
Maalim Seif Sharif Hamad.
Dar es Salaam. Tishio la Chama cha Wananchi (CUF) kutoshiriki uchaguzi wa marudio, limezidi kuiweka Zanzibar njiapanda kutokana na vizingiti vya kikatiba vinavyoongoza uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
SUK iliundwa kwa lengo la kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar ambao umekuwa ukiibuka kila wakati wa Uchaguzi Mkuu kuanzia mwaka 1995. Ilianza kutekelezwa mwaka 2010 baada ya Uchaguzi Mkuu, lakini uwezekano wa kuendelea sasa ni mdogo kutokana na hali ya kisiasa visiwani humo.
Kwa miezi mitatu sasa Zanzibar imeendelea kuwa kwenye mtanziko baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani wa Oktoba 25 na baadaye kutangaza uchaguzi mpya utakaofanyika Machi 20, ambao CUF imeugomea.
Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo la 2010, Ibara ya 39 (3), Rais, baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais, atateua Makamu wa Kwanza wa Rais.
Ibara hiyo inafafanua kwamba “endapo chama kilichotokea nafasi ya pili hakikufikisha asilimia 10 ya kura zote za Rais, au endapo Rais atakuwa hana mpinzani, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itapewa chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
Kwa mazingira ya kisiasa ya Zanzibar, mbali ya CCM na CUF, hakuna chama kingine kilichowahi kufikisha asilimia 10 ya kura za Rais tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992, wala hakuna kilichopata viti vya uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi, hali inayoelezwa na wachambuzi wa duru za kisiasa kwamba haitakuwa rahisi kupata chama mbadala katika SUK.
Endapo hali itatokea hivyo, Katiba ya Zanzibar Ibara ya 39 A (1) inasema kuwa “Rais atakayechaguliwa (bila sifa ya kutoa makamu wa kwanza), atalazimika kuteua Makamu wa Pili wa Rais na kuiacha wazi nafasi ya Makamu wa Kwanza”.
Vivyo hivyo, Katiba hiyo inaongeza kifungu cha 39 A (2) kuwa “Rais atateua mawaziri na kuacha wazi nafasi za uteuzi wa chama au vyama vya upinzani”.
Kwa mantiki hiyo, mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif amesema msimamo huo wa CUF unaweza kuathiri uteuzi wa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na uwezekano mdogo wa vyama nje ya CUF na CCM kupata sifa ya kuunda SUK.
“Hata kama Katiba inamruhusu Rais kuteua chama kinachofuata kwa kura, lakini ni mgombea gani, alikuwa Hamad Rashid wa ADC lakini na yeye kwa sasa amefukuzwa na chama chake,” alisema.
“Lakini pia, Pemba pekee uchaguzi ukirudiwa ni asilimia 10 tu ya wapigakura watakaoshiriki kwa mujibu wa taarifa za matokeo ya awali. Sasa hii itakuwa vigumu kuongoza hilo eneo bila ushirikiano wa CUF.”
Naye Jaji Amir Manento, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), alisema iwapo upinzani hautakuwa na uwezo wa kupata uwakilishi hata wa jimbo moja kwenye Baraza la Wawakilishi, basi hakuna chama cha upinzani kitakachoshiriki kuunda SUK.
Hata hivyo, Jaji Manento alisema kwa sasa kinachotakiwa ni kusubiri kuona kitakachojitokeza baada ya uchaguzi huo.
“Kwa hiyo, Serikali itakuwa na sura ya chama kimoja, ila sina hakika itakuwaje katika utekelezaji wa SUK,” alisema Jaji Manento
“Siwezi kusimamia upande wowote kwa jambo hilo. Tusubiri tuone mtoto atakayezaliwa kama ni wa kike au kiume na ataishije katika mazingira ya Zanzibar,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema bila ya CUF kushiriki uchaguzi, kunaweza kutokea mgawanyiko mkubwa wa Wazanzibari kwa kuwa chama hicho kina idadi kubwa ya wafuasi.
Profesa Mlama alisema hana uhakika kama vyama vingine vichanga vitakuwa na uwezo wa kuunda SUK kutokana na kutowahi kupata uwakilishi wa majimbo tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi.
Alisema kinachotakiwa kabla ya kufikia uchaguzi huo, juhudi ziwe zimefanyika kushawishi pande hizo mbili ili kufikia maridhiano kwa maslahi ya Wazanzibari.
“Lakini tatizo walikuwa wanazungumza kwenye mikutano yao bila kutwambia walikuwa wanasema nini huko. Ilibakia siri tu kwa hiyo wananchi tunabaki njia panda,” alisema.
Profesa Sherrif pia alizungumzia mustakabali wa Zanzibar iwapo ZEC itaendelea na uchaguzi bila ya kuwapo maridhiano, akisema itakuwa vigumu kwa Serikali kupata misaada.
Hivi karibuni, mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) walieleza kusikitishwa na kitendo cha ZEC kuitisha uchaguzi huo wakati mazungumzo ya kutatua mgogoro yakiendelea na kummtaka Rais John Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kumaliza mvutano huo.
“Kwa hivyo endapo CUF haitashiriki, basi (wahisani) wanaweza kuweka msimamo wa pamoja kwa kupuuzwa maoni yao, hii inaweza kuathiri hata upande wa Bara,” alisema Sherrif.
Akizungumzia suala hilo, makamu mwenyekiti wa zamani wa CUF, Juma Duni Haji alisema SUK ni utashi wa kikatiba unaotokana na maridhiano na hivyo si mgombea urais wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, wala wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein atakayeweza kuongoza Zanzibar bila ya serikali hiyo.
Lakini alisema vikao hivyo vya maridhiano havikuweza kuzaa muafaka baada ya kushindwa kuafikiana kwenye hoja 10 kati ya 11 zilizowasilishwa na Maalim Seif.
katika vikao hivyo, vilivyokuwa chini ya Dk Shein, ni hoja moja tu ya kudumisha amani iliyokubaliwa na pande zote.
Duni alidokeza baadhi ya hoja hizo kuwa ni uhalali wa Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi.
Pia walizungumzia suala la kura kuibwa Pemba, lakini upande uliodai kuwa kura ziliibwa ulishindwa kutoa ushahidi. Vilevile ilijadiliwa hoja ya uchaguzi majimbo ya Pemba kuvurugika, lakini hakukuwa na mgombea aliyelalamika.
Alisema kama kuna majimbo ambayo uchaguzi ulivurugika basi busara ilikuwa ni kufuta uchaguzi wa majimbo husika na kuurudia baadaye.
Pia alisema suala la Maalim Seif kujitangaza mshindi, lilijadiliwa lakini hawakueleza sababu za kutomshtaki mahakamani.
Lengo lao kuu la kurudia uchaguzi ni Tanganyika kuiogopa sera ya CUF ya kuibadilisha Zanzibar. Wao wanataka Zanzibar iwe kama vile Mafia ni eneo lao na waje wafanye kila kufru yao hapa. Pamoja na kuwaibia Wazanzibari raslimali zao, pia na kuwafanya wale wasio na asili madhubuti ya Zanzibar (wakuja)wawe ndio viongozi
ReplyDelete