Unataka kufahamu CCM na Chadema walitumia shilingi ngapi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25? Utasubiri sana.
Ugumu unatokana na mchakato wa kuziandaa kuchukua mrefu, huku Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 ikizuia mwananchi wa kawaida kufahamu gharama halisi zilizotumika ama na wagombea au vyama vya siasa katika uchaguzi huo.
Mwanasheria wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Mwailolo anasema kuwa sheria hiyo inaeleza kuwa wagombea wanatakiwa kuwasilisha ripoti za matumizi yao ya uchaguzi kwa vyama vya siasa baada ya siku 60 tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ili yakaguliwe.
Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanahusika kwa pamoja kutekeleza sheria hiyo.
“Wagombea wote walioshinda na walioshindwa uchaguzi wanatakiwa kuzikabidhi ripoti zao kwa vyama vyao vya siasa na baada ya hapo vyama hivyo vitachukua siku 180 nyingine hadi kuwasilishwa kwetu,” anasema Mwailolo.
Anasema anatarajia ofisi hiyo itakabidhiwa ripoti hiyo kufikia mwishoni mwa Juni, 2016 na kuziwasilisha kwa ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ukaguzi zaidi wa hesabu kabla ya kuchukua hatua kwa watakaovunja sheria hiyo.
Waraka wa “Amri ya gharama za uchaguzi 2015” uliotolewa Agosti mwaka jana ulikitaka kila chama kutumia kiwango kisichozidi Sh17 bilioni katika kampeni zake za uchaguzi wa Rais na wabunge.
Mgombea urais asizidishe Sh6 Bilioni
Kwa wagombea wa urais, waraka huo uliokuwa umesainiwa na Waziri Mkuu wa Serikali iliyopita, Mizengo Pinda ulimtaka mgombea wa urais kutozidisha Sh6 bilioni.
Pia, uliwataka madiwani wanaogombea katika kata za mijini kutumia kiasi kisichozidi Sh8 milioni wakati wale wa vijijini kutotumia zaidi ya Sh6 milioni.
Mwailolo anasema tayari vyama hivyo vilishawasilisha kwa Msajili makadirio ya gharama za uchaguzi siku saba baada ya uteuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na sasa wanasubiri kulinganisha na matumizi halisi muda ukifika.
Hata hivyo, hakuna mwananchi aliyefahamu makadirio ambayo vyama vilipeleka kwa msajili na gharama halisi za matumizi ya uchaguzi uliopita.
Sheria inataka usiri gharama za uchaguzi
Kwa mujibu wa kifungu namba 9(4) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka jana, kinataka gharama hizo kuwa siri isipokuwa kwa matumizi ya mahakama pekee.
“Ndiyo sheria hiyo inavyosema,” anasema Mwailolo akieleza sheria inavyozuia utoaji wa taarifa za gharama halisi za mgombea au chama zilizotumika wakati wa uchaguzi kwa umma.
Anasema iwapo chama kitazidisha matumizi bila kutoa sababu zozote za msingi kitalipa faini ya kiasi kisichopungua Sh3 milioni na kupoteza sifa ya kushiriki uchaguzi na kwa mgombea atakayekiuka ni faini isiyopungua Sh2 milioni au kifungo kisichozidi mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
Hata hivyo anabainisha kuwa msajili akijiridhisha na sababu zilizotolewa na chama au mgombea kuwa aliongeza fedha kutokana na changamoto mbalimbali atamwachia lakini ikiwa vingenevyo atadakwa na sheria.
Kiwango cha faini kwa waliokutwa na makosa huenda kikawa ni kidogo kwa chama au mgombea aliyevunja sheria kwa kutumia mabilioni ya shilingi.
Mwailolo anaona kuwa adhabu ya kufungiwa ni kubwa kwa kuwa hakuna chama ambacho kitakubali kifungiwe ili kisishiriki kabisa uchaguzi ujao.
Tutatangaza matumizi yetu
Pamoja na kwamba sheria hairuhusu kutaja hadharani gharama na vyanzo vya fedha za kampeni, Chadema wamesema watatangaza vyanzo na kiwango walichotumia katika Uchaguzi Mkuu.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene anasema chama chao ndiyo chanzo cha kuanzishwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyopo hivyo hawawezi kuivunja.
