
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Devis Mwamunyange akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
By Elizabeth Edward
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameendelea kupanga safu za taasisi za Serikali baada ya kufanya uteuzi wa maofisa mbalimbali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), huku akimuongezea muda Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Akitangaza mabadiliko hayo, Jenerali Mwamunyange, ambaye ameongezewa mwaka mmoja, alisema uteuzi huo umefanywa kuziba nafasi za maofisa waliostaafu kwa mujibu wa sheria, na walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.
Mwamunyange, ambaye alitakiwa kustaafu leo Januari 31 sambamba na maofisa wengine, ataendelea kulitumikia jeshi hilo mpaka Januari 31 mwakani.
Aliwataja walioteliwa kuwa ni Luteni Jenerali Venance Mabeyo anayekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenereali Samwel Ndomba aliyemaliza muda wake wa utumishi.
Wengine ni Meja Jenerali James Mwakibolwa aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Meja Jenerali Salum Kijuu aliyestaafu.
Aliyekuwa Mratibu Msaidizi Mkuu wa Baraza la Usalama la Taifa, Meja Jenerali Yakub Sirakwi ameteuliwa kuwa mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (Commandant NDC), nafasi iliyoachwa na Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliyeteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mwamunyange alisema Brigedia Jenerali George Ingram ameteuliwa kuwa mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Meja Jenerali Joseph Kapwani anayestaafu.
Nafasi ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa imekwenda kwa Brigedia Jenerali Mwita Isamuhyo, baada ya Meja Jenerali Raphael Muhuga kumaliza muda wake wa utumishi jeshini.
Aliyekuwa mkuu wa utawala na mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Jacob Kingu ameteuliwa kuwa mkuu wa Shirika la Mizinga, nafasi iliyoachwa wazi na Meja Jenerali Charles Muzanila anayestaafu.
Mwamunyange alisema Brigedia Jenerali Robison Mwanjela anakwenda kuwa mkuu wa Chuo cha Tiba cha Lugalo, nafasi iliyoachwa wazi na Brigedia Jenerali L.S Msangi.
Katika uteuzi huo, Brigedia Jenerali George Msongole ameteuliwa kuwa kamanda wa Brigedia ya Tembo kushika nafasi iliyoachwa na Brigedia Jenerali John Chacha aliyestaafu.
Mwingine ni Brigedia Jenerali Sylevesa Minja aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu akichukua nafasi ya Meja Jenerali Ezekiel Kyunga.
No comments :
Post a Comment