
Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Muhangwa Kitwanga.
HISTORIA NA ELIMU
Charles Muhangwa Kitwanga ni Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Pombe Magufuli. Yeye ni mbunge wa Jimbo la Misungwi, mkoani Mwanza tangu mwaka 2010 hadi sasa. Kitwanga ana umri wa miaka 55 na ifikapo Septemba mwaka huu atafikisha miaka 56 kwani alizaliwa Septemba 27, 1960 mkoani Mwanza.
Kitwanga amepata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Busagara iliyoko mkoani Mwanza kati ya mwaka 1970 hadi 1976, akaendelea na elimu ya sekondari kwa kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Same iliyopo mkoani Kilimanjaro kuanzia mwaka 1977 hadi 1980. Kisha alisoma na kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Tosamaganga mkoani Iringa, kati ya mwaka 1981 hadi 1983.
Kitwanga aliendelea na taaluma ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aliingia mwaka 1985 akichukua Shahada ya Sayansi, akahitimu mwaka 1988.
Miaka miwili baadaye, yaani mwaka 1990 alikwenda nchini Uingerea katika Chuo Kikuu cha Essex na kusomea Shahada ya Sayansi ya Umahiri (Uzamili) na kuhitimu akibobea kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari (IT), mwaka 1990 hadi 1991.
UZOEFU
Kitwanga alianza kupata uzoefu wa kazi mara alipohitimu kidato cha sita kwani aliajiriwa na Kampuni ya Usafirishaji ya Kauma akiwa Ofisa Usafirishaji Msaidizi na kufanya kazi hiyo kati ya mwaka 1984 hadi 1985.
Ajira yake ya kwanza iliyotokana na ubobezi wake kwenye masuala ya IT ilikuwa ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliajiriwa mwaka 1988 akafanya kazi hadi 1992 katika nafasi ya Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari.
Kuanzia mwaka 1992 hadi 1998 akiwa hapo BoT, alihamishiwa kitengo cha utawala na kufanya kazi kama Ofisa Utawala wa Benki. Alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 12 mfululizo, kuanzia mwaka 1998 hadi 2010, alipopandishwa cheo na kufanya kazi akiwa Naibu Mkurugenzi wa benki hiyo, akijihusisha na eneo la Uundaji wa Mifumo na Utawala.
Mwaka 2010, Kitwanga aliamua kujitosa kwenye kura za maoni ndani ya CCM ili kuwania ubunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza. Kwenye kura za maoni, alifanikiwa kumshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na mtu aliyekuwa akitetea nafasi yake, Jacob Shibiliti pamoja na mshindani mwingine wa karibu, Madoshi Makene.
Mwaka huo wa 2010, Kitwanga au kwa jina la utani ‘Mawe Matatu’, aliingia kwenye uchaguzi wa jumla na kuiweka juu CCM kwa kupigiwa kura 41,935 sawa na asilimia 83.24 huku mshindani wake kutoka Chadema, Jane Kajoki akipata kura 5,293 sawa na asilimia 10.51 na Abdallah Mtina wa CUF alipata asilimia tatu ya kura zote.
Miaka mitano ya mwanzo ya ubunge wa Kitwanga (2010– 2015), ilifuata kwa kumuweka juu katika siasa za Tanzania. Rais Jakaya Kikwete wakati huo, akamteua kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, kuanzia Novemba 2010 hadi Machi 2012, kisha akahamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais na kuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia mwezi huo hadi Januari 2014 na kuanzia Januari 2014 hadi Novemba 2015, amekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Agosti mwaka 2015, Kitwanga alishiriki kwa mara nyingine kura za maoni ndani ya CCM ili atetee kiti chake cha ubunge wa Misungwi ambako akashindana na kumshinda hasimu wake kisiasa, mbunge wa zamani wa Misungwi, Jacob Shibiliti. Kitwanga alipigiwa kura 26,171 sawa na asilimia 69.9 huku Shibiliti akipata kura 7,009 sawa na asilimia 18.
Kwenye uchaguzi wa jumla uliofanyika Oktoba 25, 2015 Kitwanga alishinda tena kwa kupigiwa kura 72,072 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Leonidas Kandela wa Chadema, aliyepigiwa kura 18,050 na kuwa wa pili.
Baada ya ushindi wake wa ubunge wa mara ya pili, ndipo Rais JPM akamkabidhi Kitwanga Wizara ya Mambo ya Ndani akawa waziri, akichukua mikoba ya Mathias Chikawe, aliyehudumu kwenye wizara hiyo nyakati za mwisho za Rais Kikwete.
Ndani ya CCM, Kitwanga amekuwa na uzoefu wa muda mrefu. Kwanza amekuwa mlezi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wilayani Misungwi kuanzia mwaka 2006, halafu akawa mjumbe wa Baraza la Wilaya la CCM mwaka 2008, kisha akateuliwa kuwa Kamanda wa UVCCM wa Mkoa wa Mwanza mwaka 2009.
NGUVU
Kitwanga ni mtu mwenye elimu thabiti. Hakusoma kwa kuunga unga au kuokoteza vyeti huku na kule. Amesoma kwa kina na katika taasisi zinazoeleweka, lakini pia ameitumia elimu na ubobezi wake katika taasisi nyeti ya Serikali, BoT. Ubora wake kwenye utendaji kiasi kikubwa unasaidiwa na uwezo wake wa elimu, pamoja na utulivu. Unaweza kujiridhisha kwa namna kiongozi huyu alivyopandishwa nyadhifa kwa utaratibu akiwa palepale BoT hadi kuwa Naibu Mkurugenzi, alipotoka BoT akahamia kwenye siasa ambako nako ameendelea kuwika bila kuchuja. Kitwanga anaweza kuwa na safari nzuri kisiasa mbele ya safari.
Nguvu nyingine ya Kitwanga inatokana na uzoefu wa kufanya kazi ndani ya Bunge na serikalini huku akibadilishiwa maeneo ya kufanyia kazi bila kuondolewa moja kwa moja. Amekuwa mbunge kwa miaka mitano, lakini pia amekuwa waziri kwenye wizara tatu tofauti, hamishahamisha ya namna yake mara nyingi huwa ni ile ya mteuzi kuhitaji anayehamishwa akafanye maboresho katika eneo lililokwama. Baadhi ya watu wa serikalini wanamuona kama “kiraka”, mimi sijathibitisha “u-kiraka” huo na huenda tukaupima kwenye miaka mitano ijayo, lakini tunakubaliana kwamba huyu ni mmoja kati ya mawaziri wasio maarufu sana, lakini ni watendaji wazuri na wanaohitajika.
Nguvu nyingine ya Kitwanga ni kujiamini na kutoyumba. Niliwahi kupita jimboni kwake mwaka 2014 nikifanya utafiti na kuwauliza vijana wengi juu ya mbunge wao, karibu wote walisisitiza wangelimchagua tena kwa sababu wanadhani kuwa kati ya wabunge wote ambao wamekuwa nao Misungwi, huyu ndiye aliyesimamia zaidi maendeleo kuliko wengine. Nilipofanya uchambuzi wa majimbo yote nchi nzima, Jimbo la Misungwi nilieleza dhahiri kuwa kwa Mwanza hakuna namna upinzani utaweza kufanya vizuri.
Kujiamini kwa Kitwanga kuko dhahiri sana, mwaka jana (2015) alipoulizwa na moja ya vyombo vya habari juu ya mipango yake kisiasa, Kitwanga alijibu: “Mimi sina sababu ya kutangaza nia, nitaendeleza ubunge. Kwa sasa ninapanga mikakati ya maendeleo ya wana-Misungwi kwa kipindi kijacho baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2015.” Kauli hiyo ya Kitwanga unaweza kuitafsiri kama iliyotolewa na mtu anayejiamini katika mipango yake, hakutaka kuongelea namna atakavyopambana na wenzake, lakini anajadili namna atakavyoongoza miaka mitano inayofuatia.
UDHAIFU
Tatizo moja la Kitwanga ni kwamba, hawezi kujiepusha na migogoro na hana mbinu hizo. Mathalani, alipokuwa mbunge na Naibu Waziri ndani ya kipindi kilichopita, amewahi kutambiana na viongozi wenzake akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi. Wawili hao waliingia kwenye migogoro ya muda mrefu, ambayo ilifikia wakati ikaiyumbisha kabisa Misungwi. Yeye kama Naibu Waziri, hakuchukua hatua za kiuongozi za kutatua migogoro hiyo, badala yake alilaumiwa na wanaCCM wengi ndani ya jimbo na mkoa kwamba hawezi kukwepa lawama.
Juhudi za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa wakati huo kutatua mzozo huo wa Misungwi ziligonga mwamba na baadaye mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi ‘alizushiwa’ tuhuma za rushwa na ufisadi na akaondolewa kwenye nafasi yake.
Baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya ya Misungwi wanasema kilichomtoa mwenyekiti huyo siyo rushwa wala ufisadi, bali ni kushindana kwake na Kitwanga. Pamoja na kwamba nilipoomuliza Kitwanga juu ya tuhuma hizo hakunijibu chochote, ukweli unabakia kwamba lazima ajitathmini namna anavyoweza kutoa uongozi na kujipunguzia migogoro na maadui kwenye majukumu yake.
