NA RAHMA SULEIMAN
19th February 2016.

Ni ukombozi uliowafikia wauzaji na wapikaji wa ubuyu wa hapa na hasa ni wanawake, ikilinganishwa na wanaume.
Katika zama za zilizopita, biashara hiyo ilidharauliwa na mwanamke aliyefanya shughuli hiyo alionekana ‘anahangaika tu.’
Hivi sasa biashara ya ubuyu Zanzibar, imekuwa maarufu sana. Hivi sasa kuna mfanyibashara wa ubuyu anayeishi eneo la Mji Mkongwe, ambalo ni kivutio kikuu cha watalii Zanzibar.
Hivi sasa mhusika mkuu ni Asha Hemed Said, ambaye ndiye mrithi wa mradi wa Babu Issa, akibeba jukumu la wazazi waliopika ubuyu kwa kipindi kirefu tangu Asha akiwa binti mdogo.
Kimsingi, mabadiliko hayo ya mdau wa kuandaa na kuuza ubuyu wa Babu Issa, hayajaweza kupoteza ladha na umaarufu wa soko lake Zanzibar hata nje ya mipaka.
Asha anaeleza kuwa kazi hiyo amerithi kutoka kwa mama yake, ambaye sasa amepumzika kushughulika nayo.
“Tangu nimezaliwa na kuwa na fahamu yangu, nakumbuka kwetu kunauzwa ubuyu na mama yangu ndiye aliyekuwa akipika na sasa mimi nina miaka 22 na kwa sasa mimi ndio msimamizi wa biashara hii” anafafanua Asha.
“Tangu nimezaliwa na kuwa na fahamu yangu, nakumbuka kwetu kunauzwa ubuyu na mama yangu ndiye aliyekuwa akipika na sasa mimi nina miaka 22 na kwa sasa mimi ndio msimamizi wa biashara hii” anafafanua Asha.
Asha anasema ubuyu wanaopika wamekuwa wakiuza kwa jumla na rejareja na wamekuwa wakipata wateja wengi kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
SOKO LA ULAYA
Kwa mujibu wa Asha ubuyu wake unauzwa Tanzania Bara, Oman, Dubai, Marekani na Uingereza, kwani Wazanzibari wanaoishi huko huwa wanauhitaji ubuyu wake.
Pia anasema wateja wanaowategemea zaidi ni wanaonunua ubuyu kwa jumla na wanaisafirisha katika mikoani kama ya Mwanza, Dodoma, Shinyanga na Singida.
Anasema licha ya kupata ajira hiyo ambayo ni tegemeo lao katika kuendesha familia kama vile kulipa ada za ndugu zake na huduma ya chakula, amewezesha kutoa ajira kwa vijana 10.
Asha anasema waajiriwa hao, majukumu yao ni kuusafisha ubuyu, kuupika na kufunga katika plastiki maalum.
“Tuna vijana 10 hapa ambao tumewaajiri kama unavyowaona wenyewe. Hapo kila mtu akiwa na kazi yake na tunawalipa kila mwisho wa mwezi kutokana na majukumu ya kazi aliyopangiwa.
“Wapo wanaopekea Shilingi 100,000 hadi Shilingi 200,000 inategemea na kazi yenyewe,” anasema Asha, huku akisema sehemu kubwa ya watumishi hao wanatoka Tanzania Bara.
Anasifu biashara ya ubuyu inamuendea vizuri na anajivuna kibiashara kutokana na wateja kumfuata nyumbani kwao katika eneo la Hamamni, Unguja.
Pia, Asha anasema wateja walio nje ya Zanzibar, hupelekewa mzigo wanaoagiza mahali waliko kwa taratibu maalum ya ‘malipo kwanza’ yanayojumuisha gharama za usafirishaji.
“Hatuna kazi nyingine zaidi ya biashara ya ubuyu, kwani biashara hii imekuwa ni mkombozi kwetu na tumepata umarufu hapa Zanzibar na nje ya Zanzibar,” anajigamba Asha.
MWANZO NA WALIKOFIKIA
Anasema walianza kuuza ubuyu kwa bei ya awali iliyokuwa Sh. 100, miaka 20 iliyopita, mhusika mkuu akiwa mama yake na sasa bei hiyo ya mwanzo imepanda hadi Sh. 1000 kwa rejareja na jumla ni Sh. 500.
