Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, February 9, 2016

MAONI YA MHARIRI: Rais aiokoe Zanzibar, si kuingilia uchaguzi



Yamekuwapo maombi ya kumtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aingilie kati mgogoro wa kisiasa Zanzibar ili kuvinusuru visiwa hivyo visiingie katika machafuko ya kisiasa. Wito huo una dhamira njema tofauti na ambavyo imekuwa ikitafsiriwa kuwa anatakiwa aingilie uchaguzi. Wito huo unamtaka awe msuluhishi wa mgogoro huo uliotokana na kuvurugika kwa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.
Uchaguzi wa marudio umepangwa kufanyika Machi 20, lakini tayari wadau wameshasema hautakuwa suluhisho la mgogoro wa kisiasa Zanzibar bali utachangia kuzorotesha hali iliyopo sasa. CUF na wengine wamekuwa wakisisitiza kufanyike mazungumzo ili kuinusuru Zanzibar.
Lakini kuna watu waliojitokeza ambao wanasema Rais hawezi kuingilia uchaguzi wa Zanzibar kwa sababu za kisheria.
Hivi karibuni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema Rais hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar, ukiwamo uchaguzi wa marudio na akasisitiza kuwa “Katiba ya Zanzibar si ya Muungano, masuala ya ulinzi na usalama ndiyo ya Muungano na ndiyo sababu ulinzi umeimarishwa visiwani humo kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama”.
Pia mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu kuwa Rais hawezi kuingilia uchaguzi wa Zanzibar kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Maoni ya wanasheria hao wawili ni sahihi kisheria, lakini kwa muktadha wa wito huo, wadau hawataki Rais aingilie kati uchaguzi, bali atumie ushawishi wake kukutana na pande zinazohusika kutafuta suluhu ili kama uchaguzi utarudiwa au hautarudiwa, amani na maelewano vitawale.
Kitendo cha CUF kumtaka Rais kuingilia kati kinaonyesha kuwa ipo dhamira njema ya kutaka kumaliza mgogoro huo kwa amani.
Na kwa kuwa pande zote mbili kuu katika mgogoro huo (CCM na CUF) zina imani na Rais Magufuli, hiyo ni fursa mwanana kwa kiongozi huyo wa nchi kuziweka mezani kujadili jinsi ya kuondoa tofauti hizo kwa maslahi ya Wazanzibari na Taifa kwa ujumla.
Magufuli ni Rais wa Tanzania na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania. Kusema kuwa mgogoro wa Zanzibar haumuhusu Rais Magufuli ni makosa makubwa kiutawala. Rais ana wajibu wa kuhakikisha nchi inaendeshwa bila ya migogoro inayoashiria kuvunjika kwa umoja wa kitaifa.
Kwa maana hiyo, wito huo unamtaka kuweka mbele amani, utulivu na mshikamano wa Taifa kwa kuzungumza na pande zinazosigana kuzizuia kuelekea kwenye hali mbaya zaidi, na si kubatilisha au kuhalalisha uchaguzi wala matokeo yake. Tunadhani huu ni wakati muafaka kwa Rais kufanya mazungumzo kabla ya huo uchaguzi wa marudio na maridhiano hayo ndiyo yaamue mustakabali wa nchi kwa kuwa hata mamlaka ya ZEC yanatoka kwa wananchi.
Tunamshauri Rais aonyeshe uongozi, akijua kuwa “zumari likipigwa Zanzibar, Bara wanacheza”. Kama Zanzibar kuna sintofahamu ya kisiasa, ni wazi kuwa Tanzania Bara haitabaki salama.
Wapenda amani wamepaza sauti, wanataka kilio cha Wazanzibari kisikilizwe, na hawamaanishi kuwa Rais Magufuli avunje Katiba, bali asaidie kutafuta suluhisho la mgogoro unaotokana na uchaguzi. Tunadhani hilo ni jukumu lake la msingi.
Ikiwa kila mtu mwenye nadhari anatahadharisha hatari itakayotokea Zanzibar kama uchaguzi wa marudio utafanyika bila kuwapo maridhiano ya kisiasa, kuna haja pia kwa Rais kuungana na wito huo na kuchukua hatua kuinusuru Zanzibar.     

No comments :

Post a Comment