
Kwa nini? Inaelezwa kuwa, mmea huo unaotumiwa katika namna ya kutafuna (kama vile bazoka) umekuwa ukitumiwa kwa kipindi kirefu cha maisha ya mwanadamu, ikiwa na kemikali zinazolevya akili ya mtumiaji.
Hiyo ni kumfanya awe anazubaa muda mwingi, hachangamki na anakosa hamu ya kula chakula, sifa ambazo dawa za kulevya inazo.
Ingawaje, WHO inasema haijafikia kiwango cha dawa za kulevya kama vile heroine na cocaine, mirungi bado ina athari hizo hizo za dawa za kulevya, ikielekeza akili katika upungufu wa uwezo wake.
Pia inaelezwa kuwa ‘mlevi’ wa mirungi anapoacha ghafla, hupata athari mbalimbali za kiafya na kisaikolojia, kama vile kujihisi mwili haujatulia, kukosa hamu ya kula na raha. Hivyo ni jambo linalohitaji tiba inayofanana na ile ya mwathirika wa dawa za kulevya.
Wadau wakuu ‘walioshika bango’ kuhakikisha mirungi inaingizwa katika orodha ya dawa za kulevya, ni Taasisi ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani, ikiungwa mkono na wadau wa kimataifa, nchi kama vile Ujerumani, Uingereza na Marekani.
Licha ya kuingizwa katika orodha hiyo ya WHO, kunanchi kama vile Djibouti, Kenya, Ethiopia, Somalia na Yemen bado inaruhusiwa na hivyo kilimo chake ni kikubwa nchini humo.
Katika eneo la pembe ya Afrika kama vile Ethiopia na Somalia, mirungi inazalishwa kwa wingi, huku katika ukanda huo na Afrika Mashariki jamii ya Kisomali ikisifika kuwa watumiaji wakuu.
Mmea huo shambani unakua hadi kimo cha mita 10 na husitawi katika mazingira tofauti ya hali ya hewa, kuanzia mazingira ya nyuzi joto kati ya setigredi tano hadi 35.
Kadri muda unavyoenda, ndivyo kilimo hicho kinavyozidi kukua katika sehemu tofauti duniani. Leo hii imekuwa maarufu katika maeneo kama vile Afrika Kusini, Msumbiji na Swaziland.
Katika baadhi ya nchi za Ulaya, zao hili kabla ya kupigwa marufuku, ilikuwa ikizalishwa kwa wingi.
Nchini Yemen, zao hilo ni maarufu na ina hadhi kubwa katika kuchangia uchumi wake na mwananchi mmoja mmoja.
Asilimia 40 ya maji yanayozalishwa nchini humo kwa matumizi ya umma, inaelekezwa katika umwagiliaji na wastani wa kati ya asilimia 10 na 15 ya uzalishaji wake unaongezeka kila mwaka.
Wataalam wa maji wanaeleza kuwa, matumizi makubwa ya maji katika kuwagilia mirungi inapunguza akiba iliyoko ardhini katika jimbo la Sanaa nchini Yemen.
Serikali ya nchi hiyo sasa iko katika kampeni ya kuwashauri wananchi wake wahamie kwingineko, ikiwemo katika pwani ya Bahari Nyekundu, ili kunusuru upungufu wa maji utokanao na matumizi makubwa yaliyopo.
Inaelezwa kuwa, kati ya mwaka 1970 na 2000, eneo ambalo mirungi uliopandwa ni wastani wa hekta 8,000 walipoanza hadi upeo wa hekta 103,000.
Mirungi katika jamii inayoitumia, wanaichukulia kuwa kitu cha starehe na burudani, hata katika baadhi ya hafla za kijamii hutumika kama sehemu ya viburudisho.
Watu wanaofanya shughuli za kuchosha mwili kama vile madereva na wanafunzi wa vyuo, nao hutumia mirungi kama nyenzo ya kupunguza uchovu mwilini na ‘kuweka upya akili’ zao katika nafasi kama vile ya kahawa.
Mmea wa mirungi hutoa maua na mbegu ambazo zikichumwa na majani yake ndiyo hutumika. Ukuaji wa shina lenyewe, kuanzia kupandwa hadi kukomaa, huchukua kati ya miaka saba na nane.
Utunzaji wake katika kulinganisha na kilimo cha mazao mengine, inaelezwa kuwa usimamizi wake ni rahisi zaidi.
Majani yake huvunwa mara nne kwa mwaka na ili isitawi vyema, inapaswa kumwagiliwa maji mengi katika kipindi kifupi kabla ya mavuno. Hapo ndipo mazao bora hupatikana.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment