wakizungumzia Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, wakati si kweli. Ukweli ni kwamba, wawili hao walikuwa wakijadiliana juu ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki na si Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ingekuwaje hivyo wakati jana yake tu Nyerere alitoka Nairobi amejawa matumaini ya EAF, mara hiyo ageuke kuzungumzia Muungano wa Tanganyika - Zanzibar ambao haukuwa mawazoni mwake?.

Ikumbukwe pia kwamba, pendekezo la kuunda Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar lilitolewa na Balozi wa Marekani nchini mapema Februari, 1964, lakini (Nyerere) alikataa katakata akidai kuwa EAF ndilo wazo kuu tangu mwaka 1960, lililofikiwa na kuafikiwa kwenye mkutano wa pili wa harakati za uhuru kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (PAFMECA), uliofanyika mjini Mbale, Uganda, Oktoba 1960.

Ukweli ni kwamba, katika kikao hicho Nyerere alikwenda mbali zaidi kwa kupendekeza nchi hizo ziunde Shirikisho hata kabla ya kupata uhuru kamili.
Tumelazimika kuelezea kwa kirefu kipengele hiki juu ya mazungumzo ya Karume na Nyerere, kuonesha kwamba, hadi Machi 1964, Nyerere hakuwa na wazo wala nia ya kuunda kitu kiitwacho “Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”.

Juhudi za kuunda EAF zashindwa


Kwa kipindi chote kati ya Februari/Machi 1964, Nyerere alielekeza nguvu na muda wake mwingi katika kuunda EAF, hivi kwamba wakati wote alikuwa kiguu na njia kati ya Dar es Salaam na Nairobi yalikofanyika mazungumzo mengi juu ya EAF tarajiwa.

Wakati ilipoonekana kila kitu kilikuwa tayari kwa Shirikisho, kikao cha mwisho kilipangwa kufanyika mjini Nairobi Machi 10, 1964 kukamilisha mchakato. Ni katika kikao hiki cha Nairobi, viongozi hao wa nchi tatu za Afrika Mashariki, walipotofautiana na kufarakana na mazungumzo kuvunjika bila mwafaka.

Upinzani mkubwa kwa EAF ulizuliwa na Uganda ikidai kuwa, Shirikisho hilo lilikuwa mbinu chafu za wakoloni kutaka kuwatawala upya kwa mlango wa nyuma; wakati Kenyatta naye alisikika baada ya mchakato kushindwa, akisema hakuwa tayari “kupiga magoti kwa Nyerere”.

Huko Kusini mwa Afrika, juhudi za kuunda Shirikisho kama hilo la “Nyasaland – Rhodesia” (Rhodesia mbili: Rhodesia Kaskazini sasa Zimbabwe na Rhodesia Kusini, sasa Zambia) nazo zilivunjika baada ya Dakta Hastings Kamuzu Banda wa Nyasaland (sasa Malawi) kuibuka na madai kama hayo akifafanua kwamba, “Shirikisho” hilo lilikuwa mbinu ya Ukoloni Mamboleo kutaka kuzitia nchi hizo huru ndani ya kapu moja na kuzidhibiti zisiweze kutumia uhuru ziliopata kujiamulia mambo yake.

Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba, kushindwa kwa juhudi za kuunda EAF na “Nyasaland – Rhodesia Federation”, kulitokana na “mwamko” mpya wa nchi hizo huru dhidi ya ukoloni mamboleo uliozinyemelea kwa kuzitia boriti pamoja, yaani (balkanization) zicheze muziki kwa mdundo wa ukoloni mpya.
Nyerere, Marekani/Uingereza njia panda.

Nyerere alirejea kutoka Nairobi kama mtu aliyefiwa na kwa kuchanganyikiwa, huku nchi za Magharibi zikiendelea kumtahadharisha juu ya hatari ya Wakomunisti kwenye ngazi za mlango wake. Kilikuwa kipindi kigumu na chenye majaribu makubwa kwake.