Asha anasema wamekuwa wakipata faida kubwa na kuna wanavuka malengo waliojiwekea.
Changamoto inayowakabili kwa mujibu wa Asha, ni kukosekana malighafi ya biashara ambayo ni ubuyu mbichi na kulazimika kuagiza kutoka mbali katika mikoa ya Dodoma, Singida na Mwanza.
Hivi sasa anaelekeza kilio cha soko la biashara linalotokana na changamoto yaa hali ya kisiasa inayoambatana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.
Anafafanua kuwa wateja wengi watokoa nje ya Zanzibar, wamepungua wakihofu hali ya kisiasa inayoendelea.
“Wateja wetu wamekuwa na hofu. Wanasema nchi bado haijatulia hivyo wanaogopa kuja kununua ubuyu na kisha kufanya biashara.
“Kwa sasa wateja wetu ni wale wanaonunuwa kwa rejereja na mtu ananunua kwa kula au kupeleka zawadi,” anasema Asha.
MATARAJIO
Anasema matarajio makubwa walio nayo ni kuiboresha biashara zaidi kwa kuwa vifaa vya kisasa vya utengenezaji ubuyu, unaowafanya wasitumie nguvu katika kuuanndaa.
Mwanamke huyo anatumia fursa hiyo kuwaasa kinamama wenzake na hasa vijana wasio na ajira, kujishughulisha na biashara ndogondogo zitakazowapa ajira na hatimaye kujikomboa kiuchumi.
Anasema dhana ya utegemezi wa kiuchumi kupitia kuolewa, hivi sasa umepitwa na wakati.
WATEJA WA UBUYU
Mary Mwita ni mteja wa jumla wa ubuyu wa Babu Issa, ambaye anausafirisha hadi katika masoko ya mikoa ya Tanga, Arusha, Shinyanga na Singida. Pia ana soko ndani ya Unguja.
Anakiri kuwa biashara ya ubuyu ina faida kubwa iwapo kutakuwepo wateja wengi wa kuaminika.
“Mimi nanunua ubuyu wa kwa Babu Issa, ndoo moja ndogo Shilingi 15,000, mimi nauza Shilingi 35,000, napata Shilingi 20,000. Si haba! Nikidunduliza hizo fedha maisha yananiendea kuliko kukaa bila ya kufanya kazi,” anatamka Mary anayeishi eneo la Mombasa, Unguja.
Anasema watu wengi wana hulka ya kudharau biashara ndogo kama vile kuuza ubuyu, huku kukiwepo mifano ya wafanyabiashara wakubwa walioanza na hatia ya biashara ndogo, wakafanikiwa.
Mary anausifu ubuyu wa Babu Issa kuwa ‘mzuri’ na unakubalika sokoni. Anaongeza: “Nikienda Dar es Salaam nikiwaambia nauza ubuyu, basi utawasikia ‘ubuyu wa Kwa Babu Issa wa Zanzibar?’ Nikiwaambia ‘ndio wenyewe’ huwa napata wateja kibao.”
Anataja changamoto ya biashara yake ni baadhi ya wafanyabiashara wa ubuyu, kupotosha wateja kwamba ubuyu wanaouuza ni wa Babu Issa, ilhali siyo kweli.
Mary anasema upotoshaji huo umesababisha baadhi ya wateja kuwa na shaka na hudai hadi wajiridhisdhe kwa kuonja ndio wanakuwa tayari kununua.
“Kama mpenzi wa ubuyu, basi ubuyu wa Kwa Babu Issa haufichiki na haubadiliki. Ladha yake na ubora wake ukiula tu utajua, kwa maana mzuri kweli kweli, sio kama nawafagilia” anasema Mary.
Pia anataja changamoto nyingine ni kikwazo cha aina kodi wanachokabliana nacho bandarini wakati wa kusafirisha ubuyu nje ya Zanzibari, jambo analodai linawaathiri sana kibiashara.
“Kwa kweli mimi nachoshwa hasa! Hata ubuyu ukisafirisha wanataka ulipie kodi bandarini,” analalamika Mary.
Pamoja na changamoto hizo, Mary anapa kusonga mbele kibiashara na mahsusi uuzaji ubuyu wa Babu Issa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment