Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Boniface Simbachawene
Historia na Elimu
George Boniface Taguluvala Simbachawene ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Pombe Magufuli akiwa mbunge wa Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma tangu mwaka 2005.
Simbachawene (47) alizaliwa Julai 5, 1968 na alianza elimu ya msingi mwaka 1978 katika Shule ya Pwaga iliyoko wilayani Mpwapwa. Alisoma shule hiyo hadi mwaka 1982 na mwaka uliofuata alihamia Shule ya Msingi ya Mahomanyika iliyoko mkoani Dodoma ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1982.
Elimu ya Sekondari aliipata kuanzia mwaka 1985 hadi 1988 katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mazengo, pia ya mkoani Dodoma. Mwaka 1989 hadi 1993 alikwenda jijini Arusha na kusoma Chuo cha Ufundi cha Arusha ambako alitunukiwa Cheti cha Ufundi (TFC).
Mwaka 2001 hadi 2005 aljiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambako alitunukiwa shahada ya kwanza ya sheria (LLB). Mwaka 2007 alishiriki mafunzo ya kazi na taratibu za uendeshaji wa Kamati za Kibunge kwenye Bunge la Westminister na kutunukiwa cheti na mwaka 2010 alitunukiwa cheti kingine baada ya kuhitimu mafunzo juu ya bunge hilo.
Uzoefu
Uzoefu wa kazi wa Simbachawene unaweza kuwekwa kwenye makundi manne, kwanza ni uzoefu wa kazi za kitaalamu, pili wa kazi za kibunge, tatu ni uzoefu wa kazi za uwaziri na mwisho ni uzoefu wa utendaji ndani ya CCM.
Baada ya kuhitimu na kubobea katika masuala ya ufundi, ilimchukua miaka miwili kabla ya kuajiriwa na kampuni ya mabasi ya Urafiki, tawi la Dodoma mwaka 1995. Alikuwa kondakta, meneja wa kitengo cha ufundi na ofisa usafiri. Mwaka 1997 hadi 1998 aliajiriwa na Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Future World akiwa mwalimu. Kati ya kipindi hicho hadi mwaka 2000, alifanya kazi kama mkurugenzi mtendaji wa shirika la kiislamu la Muzdalifa linalojishughulisha na masuala ya misaada.
Mwaka 2005 Simbachawene, akiwa na miaka 37, aliachana na ‘ukonda’ akaamua rasmi kuitafuta ofisi kubwa ambayo watu wengi waliokuwa naye hawakudhani kama angeliweza kuifikia. Alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa tiketi ya CCM, akamwangusha aliyekuwa mbunge wa Kibakwe na hivyo kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huo.
Mshindani wake mkubwa alikuwa Benson Kigaila wa Chadema na Gabrile Elias Masinjisa wa NCCR Mageuzi. Matokeo ya mwisho yalimpa Simbachawene ushindi wa asilimia 86.1 (kura 37,359), Benson akifuatia kwa asilimia 12.8 (kura 5,542)
Baada ya ubunge wa miaka mitano, Simbachawene alitupa tena karata yake mwaka 2010, na akaibuka kidedea kwenye kura za maoni za kata 13 kati 16 baada ya kupata kura 8,824 huku mpinzani wake, Aggrey Galawika akiwa na kura 2,537 na hivyo, Simbachawene akapata ridhaa ya kuiwakilisha CCM.
Kwa mara ya pili alikumbana na Kigaila wa Chadema, lakini akamshinda tena kwa kupata kura 22,418 sawa na asilimia 77.12 dhidi ya kura 5,585 sawa na asilimia 19.21% za Kigaila.
Mwaka jana, Simbachawene alitupa ndoano yake jimboni Kibakwe kwa mara ya tatu akashinda kwenye kura za maoni kwa kupata kura 18,159 akiwaacha mbali washindani wake sita ambao ni Gabriel Mwanyingi (kura 6,900), Akrei Mnyang’ali (kura 3,563) na Amani Bendera (kura 410).
Kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, alipambana na Mzinga William wa Chadema na kumshinda kwa kura 37,327 sawa na asilimia 81,55 dhidi ya kura 8,447 za mpinzani huyo.
Baada ya kushinda Ubunge mwaka 2010, Simbachawene aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kuanzia Mei 2012 hadi Januari 2014 alipohamishiwa Wizara ya Nyumba na Makazi akiendelea na unaibu.
Januari 2015 alipandishwa na kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu kutokana na sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
JPM alipotangaza baraza lake mwaka jana, Simbachawene alipangwa Tamisemi akiwa waziri.
Ndani ya CCM alianza kama mwanachama na kiongozi wa matawi, likiwamo la Chuo cha Ufundi Arusha kati ya mwaka 1990 hadi alipomaliza. Pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kati ya mwaka 2002 – 2005.
Nguvu
Simbachawene amekuwa mbunge kwa miaka 10 na amekuwa Naibu Waziri na waziri kwa zaidi ya miaka mitano. Uzoefu wa aina hii ni nadra kuupata kwa baadhi ya mawaziri wapya, kila mtu anatarajia kwamba kujiamini kwake kumekua na hata staili yake ya uongozi imeshapevuka zaidi. Kwa kipindi chote ambacho amekuwa mbunge, naibu waziri na waziri, Simbachawene hajawahi kutajwa kwenye kashfa zozote kubwa licha ya wizara alizofanyia kazi kukumbwa na tuhuma kedekede za kashfa dhidi ya viongozi wake wa juu.
Jambo hilo linamfanya kuwa miongoni mwa mawaziri watiifu na waaminifu katika serikali ya JPM, na ambao bado wanaweza kumaliza vipindi vyao bila mazonge na kashfa.
Pili, sifa nyingine kubwa ya Simbachawene ni subira. Watendaji ambao wamefanya kazi naye Wizara ya Nishati na Madini wameniambia kuwa Simbachawene ni mtu mwenye kuuliza kila jambo analotaka kuamua, lakini pia anawasikiliza sana watendaji na wataalamu.
Haiba hii huenda ndiyo imesababisha hadi leo hii Simbachawene ameendelea kuwa na ‘namba ya uhakika’ kwenye mabaraza ya mawaziri hata katika serikali zinazokuja kwa gia ya “kasi” kama hii ya JPM. Wakati alipoachiwa Wizara ya Nishati na Madini kutokana na waziri wake kujiuzulu, wengi walidhani angeanza kwa gia ya kufanya maamuzi lukuki ambayo ndani yake lazima kungekuwa na makosa mengi, badala yake aliongoza kwa utulivu na subira kubwa hadi kumaliza kipindi chake.
Udhaifu
Simbachawene anaweza kukupa mashaka makubwa kwenye aina ya utendaji na uongozi wake katika ngazi ya kufanya maamuzi imara na yanayoacha alama. Siyo mbunifu sana kwenye wizara alizopitia, siyo mtu wa mipango mingi mikubwa. Namuona katika jicho la kufanya kazi za kuelekezwa zaidi kuliko za mipango ya muda mrefu.
Viongozi wa aina hii huingia kwenye kundi la wale wanaoogopa kufanya uamuzi, viongozi wanaoogopa kukosea na kwa hiyo kwao kinga kubwa ni kutofanya uamuzi, jambo ambalo huwa ni salama kwao kuendelea kuwa salama. Pamoja na udhaifu huo, walau kwa hali ya sasa anaweza kupewa muda na nafasi ya kufanya vizuri zaidi ikizingatiwa kwamba wizara yake iko chini ya Ofisi ya Rais na kwa hiyo masuala anayoyashughulikia yako chini ya rais pia. Bahati mbaya aliyonayo ni kwamba aina ya rais wa sasa ni mtu wa kufanya uamuzi na huenda yeye pia atalazimika kuwa mtu wa uamuzi ili kasi za wawili hawa ziendane.