Nyerere aliona wazi uchanga na udhaifu wa Serikali yake na Serikali kama yake barani Afrika, katika mpambano kama huo. Akaingiwa hofu alipokumbuka kuuawa kwa Waziri Mkuu Patrice Lumumba wa Congo (sasa DRC) mwaka 1961 na Rais Sylivanus Olympio wa Togo mwaka 1963, kutokana na nchi zao kuingizwa katika migogoro ya kimataifa, kati ya nchi za Magharibi na Mashariki, kama ilivyoelekea kutokea kwake.

Akakumbuka pia jinsi alivyookolewa na Majeshi ya Uingereza pale Jeshi lake lilipoasi ambapo, kwa siku nne mfululizo nchi ilikuwa mikononi mwa Jeshi wakati yeye amejificha mahali pasipojulikana. Dhamiri ikamtuma kuona “lazima kitu fulani kifanyike” kwa juhudi na busara zake, kuliko kuwa kibaraka wa mataifa makubwa yenye nguvu za kijeshi.

Haya yakitokea, Marekani na Uingereza zilibakia na uamuzi mmoja tu, nao ni kuivamia Zanzibar kijeshi. Ziliunda mpango wa kijeshi madhubuti kutekeleza hilo, ulioitwa “Zanzibar Action Plan” – ZAP.

Ukweli, tayari Makamanda Wakuu wa Majeshi ya Uingereza – Afrika Mashariki, I. S. Stockwell wa Jeshi la Anga (RAF) na I. H. Freeland wa Jeshi la nchi Kavu, walikuwa wametoa Amri ya pamoja kuweka majeshi yao katika hali ya tahadhari (Joint Operations Instructions), Namba 2/64; huku wakitarajia upinzani mkubwa kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa Zanzibar – ZPLA, likiongozwa na Kamanda Ali Mahfoudh.

Mkakati kuivamia Zanzibar waiva


Mkakati huo ulisukwa kistadi kuonekana kwamba, Uingereza na Marekani hazikuwa na lengo la kuitawala Zanzibar. Hatua ya kwanza ilikuwa kuwaondoa kwa njia yoyote ile, wahafidhina wa fikra na mbinu za kimapinduzi, akiwamo Babu.
Pili, ilikuwa ni kutoa kisingizio cha kuondoa askari 300 wa Tanganyika waliokuwa Zanzibar. Hii ingemwacha Karume hatarini kiusalama wa ndani, na kwa sababu angelazimika kutafuta msaada kutoka pengine.

Njia bora ya kuondoa askari wa Tanganyika iliyopangwa ni kwa Balozi wa Uingereza pamoja na Mkuu wa Jeshi la Tanganyika (T.R.), kumshauri Nyerere aone kwamba, kutokana na hali tete kiusalama nchini Tanganyika kufuatia Jeshi kuasi, Polisi wote wa Tanganyika waliokuwa Zanzibar warejee, na kwamba kama Karume bado alikuwa anahitaji askari kuchukua nafasi yao, mipango ingefanywa kupeleka kikosi cha Askari wa Uingereza.

Kwa kuwa kati ya nchi za Afrika Mashariki hapakuwa na moja yenye utulivu ndani yake kufuatia maasi ya Majeshi yao, Karume asingekuwa na njia, isipokuwa kuwaita Waingereza. Na kama mkakati huu ungepingwa na Karume au Nyerere, Marekani na Uingereza zilikuwa tayari kuivamia Zanzibar kijeshi.

Nyerere alegea


Wakati hayo yakiandaliwa, Waingereza walimtaka Nyerere afikirie juu ya uwezekano wa Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar kwa madhumuni yale yale ya EAF ili Zanzibar imezwe ndani ya tumbo kubwa la Tanganyika. Nyerere kwa hofu ya vita ya kimataifa kupiganwa mlangoni kwake, akalegea na kukubali wazo la Waingereza alilolikataa kabla ya hapo.

Mikakati mitatu ilisukwa kuwezesha hilo. Kwanza, ilikuwa ni kumtumia Nyerere kumshawishi Karume akubali wazo la kuungana, na akikataa, atishie kuondoa Askari wake 300 wa Tanganyika Visiwani ili Karume apinduliwe na mahasimu wake ndani na nje ya ASP na ambao tayari walioanza kuhoji uwezo wake wa kuongoza Serikali ya Mapinduzi.

Pili, kumgombanisha Karume na “Makomredi” wake ndani ya Baraza la Mapinduzi (Babu na wenzake wenye siasa za mrengo wa kushoto), kwa kutoa misaada na kupandikiza hofu kwa Karume kwamba Makomredi hao kwamba walikuwa tishio kwa madaraka na uongozi wake.

Tatu, kuhakikisha kwamba, Zanzibar inamezwa ndani ya Tanganyika kwa njia fulani ya ushirikiano (association), ikiwezekana Shirikisho, kati ya Zanzibar na Tanganyika kama ilipendekezwa mwanzo na Marekani, Februari, 1964.


Mkataba wa Muungano Waandaliwa


Wakati fulani, Aprili 1964, Nyerere alimwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Roland Brown, akamtaka amfanyie kazi moja ya siri “bila mtu mwingine yeyote kujua”. Kazi hiyo ilikuwa ni kuandaa Mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Brown aliwaita Wasaidizi wake na kuwafahamisha juu ya hilo. Hao walikuwa Mabwana Mark Bomani (Mwanasheria) na P. R. N. Fifoot (Mwandishi wa Sheria). Ni Mark Bomani aliyegonga Hati hiyo Muhuri wa “Siri Kubwa”.

Aprili 21, 1964, Nyerere alimwita Dar es Salaam Karume kwenda “bila kufuatana na mtu”. Karume akaoneshwa rasimu ya Mkataba wa Muungano ulioandikwa kwa Kiingereza japo hakujua lugha hiyo.

Na alipojulishwa juu ya kusudio la Muungano, alibisha akidai aachwe kwanza asafishe nyumba yake. Nyerere akavuta mpini wa panga wakati Karume ameshika makali kwa kumtishia kuondoa askari wake 300 visiwani ili mahasimu wake (Karume) “wamchune ngozi”. Karume akasalimu amri hima.

Aprili 22, 1964, Nyerere, akiwa na rasimu ya Mkataba wa Muungano mkononi, alikwenda Zanzibar akifuatana na Roland Brown, Fifoot, Oscar Kambona, Job Lusinde na Bhoke Munanka.

Huko Zanzibar, alipokewa na alikutana na Karume, Abdulaziz Twala, Kassim Hanga na Ali Mwinyigogo, bila kuwepo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (Wolfgang Dourado) ambaye iliagizwa apewe likizo ya lazima hadi mchakato wa Muungano utakapokamilika. Siku hiyo, Mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukatiwa sahihi kwa siri kubwa, kabla ya kutangazwa rasmi hapo Aprili 26, 1964.

Kilichofuata na kinachoendelea ndani ya Muungano huu, ni kile kilichoelezewa na Mhariri wa Gazeti “The Economist” la Juni 1964 kwamba, “Rais huyo (Nyerere) amemudu nusu tu ya kazi ya chatu (ya kumeza mawindo yake); amefanikiwa kummeza mnyama (Zanzibar) bila kuzivunja nguvu za mnyama huyo ambaye bado yu mzima, angali bado anayeyushwa tumboni; uchungu wa mateke yake unaonekana dhahiri ndani ya siasa za Tanganyika na unaweza ukaua”.

“Uchungu wa mateke” anaozungumzia mhariri huyu unawakilisha kero za Muungano ambazo zimeendelea kuyumbisha Muungano huo, tangu mwanzo, hadi leo.

No comments :

Post a Comment