
Baada ya Rais, John Magufuli, kumaliza siku 100 Februari 12, mwaka huu tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana, baadhi ya wadau wameonyesha shauku ya kujua dira na hatima ya Tanzania katika uchumi na utekelezaji wa ahadi zake alizotoa.
Katika hali hiyo, mambo 12 yamejitokeza zaidi kama vitu vitakavyotumika kupima hatima ya siku 1,825 (miaka mitano) ambazo kiongozi huyo atakaa Ikulu kwa awamu ya kwanza ya miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kufanyika uchaguzi mwingine. Kwa sasa Rais Magufuli amebakisha siku 1,719 kukaa madarakani kwa awamu ya kwanza baada ya kumaliza siku 106 za awali tangu aapishwe.
Itakumbukwa kwamba, kwa siku 100 alizokaa Ikulu, mbali na kufanikiwa kuanza na ahadi yake ya elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne na kupunguza safari za nje, serikali yake tayari imesimamisha zaidi ya watumishi wa umma 100 kutoka sekta mbalimbali kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi, wameeleza kuna mambo ambayo walitarajia kuwa angeyatolea uamuzi mapema, lakini bado halijaonekena hivyo.
KASHFA YA ESCROW
Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na utekelezaji wa maazimio nane ya Bunge la 10, juu ya kashfa ya Tegeta Escrow inayotajwa kuwa ni moja ya mambo yaliyopelekea serikali ya CCM kutumia nguvu nyingi kupata ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 tofauti na miaka ya nyuma.
Itakumbukwa kuwa, kashfa ya Tegeta Escrow iliyosababisha kutafunwa kwa takribani Sh. bilioni 300, mbali na kung’oa baadhi ya mawaziri na mwanasheria mkuu wa serikali, baadhi ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge mpaka leo hakuna kilichofanyika.
Azimio la saba la Bunge lilisema kwa kuwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha kuwa, Tanesco imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya shirika hilo, serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa shirika la umeme nchini kwa lengo la kuokoa fedha.
Agizo hilo lililotolewa mwishoni mwa mwaka 2014 lakini mpaka leo halijatekelezwa na inadaiwa kuwa, kila mwezi Tanesco inailipa IPTL Sh. bilioni nane, izalishe ama isizalishe umeme.
Hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyowasilisha ripoti yake Bunge la 10 juu ya Escrow, alisema: “Mapato ya nchi makubwa kuliko ya utumbuaji majipu yanaendelea kupotea. Mkataba wa IPTL bado unaendelea kunyonya nchi na serikali inatazama Sh. bilioni nane zinalipwa IPTL na PAP kila mwezi. Katika siku 100 tangu Rais Magufuli aingie madarakani, jumla ya Sh. bilioni 30 zimeshalipwa kwa IPTL/PAP.”
BENKI YA STANBIC
Mbali na IPTL, Benki ya Stanbic Tanzania ilitajwa kwenye maazimio hayo kutokana na kupitisha mabilioni ya fedha na kuyatoa kwa kinyume cha sheria.
Kutokana na hali hiyo, Bunge lilitaka benki hiyo itangazwe kuwa ni chombo cha kusafisha fedha haramu, lakini mpaka leo hakuna hatua iliyochukuliwa.
Wakati hilo halijatulia, hivi karibuni pia benki hiyo ilihusishwa kwenye kashfa ya Sh. trilioni 1.3, ambazo Serikali ya Tanzania iliomba mkopo Benki ya Standard ya Uingereza kupitia benki hiyo ya Stanbic Tanzania.
Kwenye mkopo huo, Benki ya Stanbic iliongeza riba ya asilimia moja (Sh. bilioni 12) kinyume cha makubaliano na kuingia kwenye kampuni ya EGMA na kisha zikatolewa kwa njia ileile iliyotumika kutoa za Escrow.
KATIBA MPYA
Katiba Mpya ni jambo jingine ambalo linatarajia kuwa kipimo cha kiongozi huyo na kikubwa kinachoangaliwa ni kama je, ataendelea na Katiba pendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalim la Katiba, Oktoba 2, mwaka juzi, chini ya Mwenyekiti wake, Samuel Sitta na Makamu, Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais, ama ataurudisha mchakato nyuma kama ambavyo wadau wengine wanataka.