“Kwa sasa tunaendelea kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wagombea sababu baadhi walioshindwa uchaguzi walikata taama, hivyo tunawahimiza wafanye hivyo na hadi sasa bado tupo ndani ya muda uliowekwa kisheria.
“Tukishamaliza hesabu zetu hatutaficha kitu. Tutawatangazia wananchi na hii haitakuwa mara ya kwanza hata mwaka 2010 tulifanya hivyo,” anasema Makene.
Itakumbukwa kuwa upitishwaji wa sheria hiyo uliibua mjadala mzito bungeni miaka mitano iliyopita kutokana na kutokuwa na uwazi wa kutosha na kuruhusu mianya mingi ya kuzidisha gharama za Uchaguzi.
Baada ya kutolewa waraka huo mwaka jana CCM kupitia msemaji wake wa kampeni, January Makamba kilisema kisingeweza kuzidisha kiwango cha Sh17 bilioni kwa sababu ni kiasi kikubwa sana cha fedha.
Maoni ya wadau
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo anasema sheria haikushirikisha wadau wengi katika uandaaji wake, haijajaribiwa ipasavyo ufanisi wake na wananchi wengi hawaifahamu kutokana na elimu ndogo iliyotolewa.
Anasema pamoja na uelewa mdogo wa wananchi bado ni busara kufahamu vyanzo vya fedha zilizotumika na vyama na wagombea wakati wa kampeni ili kubaini iwapo kuna fedha chafu zilizoingia kwa lengo baya.
“Ni muhimu kufahamu vyanzo vinamvyomuunga mkono mgombea lakini tatizo kwetu hatuna uwazi. Tumeona baadhi ya wachangiaji ni wakwepa kodi wakubwa hivyo wanaona labda kuonekana kutazua maswali kwa wananchi juu ya usafi wao,” anasema Dk Makulilo.
Anasema kuwa kwa sasa bado hawawezi kujificha kuwa itafahamika waliovunja sheria pale Msajili atakapotoa adhabu kwa chama au mgombea aliyekiuka.
“Sioni mantiki yoyote mtu akajitolea kusaidia chama au mgombea halafu ajifiche jina. Ni bora ajitaje tu ajulikane kwa sababu nchi nyingine zenye uwazi wanafanya hivyo,” anasema.
Januari mwishoni mwa wiki alieleza kuwa, kama mbunge wa Bumbuli (CCM) anaunga mkono uwazi katika uchaguzi kwa kutoa taarifa zote za fedha zinazohusiana na uchaguzi.
“Mimi nilishawasilisha gharama nilizotumia kwa chama changu ili viongozi wa juu waweze kuzihakiki. Lakini ningependa kuwe na uwazi siyo tu kutaja gharama zilizotumika bali vyanzo vya fedha hizo. Kusema zimetoka wapi ni jambo la msingi,” anasema.
Mratibu wa wapigania haki za binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa anasema, sheria ya uchaguzi ni mwendelezo wa sheria mbovu zinazosimamia uchaguzi nchini na njia bora ya kuondoa udhaifu huo ni kuleta Katiba Mpya ili kubadili mfumo mzima wa sheria kandamizi.
“Uchaguzi ni suala la wazi na matumizi yake yanabidi yawekwe wazi. Sasa inakuaje hawataki kuweka wazi gharama zilizotumika kununua magari, kukodi helikopta, kuweka mabango na mengineyo?
“Uchaguzi huu ulikuwa ni ghali katika historia ya nchi yetu lakini kwa kuwa wao ndiyo wanaotunga sheria na kufanya mabadiliko wanahisi wakifanya mabadiliko ya sheria hizo wataumbuliwa,” alisema Ole Ngurumwa. Anasema iwapo Katiba Mpya itapitishwa, mfumo wa sheria mbovu ikiwemo ya gharama za uchaguzi utaondolewa kwa asilimia zaidi ya 50 na pia hiyo itatoa fursa ya kutungwa sheria mpya.
No comments :
Post a Comment