Wizara anayokabidhiwa Kitwanga sasa haihitaji tabia za migogoro, kushughulikiana na kulipiza kisasi. Hii ni wizara ambayo pia inavyo vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa hiyo, anao ushawishi mkubwa kwa vyombo hivyo na muhimu akajivua watu wote aliodhani ni maadui zake kisiasa au wale watakaojitokeza na afanye kazi kwa misingi ya kazi yake, ili asije kuhusishwa tena kwamba kuna watu anawapiga vita siku za usoni kwani kwa asili ya Serikali aliyomo, yeye ndiye anaweza kujikuta anaanguka.
MATARAJIO
Matarajio ya Kitwanga ni makubwa, kwamba anayo fursa ya kipekee ya kurekebisha vyombo vya utendaji vya ulinzi na usalama wa raia katika wakati anaofanya kazi chini ya Rais anayejitambua na ambaye amekwishatangaza vita dhidi ya rushwa, ufisadi, uzembe na mambo kama hayo. Hiyo ina maana kwamba Kitwanga atakuwa na kazi ya kumsaidia rais wake kila kukicha, lakini analo jukumu la kuwa mstari wa mbele kufanya kabla hajatumwa na mkubwa wake.
Watendaji wengi wa wizara yake wanayo yao ya moyoni. Wanasema wanasubiri kuona waziri wao atakuwa karibu na wao kwa kiasi gani. Changamoto kubwa ambayo wengi wamekuwa wanakumbana nayo ni kuwekwa kando na mawaziri wa wizara hii (wengi kati ya waliopita). Wanasema ifikie wakati wanasiasa wanaopewa uwaziri wa Mambo ya Ndani wajue kuwa askari siyo jiwe bali ni mtu anayetii amri, lakini anapaswa asikilizwe na atimiziwe mahitaji yake muhimu Askari nao wana maisha baada ya uaskari, wanapaswa kurudi uraiani. Wengi wanatarajia kuona hatua zaidi zinachukuliwa ili kuboresha maisha yao.
CHANGAMOTO
Dawa za kulevya ni changamoto ya dhahiri ambayo inabaki kuweka doa katika taifa letu. Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani alitangaza kuwa anawafahamu watu wanaouza na kusambaza dawa za kulevya na aliahidi kuwa atapambana nao. Vita aliyoitangaza iliahirishwa kimya kimya na matajari wa dawa za kulevya wameendelea kuwa mabosi katika miji yetu. Athari za dawa hizo zinafahamika vizuri na hazihitaji kuelezewa. Kitwanga anayo kazi ya moja kwa moja ya kujivika kazi ya kupambana na watu wanaojihusisha na biashara hii mbovu kwa ukuaji wa maendeleo, ustawi na uimara wa taifa letu. Na yeye asije tena na vijisababu kuwa bado wanachunguzwa kwa sababu Rais Kikwete aliwahi kusema anayo orodha yao, uchunguzi ulishakwisha sasa tunahitaji kuona watu hawa wakifikishwa kwenye mkono wa sheria, siyo kila kukicha tunaona vijidagaa vikisombwa mahakamani.
Wahamiaji haramu ni changamoto nyingine dhahiri ambayo Kitwanga na wenzake wanalo la kufanya. Sote tunafahamu kuwa hivi sasa Tanzania kila anayetaka kuja kukaa, kufanya biashara, kuuza karanga na hata ndizi anakuja na anafanya anachotaka. Sera zetu zimelegezwa mno kiasi kwamba hata ajira za vijana wetu zinawekwa mashakani kwani zinachukuliwa na watu wanaotoka nje ambao hawakustahili kuja kuzifanya. Nchi hii inahitaji wageni ambao watatoa ajira za maana, hatuhitaji mwekezaji atoke uchina aje kufungua duka la simu Kariakoo, mtaji wa kufungua duka la simu mamilioni ya Watanzania wanao ila wanachokosa ni “fremu” za kufanyia hivyo hapo Kariakoo. Kitwanga na wenzake wanayo kazi ya kuhakikisha kuwa kila mtu anayekuja kuishi ndani ya nchi yetu anakuwa na biashara imara ambayo itatoa ajira za kutosha kwa vijana wetu. Waliobaki kwa maelfu ambao wamekuja ‘kukuyanga’ ni vyema wakarudi makwao.
