Toleo la 446

Walisisimkwa na kuwa chemchemi ya furaha na buraha kiasi cha kuonekana kama waliingiwa na wazimu.
Utafikiri walizugwa, walikuwa hawaoni wala hawasikii ila kwa Abdel Nasser.
Nasser alikuwa kipenzi cha umma. Alikuwa kiongozi ambaye watu wa nchi nyingine za Kiafrika na za Kiarabu wakitamani angekuwa kiongozi wao.
Si ajabu kwa kiongozi aliyekuwa akipendwa hivyo kujisahau.Badala ya kuona anapendwa akadhani anaabudiwa.
Siku umati wa Damascus ulipokuwa ukimshangilia Nasser, mtu mmoja aliyekuwa naye alimyemelea na akamnong’oneza kwa kumwambia: “Umati huu umejawa na furaha kwa vile upo hapa, lakini wakati wote lazima ukumbuke kuwa wewe ni binadamu tu.”
Aliyempa Gamal Abdel Nasser wasia huo alikuwa Mohamed Hassanein Heikal, aliyefariki dunia Cairo Jumatano iliyopita akiwa na umri wa miaka 93. Tafsiri ya “Heikal”, jina lake la ukoo, ni hekalu.Heikal alikuwa msiri wa Nasser na gwiji wa mengi.
Alikuwa mwandishi, mhariri, mwanasiasa, mwanahistoria na shuhuda wa historia. Aliwahi pia kuwa waziri wa habari wa Nasser na wa Rais Anwar Sadat. Ni mtu aliyeshuhudia mengi; aliiona historia ikitokea na aliiandika ilipokuwa ikitokea.
Ameandika vitabu vipatavyo 40 kwa Kiarabu na Kiingereza. Mwishoni mwa maisha yake kumbukumbu nzima ya Misri alikuwa nayo yeye; au yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa kumbukumbu hiyo.
Heikal alibahatika kujuwana na waliokuwa wakizicheza siasa za dunia. Wakimheshimu kiasi cha kumkaribisha sebuleni na ofisini mwao kuzijadili.
Aliyokuwa akiyachota huko ndiyo aliyokuwa akitudokolea katika makala yake yaliyokuwa yakichapishwa kwenye gazeti la Al Ahram, alilokuwa mhariri wake mkuu tangu 1957 hadi 1974. Hili ni gazeti lililoasisiwa mwaka 1875 na linamilikiwa hadi leo na serikali ya Misri.
Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Cairo, Heikal alianza kazi 1943 akiwa ripota wa gazeti la Kiingereza la Egyptian Gazette.
Baadaye alikuwa mhariri wa magazeti mbalimbali ya Kiarabu kabla ya kuwa mhariri mkuu wa Al Ahram. Huko ndiko alipojipatia umaarufu mkubwa kwa makala aliyokuwa akiyaandika kuhusu matukio aliyokuwa akikumbana nayo.
Tafsiri pamoja na tafsili zake za matukio hayo zilikuwa za hali ya juu kama zilivyokuwa chambuzi zake za kisiasa. Mwenyewe siku zote akisema kwamba alikuwa mwandishi wa habari tu.
Ni kweli lakini duniani kuna waandishi na waandishi. Wote si sawa. Hawa wa kaumu ya pili ni waliobobea katika tasnia ya uandishi wa habari. Heikal alikuwa katika kundi hili.
Hili ni kundi la waandishi waliopevuka, wenye kuhusudiwa, kuigwa na kuheshimiwa na waandishi wenzao. Hawa ni “waandishi wa waandishi”.
Waandishi hawa ni waandishi waliobobea kwa namna wanavyoicharaza na kuichezea lugha au kwa namna wanavyoichukuwa na kuisarifu dhana, tukio au jambo la kawaida na kulifanya liwe la ajabu au la maajabu.Wakati wote msomaji hachoki, anaona utamu anapoyasoma makala.
Wengine huwa na uwezo wa kuichukua dhana ngumu na kuielezea kwa njia laini na lugha nyepesi hata mtoto wa skuli akaweza kuifahamu. Na akaona raha anapoifahamu.
Heikal alikuwa na sifa nyingine. Alikuwa shujaa na mtu wa msimamo.Siku zote aliitumia kalamu yake kuitetea au kuiendeleza misimamo yake.
Kwake uandishi haukuwa kazi tu, lakini ulikuwa chombo cha kutumiwa kwa madhumuni adhimu zaidi ya kutetea haki na kupigania utu. Kwa ufupi, kupigania misimamo yake.
Wanasiasa wa itikadi tofauti wakimuenzi na kuna waliokuwa wakimchukia. Mwanasiasa wa mwanzo aliyemvuta akawa upande wake alikuwa Nasser.
Inasemekana kwamba alikuwa Heikal aliyemuandikia Nasser kile kitabu chake maarufu Falsafat Thawra (Falsafa ya Mapinduzi) na ni yeye pia aliyemsaidia Nasser kuvitumia vyombo vya habari kujijenga kwa umma.
Mashariki ya Kati nzima Nasser akisifika kuwa kiongozi pekee wa wananchi wa kawaida na mtetezi mkuu wa uzalendo wa Kiarabu.
Wakati huohuo, Nasser alikuwa akiutukuza uzalendo wa Kiafrika na alikuwa katika safu ya mbele pamoja na akina Kwame Nkrumah wa Ghana, Ahmed Ben Bella wa Algeria, Modibo Keita wa Mali na Ahmed Sekou Touré wa Guinea katika mapambano dhidi ya ukoloni barani Afrika. Aliifanya Misri ijitolee kwa hali na mali kusaidia ukombozi wa Afrika.
Wakati wote Heikal alisimama naye Nasser bega kwa bega. Wapinzani wao wanasema Nasser akimtumia Heikal.
Wapinzani hao hupenda kukumbusha jinsi Heikal alipopata changamoto kubwa ya propaganda zake wakati Misri ilipoingia vitani na Israel Julai 1967.
Aliliachia Al Ahram lichapishe taarifa lilizopata kutoka jeshini. Tena zilichapishwa kwenye ukurasa wa mbele bila ya kuhakikisha kwamba zilikuwa za kweli.
Kwa hivyo, palichapishwa kichwa cha habari kilichosema: “Ndege 130 za adui za aina ya jet zimeangushwa” asubuhi.
Baadaye ndipo Heikal alipotanabahi kwamba hakukuwa hata ndege moja ya kijeshi ya Israel iliyotunguliwa.Yaliyotokea ni kwamba Israel ilikuwa imeziangamiza ndege zote za jeshi la angani la Misri, ilivitwanga viwanja vyote vya ndege vya Misri, ililiteka eneo la Sinai Peninsula lenye ukubwa mara tatu zaidi ya eneo zima la Palestina na iliudhibiti Mfereji wa Suez.
Juu ya hayo mpaka kufa Heikal akimtetea Nasser.
Masahibu hao walikutana mwanzo vitani 1948 pale magaidi wa Kiyahudi walipowashinda Waarabu na kuunda taifa la Israel. Heikal aliwahi kueleza kwamba walipokutana kwa mara ya kwanza alistaajabu kumuona Nasser kuwa ni kijana.
Akitarajia atakuwa na umri mkubwa zaidi. Nasser alimwambia Heikal, “nimekuwa nikiyasoma makala yako.” Siku hizo nafikiri Heikal alikuwa mwandishi wa gazeti la Rose el Yusuf.
Usuhuba wao ulianza hasa mwaka 1951, siku Nasser alipokwenda ofisini kwa Heikal kuazima kitabu alichoandika kuhusu Iran. Wakati huo takriban wapinzani wakuu wote wa Mfalme Farouq wakiwasiliana naye. Miongoni mwao walikuwa vijana wa kijeshi waliokuwa wakipanga kumpindua Farouq.
Vijana hao waliokuwa wakiongozwa na kina Gamal Abdel Nasser hawakumshirikisha Heikal katika harakati zao lakini Heikal alipata fununu dakika za mwisho za mpango wa mapinduzi.
Kuna siku Heikal alimkuta Nasser nyumbani kwa jenerali mmoja wa jeshi. Heikal alimgeukia Nasser akamwambia kwamba mwaka 1948 jeshi la Misri lilishindwa kuilinda heshima yake. “Na hivi sasa hata halina tena hiyo heshima,” alilalamika Heikal.
“Unashauri tufanye nini?Unataka jeshi lipindue?”” Nasser alimuuliza.
Siku tatu baadaye, Julai 22, 1952, kina Nasser wakampindua Farouq.
“Heshima” ni kitu ambacho Heikal akikienzi sana.
Alikuwa na heshima katika maingiliano yake na watu na pia katika uandishi wake. Ingawa alikuwa na usuhuba mkubwa na Nasser hata hivyo alijiwekea mipaka. Hakujiachia akubali kuandika kila alichokuwa akiambiwa na Nasser.
Aliofanya kazi nao Heikal wanamsifu kwamba akiwasikiliza kwa heshima watu aliokuwa akiwapigia simu kutafuta habari au waliompigia yeye simu kumpasha habari lakini wakati wa kuandika makala yake alikuwa akiandika yale aliyotaka yeye kuyaandika.
Sahafu yake katika Al Ahram, iliyompatia umaarufu, ilikuwa ikichapishwa kila Ijumaa na ikiitwa “Besaraha” (Kusema kweli). Ikichapishwa pia na magazeti kama ya Akhbar El Yom, Akher Sa’a na magazeti mingineyo ya Kiarabu.
Isitoshe, ikisomwa kwenye Radio Cairo na halafu ikitafsiriwa kwa Kiingereza na kile kitengo cha Shirika la Habari la BBC cha Monitoring Service kilicho Karen, Kusini Magharibi mwa Nairobi.
Kazi ya kitengo hicho ni kuyanasa matangazo ya redio ya lugha mbalimbali za Afrika na kuyatafsiri. Kwa muda mrefu sasa huduma yake imekuwa ikiwasaidia waandishi, hasa walio nje ya Afrika, wanaofuatilizia matukio ya bara la Afrika na Mashariki ya Kati.
Kwa hivyo, pamoja na wasomaji wake wa kawaida nchini Misri, makala ya Heikal yakisomwa pia na waandishi wenzake, wa Misri na nje ya nchi hiyo, mabalozi na waliokuwa wakihusika na sera za Mashariki ya Kati katika wizara za nchi za Ulaya na Marekani. Walikuwa lazima waisome sahafu hiyo kwa sababu ikitoa mwanga wa siasa za Gamal Abdel Nasser na muelekeo wa siasa katika Mashariki ya Kati.
Sisi wengine tukionja ladha ya maandishi yake.Alikuwa akizieleza siasa za ndani jikoni zilipokuwa zikipikwa. Nani kasema nini, kamwambia nani nini na katika mazingira gani.
Uandishi wake haukuwa mkavu na, kwa hivyo, haukuwa chapwa. Aliutia viungo ukachipukia. Ulikuwa uandishi wa kuzichambua siasa lakini kwa mtindo wa fasihi.
Hadi leo ninayakumbuka bado makala aliyoyaandika akieleza mauti yalipomkuta Gamal Abdel Nasser Septemba 1970.
Saa chache baada ya kumalizika mkutano mkuu wa viongozi wa Umoja wa Kiarabu na akiwa amekwishawasindikiza wageni wake, Nasser alipata mshtuko wa moyo akakimbizwa kwake alikofariki dunia.
Heikal alieleza jinsi Mfalme Hussein wa Jordan na Yasser Arafat, kiongozi wa Wapalestina, walivyolia kama watoto wadogo. Mua’mmar Qadhafi hakuweza kujizuia; alizimia mara mbili.
Kadhalika, nakumbuka makala aliyokuwa akiyaandika Heikal baada ya Qadhafi kumpindua Mfalme Idris wa Libya mnamo mwaka 1969.
Baada ya kufariki Nasser, Heikal kwanza akishirikiana na Sadat lakini kwa sababu ya tofauti zilizoibuka baadaye baina yao Heikal akabidi ajiuzulu uhariri wa Al Ahram.
Sadat alipopatana na Israel, Heikal naye alizidi kumshambulia kwingine. Mwishowe mwaka 1981, Sadat akamfunga Heikal gerezani pamoja na wapinzani wengine.
Mahusiano ya Heikal na marais wengine waliofuatia — Hosni Mubarak, Mohamed Morsi na Abdel Fattah al Sisi — yalikuwa vivyo hivyo: kwanza wakipatana halafu wakikorofishana.
Akimdharau hasa Mubarak, ambaye kinyume na Nasser na Sadat, alikuwa hasomi vitabu. Akihisi kwamba Mubarak alichelewa kuzivaa siasa na hakuwa na ujuzi uliohitajika wa kuongoza taifa.
Nje ya Misri katika miezi ya karibuni, Heikal aliiudhi Saudi Arabia aliposema kuwa hatua yake ya kuingilia kijeshi Yemen ni “upuuzi wa kisiasa”.
Heikal alikuwa hapendezi katika nchi nyingine za Ghuba kwa vile amekuwa na msimamo tofauti na wao kuhusu Syria na hakukubaliana nao kuwa Iran ni zimwi la Mashariki ya Kati.
Heikal alikuwa na ari na akiwataka waandishi wake nao pia wawe na ari katika uandishi wao.
No comments :
Post a Comment