Itakumbukwa kuwa, katiba hiyo inayopendekezwa ambayo ilikabidhiwa kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Oktoba 8, mwaka jana ili mchakato wa kura za maoni uendelee, umetumiaa Sh. bilioni 101.
Fedha hizo ni Sh. bilioni 27 zilizotumika kulipa wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, Sh. bilioni 8.2 zilizotumika kurekebisha ukumbi wa Bunge ili kuongeza idadi ya viti vitakavyochukua wajumbe wote na Sh. bilioni 66 zilizotumiwa na Tume ya ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiiongozwa na Jaji Joseph Warioba kukusanya maoni ya wananchi.
BANDARI YA BAGAMOYO
Kiporo kingine cha serikali ya awamu ya nne, ambacho kinatarajiwa kuwa kipindo cha serikali ya Rais Magufuli ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unaokadiriwa kutumia Sh. bilioni 10.
Fedha hizo ni mkopo kutoka China ambao umepingwa na baadhi ya watu, wakisema kama upanuzi wa Bandari ya Mombasa, nchini Kenya na ujenzi wa reli mpya itakayounganisha Rwanda, Uganda na Kenya, tayari imeiweka Bandari ya Dar es Salaam katika hatari ya kupoteza soko la nchi hizo ni kitu kisichoingia akilini kujenga Bandari ya Bagamoyo.
Wanasema tayari Zambia nayo inaboresha miundombinu yake ili ipitishie bidhaa zake katika Bandari za Beira (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini) na Walvis Bay (Namibia), hivyo inakuwa ni masihara kujenga Bandari ya Bagamoyo.
Wanasema kuliko kujenga bandari mpya ya Bagamoyo, ni vema serikali ikafikiria kuitanua Bandari ya Dar es Salaam na ya Tanga na kuimarisha reli zinazotoka kwenye bandari hizo.
Serikali ya Rais Magufuli bado haijaonyesha kama itaendelea na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo au itaelekeza fedha hizo kwenye eneo jingine ambalo tija yake itaonekana kwa haraka zaidi.
BOMBA LA GESI
Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam, ni kati ya miradi mikubwa ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya rushwa kama ambavyo baadhi ya wabunge wamewahi kusema.
Mradi huo umetumia dola za Marekani bilioni 1.22, kati ya fedha hizo, Benki ya Exim ya China imechangia asilimia 95 na Serikali ya Tanzania asilimia tano.
Zitto wakati akiwa Mwenyekiti wa PAC, aliibua utata wa Sh. bilioni 821 ambazo Serikali ya Tanzania imelieleza Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwamba imezitumia katika mradi wa ujenzi wa bomba hilo.
Mbali na hofu ya kuzidishwa kwa fedha zilizotarajiwa kutumiwa kwenye mradi huo, bado inadaiwa kuwa utendaji kazi wa mitambo ya gesi inayozalisha umeme siyo ya kuridhisha.
DARAJA LA KIGAMBONI
Mradi mwingine wenye utata wa fedha ni ujenzi wa Darasa la Kigamboni, Dar es Salaam, lililogharimu takribani Sh. bilioni 248.
Imeelezwa kuwa, fedha hizo ni nyingi kuliko uhalisia, ingawa mpaka sasa hakuna aliyethibitisha tuhuma hizo.
Wengi wanatumaini kuwa, serikali ya Rais Magufuli iliyojipambanua kuwa inapiga vita rushwa, itashughulikia suala hilo na ukweli kuwekwa hadharani.
RELI YA KATI
Ujenzi wa Reli ya kati unaotarajiwa kugharimu kati ya Sh. trilioni saba hadi tisa, ni jambo jingine linaloiweka serikali ya Magufuli mtegoni.