Matarajio
Simbachawene anatarajia kusukumwa zaidi na kasi ya uongozi wa sasa kuliko ilivyokuwa kwenye serikali iliyopita, mawaziri wengi na manaibu wao kwenye baraza la JK wanasema walikuwa na wakati mgumu kila mara kufanya maamuzi kwa sababu ya aina ya rais waliyekuwa naye, alikuwa anawaachia uhuru mkubwa wa kufanya mambo mengi lakini kuna mengine nyeti na muhimu wangeyagusa lazima wangeelekezwa yanapaswa kufanywaje hata kama ilikuwa ni kinyume na fikra zao. Mbinu ya uongozi wa JPM ni tofauti kidogo na lazima itamsukuma Simbachawene kwenye maamuzi ya haraka na yaliyo maarufu.
Wananchi wengi wanasubiri kwa hamu na kwa matarajio makubwa kuiona TAMISEMI mpya, inayoshughulikia masuala ya mipango yote ya elimu iliyo chini ya mamlaka za halmashauri, kata, vijiji, mitaa na vitongoji – kwa kushirikiana na wizara ya elimu. Kinachowavutia wengi ni suala la utoaji wa elimu bure na utaratibu utakavyokuwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu ambapo utaratibu huo unaanza, wengi watampima sana Simbachawene katika eneo hili na kuanza kujua mwelekeo wake na wa wizara yake utafanikiwa kwa kiasi gani katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Changamoto
Changamoto ya kwanza inayomkabili Simbachawene na wenzake wa Tamisemni ni namna gani watakuza ufanisi wa utendaji katika halmashauri na serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Ukienda katika halmashauri zetu unabaini kuwa kuna upungufu mkubwa wa watendaji na jambo hilo ni dhahiri kuwa linakwaza na kukwamisha juhudi za watu wa chini kujiletea maendeleo kupitia mfumo wa uongozi waliowekewa. Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi ambazo hata kwenye ngazi ya chini kuna urasimu uliopitiliza. Unakuta mwananchi anazungushwa kuandikiwa barua ya kwenda mahakamani hadi atoe rushwa.
Lakini hiyo ni tisa, kumi ni namna gani ambayo watendaji wa mamlaka hizi wametelekezwa. Mathalani, wenyeviti wa vijiji na mitaa wanafanya kazi kubwa ya kuhamasisha jamii na kuifanya ipige hatua, kwa hiyo ndio watekelezaji wakubwa wa masuala yote muhimu ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia, lakini nani amewahi kufikiri kuwa viongozi hawa wanapaswa kulipwa walau mshahara wa kila mwezi ili kujikimu na kufanya kazi kwa ubora zaidi?
Simbachawene anapaswa kuja na mipango ya muda mrefu juu ya namna gani tutakwamua ufanisi wa utendaji wa ngazi ya chini.
Kuna suala la utoaji wa elimu bure ambalo limeshatafutiwa ufumbuzi na kama tulivyosema tunasubiri kuona aina ya usimamizi wake kwa ujumla. Lakini vipi kuhusu chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wengi wao wanatoka kwenye familia maskini. Mmoja wa wachumi nguli na mwanasiasa wa upinzani nchini, Profesa Ibrahimu Lipumba mara kadhaa amewahi kutoa takwimu za kitaifa na kimataifa kuonyesha athari za ubongo anazozipata mtoto anayekaa darasani na njaa kama ilivyo kwa watoto wengi wanaokwenda kupata elimu bure.
Ni lini serikali itaanzisha programu ya kuwapa watoto chakula angalau cha mchana kila siku ili wengi wapate motisha na wajenge ubongo wao wakifikiri zaidi masomo kuliko njaa? Mwenye majibu ya maswali muhimu kama haya ni Simbachawene.
Nenda maeneo mengi kaangalie hali ya nyumba za walimu, utasikitika sana. Hazifai na hazifai hata kidogo. Mwenye jukumu la kuhakikisha walimu wanakaa kwenye makazi bora ni Simbachawene na wizara yake kwa kushirikiana na wizara ya elimu. Ni lini basi walimu watatulia kwenye madarasa na kufundisha bila kutoka kilomita 10 mbali na shule? Hizi ni changamoto za wazi ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka ili kuona elimu yetu inakua.
