
Kada wa CCM, Pius Ngeze, akifafanua jambo wakati akihojiwa na gazeti hili mkoani Kagera hivi karibuni. Picha na Phinias Bashaya
Ingawa kwa baadhi ya watu siasa ni mchezo mchafu, kwa Pius Ngeze (73), kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM )aliyeshiriki kwenye harakati za siasa za serikali za awamu zote tano, hali ni tofauti.
Ngeze, ambaye amewahi kuwa mbunge wa Ngara kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2000 kwa tiketi ya CCM, anasema siasa ni nzuri ikimpata kiongozi sahihi. Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mkoani Kagera hivi karibuni, kada huyo mkongwe ametaka Rais John Magufuli akabidhiwe uenyekiti wa CCM ili akisafishe na kukisuka upya chama hicho.
Ngeze anasema wakati Rais Magufuli akiendelea ‘kutumbua majipu’ kwenye sekta na idara za umma, akumbuke kuwa hata ndani ya CCM yapo majipu yanayohitaji kupasuliwa ili kukiboresha zaidi chama hicho.
Kwa utaratibu wa CCM, Rais hukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi unaofanyika baada kuingi Ikulu, ingawa katika miaka ya karibuni Rais anayeondoka madarakani huachia mapema uenyekiti.
“(Magufuli) Akipewa uenyekiti wa chama lazima watendaji wabadilike na kwenda sambamba na kasi yake kama inayoonekana serikalini. Atapunguza uteuzi wa kupeana zawadi na vitendo vya rushwa hasa katika chaguzi,’’ anasema.
Ngeze anasema iwapo Magufuli atakuwa mwenyekiti wa CCM kabla ya mwaka 2017, atakiwezesha chama kuajiri watumishi wenye elimu ili kuendelea kumudu ushindani wa vyama uliopo. Pia, anasema Rais atakapokabidhiwa chama ahakikishe kinakuwa na vyanzo vingi zaidi vya mapato tofauti na sasa kinategemea ruzuku kutoka serikalini.
Ngeze anasema kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha, baadhi ya vikao na shughuli nyingine za chama zimekuwa zikifanywa kwa ufadhili wa wenyeviti, huku baadhi ya watendaji wakiwa waoga kubuni vyanzo vya mapato.
Pia, anasema haridhishwi na utaratibu wa kupata wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ulioanza miaka michache iliyopita.
“Muundo wake ni gharama kubwa kwa chama kwa kuwa mjumbe anatoka kila wilaya tofauti na zamani alitoka kila mkoa, mfumo wa sasa unatakiwa utazamwe upya ili kubana matumizi,’’ anasema.
Alimpigia kampeni Rais Kikwete
Mzee huyo mwenye miaka 73, anasema wakati wa kampeni za kuwania muhula wa pili wa Rais Jakaya Kikwete, alikuwa kiongozi wa timu ya ushindi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Ngeze anasema amekuwa akishiriki kwenye kampeni hizo miaka yote tangu alipoanza kujihusisha na siasa na katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, aliteuliwa kuwa kiongozi wa timu ya ushindi ya Rais Magufuli.
Alimuunga mkono Lowassa
Katika mchakato wa uchaguzi wowote wenye ushindani unaowakutanisha wagombea wenye sifa na mvuto tofauti, ni vigumu kukwepa kuibuka kwa makundi yanayomuunga mkono mgombea fulani.
Katika mrengo huo, harakati za kumpata mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, wanachama wa chama hicho walikuwa katika makundi tofauti; Ngeze alikuwa miongoni mwa wanachama waliomuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Mzee huyo, ambaye mpaka sasa anajivunia kumuunga mkono Lowassa aliyeenguliwa na chama hicho katika hatua na awali na kujiunga na Chadema kisha kupewa nafasi ya kugombea urais chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anasema ushabiki wake kwa Lowassa haukuwa wa siri.
“Wakati wa kutafuta mgombea wa chama nilikuwa upande wa Edward na wala halikuwa jambo la siri ila baada ya uteuzi wa mgombea wa chama chetu tuliungana na kuanza kuinadi ilani ya chama na kutafuta kura,’’ anasema.
Hata hivyo, Ngeze anasema kuwa CCM ilipata wakati mgumu kwenye kampeni kutoka kwa wapinzani wake takribani katika majimbo yote ya Mkoa wa Kagera, ambayo ilikwenda kuomba kura za wananchi.
“Uchaguzi ulikuwa mgumu na mzito; kusema hilo halikuwapo ni kujidanganya. Kampeni zilikuwa ngumu kutokana na wagombea urais wawili kuwa na nguvu na baadaye mgombea wa CCM ndiye aliaminiwa na wananchi,’’ anasema.
Amsifu Jakaya Kikwete
Mwanasia huyo ambaye aliingia kwenye siasa baada ya kuacha kazi ya utumishi wa umma, anasema kwamba utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ameacha mambo mengi ya kujivunia ambayo yanajenga msingi imara kwa Serikali ya sasa na nyingine zijazo.
Anasema uwekezaji unaoendelea kufanyika nchini katika sekta mbalimbali ni matokeo ya ziara za Rais huyo mstaafu nje ya nchi alikokutana na watu mbalimbali na kufanya nao mazungumzo.
Anasisitiza kuwa licha ya baadhi ya watu kukosoa safari za nje ya nchi wakati wa utawala wake, matokeo ya mazungumzo yaliyofanyika huko yataendelea kulinufaisha taifa kwa miaka mingi ijayo.
“Naomba Watanzania wasisahau Rais Kikwete amezunguka nchi mbalimbali duniani na kupata wawekezaji. Kuna miradi ya bandari hata kiwanda cha saruji (Dangote) ni matokeo ya ziara zake na wanaobeza juhudi zake wana sababu zao,’’ anasema.
Anaongeza kuwa uwekezaji mkubwa unaofanyika nchini katika sekta ya afya unalenga kupunguza gharama kwa wagonjwa kutafuta matibabu nje ya nchi ni juhudi kubwa zilizofanywa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mgogoro wa Zanzibar
Msimamo wake kuhusu mgogoro wa kisiasa unaofukuta Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi na kutangazwa kwa tarehe mpya ya kufanyika marudio, mzee huyo anataka uwapo umakini mkubwa kwa kuwa upande mmoja wa Muungano ukikosa amani upande wa pili hauwezi kuwa salama.
Anaamini kuwa kinachoendelea katika visiwa hivyo wakati huu ni jambo linalotakiwa kuungwa mkono na kila mwananchi kwa kutumia njia mbalimbali ili kuwezesha upatikanaji wa amani ya kudumu.
Pamoja na kusifu jitihada za utawala wa Awamu ya Nne uliowezesha kuundwa kwa SUK) Visiwani Zanzibar kati ya pande zenye, mwanasiasa huyo mstaafu anazitaka tume zinazoundwa kwa ajili ya kutafuta suluhu kwa kutumia kodi za wananchi kuhakikisha zinaweka wazi majibu ya matokeo ya vitu walivyovibaini katika uchunguzi wao.
Anasema siyo jambo jipya Serikali kuunda tume kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro fulani, hivyo mambo yanayobainika kwenye taarifa za tume hizo ambayo si lazima kufanywa siri badala yake yawekwe wazi kwa wananchi.
Anapendekeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Magufuli iunde tume ambayo itafanya kazi kwa kuzingatia tija na kubana matumizi ambayo ni kodi za wananchi huku wakijua kwamba kufungia taarifa za tume kabatini ni kuwanyima haki wananchi.
No comments :
Post a Comment