Ushiriki wa polisi kwenye hujuma za uchumi wa nchi ni changamoto nyingine dhahiri. Tunaambiwa makontena yanaibiwa bandarini, wananchi wanapigwa risasi mbele ya benki, majambazi wanavamia na kutawala mahali kwa saa tatu na upuuzi mwingine kedekede. Haya yote yanatokea kwenye maeneo ambako polisi wapo na silaha za moto wanazo. Polisi ni washiriki wakubwa katika njia za uhujumu wa uchumi na wanafanya hivyo kila wanapojisikia. Kumekosekana mtu wa kuwafuatilia na kuchukua hatua na ndiyo maana nchi yetu haiishiwi kashfa. Kitwanga na wizara yake wanayo kazi ya kubadilisha hali hii, Jeshi la Polisi lirejeshwe kwenye maadili ya ulinzi wa raia na mali zao na si kusindikiza misafara ya wahujumu uchumi wapitishe salama magendo yao.
Changamoto ya polisi kuwa mbali na jamii wanayoilinda ni kitu kingine kikubwa. Ukienda katika nchi nyingine, polisi ni rafiki wakubwa wa raia na raia wanaviona vituo vya polisi kama mahali pa kupata haki na pa kukimbilia. Hapa kwetu kijana anaweza kukatwa panga na ‘Panya Road’ akakimbilia kituoni kuomba msaada ili akapate matibabu, polisi wakamuweka ndani ili wachunguze kama kijana huyo naye ni ‘Panya Road’. Mbinu za jeshi letu zimekuwa za zamani hadi zinakera na huu ni ukatili mkubwa kwa raia wanaotafuta msaada wa polisi. Lazima sasa jeshi letu liache kuwa ‘POLICE FORCE’ na liwe ‘POLICE SERVICE’, liwe na kazi ya kutoa huduma ni si kuadhibu raia. Kitwanga anayo kazi ya kulibadilisha kisera na katika mbinu za ufanyaji kazi. Tunataka kuona jeshi la kisasa, linalojitambua na ambalo litakuwa rafiki kwa wananchi.
Kuzingatia maslahi ya askari wa vikosi vyote vilivyo chini ya wizara ya mambo ya ndani na kuwajengea miundimbinu mizuri ya kazi ni jambo lingine. Hawa ni watu muhimu sana ambao lazima maslahi yao yatazamwe. Haiwezekani unamuweka mpakani askari wa uhamiaji anazuia bidhaa za magendo zisizolipiwa ushuru za shilingi bilioni moja wakati yeye kwa mwezi unamlipa shilingi laki tano. Lazima tujitathmini tena na kukumbuka kuwa moja kati ya mambo ambayo yanashamirisha rushwa hapa nchini ni kutotosheka kwa watendaji wetu na ugumu wa maisha unaowakabili. Ikiwa tunataka kukuza taifa kiuchumi na kuwafanya askari wetu waanze kuzoea kuwa waaminifu ni lazima tuboresha maslahi yao ya kazi na tuwalipe vizuri.
Mwisho, Kitwanga anayo changamoto ya kuvifanya vikosi vya usalama vilivyo chini ya wizara yake visifanye kazi kwa maagizo ya kisiasa, bali yawe ya kitaalamu. Jeshi la Polisi hivi sasa lina wataalamu chungu mbovu, usalama wa taifa pia wamejazana wataalamu wa kutosha. Lakini bado vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya maamuzi ya ajabu ajabu kila kukicha. Vinasubiri na kutii amri za wanasiasa kila mara na bila kujali weledi wa kazi zilizoko mbele yao. Ndio maana kati ya mambo ambayo Kitwanga anakwenda kupimwa nayo ni pamoja na hilo, Je, atalitumia Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa kama vyombo vya kufanya propaganda za chama kinachoongoza dola? Au atapambana kuhakikisha vinaheshimiwa na kazi yao inaachwa kwenye ulinzi na usalama wa taifa?
HITIMISHO
Kitwanga siyo maarufu sana kwenye siasa za Tanzania. Lakini ni mwanasiasa mzoefu ambaye amekuwa mtendaji ndani ya Serikali katika kipindi kirefu. Wizara aliyokabidhiwa ni mzigo mzito kuliko zote alizowahi kupitia huko nyuma. Akicheza vibaya lazima ataanguka kama ambavyo wenzake wengi tu wamewahi kuanguka huko nyuma. Masuala ya ulinzi na usalama wa raia yanaweza kukuweka nje hata kama hukusika na yale yaliyotendwa na vyombo hivyo, kila mara anapofanya kazi zake akumbuke yaliyowatokea kina Rais Mwinyi miaka ya sabini. Namtakia kila la heri.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi
KUHUSU MCHAMBUZI
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; juliusmtatiro@yahoo.com).
No comments :
Post a Comment