Mishahara na stahili sahihi imebaki kuwa changamoto ya kudumu. Ukienda kijijini au mjini ukapewa mshahara wa mwalimu ukaambiwa uishi hata kama ukiwa mwenyewe, unaweza kutoroka. Tunajiuliza hawa walimu wenye wake na waume zao na watoto wanawezaje kustahimili hali hii?
Moja kati ya mambo ambayo kila Mtanzania anataka kuyaona ndani ya miaka mitano ijayo ni uboreshaji wa mishahara na stahili za walimu. Mwalimu mmoja wa Wilaya ya Bagamoyo ameripoti kwangu kwa vielelezo kwamba tangu mwezi Septemba 2015 hadi hivi leo yeye na wenzake hawajalipwa mishahara yao (takribani miezi mitatu). Watumishi wa namna hii wanaishi namna gani? Wakaibe wapi? Wafanye nini? Simbachawene anayo kazi ya kufanya kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) umeishia wapi? Unatekelezwa kwa kiwango gani? Hili ni jambo jingine kubwa lisilofanyiwa kazi na likijaribu kufunikwa. Ukiongea na walimu vijijini wanakwambia mpango kama huo na mingine mingi ya aina hiyo ni ‘miradi ya wakubwa’ na haina lolote la kufanya katika elimu. Mipango ya namna hiyo imekuwepo kwa muda mrefu lakini imekamilika na kuacha wao hawana nyumba, hawana mishahara bora, hawana vifaa vya kufundishia na hawana nafasi za wazi kuongeza ujuzi. Ofisi ya Rais na waziri mwenyewe wanapaswa sasa kuikagua miradi kama hii ambayo ni mtambuka na kuona ikiwa imekuwa na tija kwa taifa na kwa sekta nyeti za nchi yetu.
Tusisahau pia kwamba masuala maji, ufugaji na afya yanashughulikiwa pia na Tamisemi kwa ngazi za halmashauri, kata, vijiji na vitongoji. Watendaji na watumishi wa Tamisemi wanafanya kazi hii moja kwa moja kwa kushirikiana na watendaji wa wizara zinazohusu maji, ufugaji na afya walioko katika ngazi za chini.
Sekta zote nilizozitaja hapa zina matatizo lukuki na ya muda mrefu. Tamisemi kama mdau mkubwa na Simbachawene kama waziri wake wa sasa anayo kila sababu ya kuhakikisha changamoto husika zinamalizwa kwa wakati.
Hitimisho
Unapokabidhiwa wizara ya aina ya Tamisemi unaweza kumalizika kabisa kisiasa ikiwa hautazikabili changamoto zilizopo. Simbachawene anao uwezo wa kukimbizana na matatizo yaliyoko kwenye maeneo muhimu ya Tamisemi nchini ikiwa atakuwa na uongozi wa ushirikishaji kama alivyosifika Wizara ya Nishati na Madini, lakini naamini anapaswa kubadilika sana.
Anapaswa kuchangamka, kukimbizana, kufuatilia kwa nguvu na kujifunza takwimu na umuhimu wake. Haya ni mambo ambayo bado kwa kiasi kikubwa hata anapoongea na kutoa maelekezo kwa watendaji wa chini yake, unaweza kugundua kwamba anayakosa na kwa asili ya wizara hii, yanaweza kumgharimu. Jambo kubwa linalomsaidia ni kwamba amekuwemo serikalini kwa miaka kumi sasa, anayajua haya na anajua ndiyo siri ya kufanya mabadiliko makubwa katika serikali aliyomo.
Namtakia kila la heri.
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi.
Kuhusu mchambuzi
Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana cheti cha juu cha sarufi (“Adv Cert of Ling”), shahada ya sanaa (B.A) katika elimu (lugha, siasa na utawala), shahada ya umahiri (M.A) katika usimamizi wa umma na shahada ya sheria (LLB);
Simu +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com, https://www.facebook.com/JuliusSundayMtatiro/. .
No comments :
Post a Comment