Wabunge wanaotoka maeneo inakopita reli hiyo tayari wameunda umoja wao wenye lengo la kushinikiza ujenzi wake kwa kiwango cha kisasa, wakisema itasaidia wananchi wa maeneo hayo kukuza uchumi wa nchi na kuokoa barabara zinazoharibika kwa kubeba mizigo mikubwa ambayo ingetakiwa ipite kwenye reli.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alionyesha ugumu wa suala hilo alipolieza Bunge kuwa fedha zinazohitajika ni nyingi na haziwezi kurudi kwa upesi.
MAHAKAMA YA MAFISADI
Eneo hilo ni moja ya ajenda zilizobebwa na Magufuli wakati wa kampeni zake, lakini mpaka sasa hakuna kitu kilichofanyika licha ya wananchi kutarajia kuona mwanga mapema.
Hata hivyo, siku zilizobaki za uongozi wake bado ni nyingi hivyo wapo wanaotarajia kuona ndoto hiyo ikitokea.
UJENZI WA VIWANDA
Wakosoaji wengi wa serikali hii, wanasema mpaka sasa bado nchi inaendeshwa kwa matamko na kwamba hakuna dira iliyoonekana dhahiri.
Kutokana na hali hiyo, wanasema ingetakiwa mwanga wa Tanzania ya viwanda uwe umeonekana, lakini mpaka sasa Rais bado hajaweka bayana ni viwanda gani anataka na viwe chini ya nani na kwa namna gani.
UMEME
Tatizo la kukosekana kwa umeme wa uhakika ni changamoto nyingine kubwa inayoikabili serikali ya Rais Magufuli.
Katiba hutoba yake ya kulifungua Bunge la 11, Rais Magufuli alsema tatizo hilo ni moja ya mambo yaliyolalamikiwa na wananchi wengi, hivyo serikali yake inakabiliwa na kazi nzito ya kuboresha sekta hiyo.
UCHUMI
Kwa siku 100 za mwanzo, bado suala la uchumi halijaeleweka, kwani thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuporomoka.
Hali hiyo imeendelea licha ya kuambiwa kwamba, makusanyo ya kodi kwa mwezi yameongezeka kwa takribani Sh. bilioni 400.
Pia hali ya uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja bado imeendelea kuwa changamoto.
Dira ya maendeleo itakayowekwa wazi, ndiyo itakayofanya Watanzania wawe na kitu cha kusema baada ya miaka mitano.
DIRA
Baadhi ya wadau wa siasa wamezungumzia suala hili, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Mwesiga Baregu, alisema lazima ifike mahali wananchi wajue dira na mwelekeo wa Rais ambavyo itaonyesha amejipangaje na kumsaidia namna ya kusonga mbele, kwani hawezi kuleta mabadiliko peke yake bila Watanzania wote.
“Hadi sasa dira na mwelekeo wake haujafahamika ili tuweze kumsaidia. Kuna vitu amefanya kushtua nchi, ila Watanzania wapewe mwelekeo wa wazi kusudi wote tujue tunaeleka wapi, nafasi, mchango na wajibu wetu kama Watanzania ndiyo siasa na utawala bora,” alisema.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Charles Kayoka, alisema serikali ingalie mambo ambayo inaweza kufanya kuboresha hali ya maisha, uchumi ikiwamo kuimarisha shilingi ili kipato wanachopata watumishi kitoshe.
“Kama tukiwabana sana wakashidwa kujipatia mahitaji kwa kipato halali, mfano anayepokea Sh. milioni moja au mbili, ikifika wiki ya kwanza ya mshahara imekwisha hata ajibane vipi, morali ya kazi itapungua, pia waweke motisha kwa mtendaji aliyeokoa fedha za nchi ili kusiwe na nidhamu ya woga,” alisema.
Alisema wakati wanafikiria kutumbua majipu waangalie namna ya kuweka vitu vya kuwapunguzia makali ya maisha watumishi kama kuwapa chakula cha mchana na usafiri.
Dk. Kayoka alisema siyo kila siku kusikia habari za kufukuzwa pekee, bali kuwe na uboreshaji wa ofisi kwa kuweka vifaa muhimu kama komputa, barua pepe, samani ili kuboresha utendaji kazi ndipo watumishi waweze kulaumiwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment