
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva
Morogoro. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uligubikwa na changamoto nyingi ikiwamo lugha za matusi na maandishi kwenye picha za wagombea.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume ya uchaguzi, Jaji mstaafu Merrystella Longway kwa niaba ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva katika mkutano na tathimini kati ya tume na asasi za kiraia kuhusu elimu ya mpigakura.
Jaji Longway alizitaka asasi za kiraia kuendelea kushirikiana na tume kutoa elimu ya mpigakura kwa wananchi.
Alisema NEC imefanya tathimini ya uchaguzi ili kubaini changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kuzifanyia kazi huku akisema wanathamini kazi kubwa iliyofanywa na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpigakura.
Alisema changamoto zilizojitokeza ni uelewa mdogo kuhusu alama sahihi inayohitajika wakati wa upigaji kura.
Alisema kabla ya uchaguzi tume ilitoa elimu kwa asasi za kiraia ili kufikisha elimu hiyo kwa wananchi na kuwahamasisha kujiandikisha kwenye Daftari la Mpigakura.
Alisema katika mchakato huo asasi 451 zilijitokeza kuomba kutoa elimu ya mpigakura, kati ya hizo, 447 ndizo zilizokubaliwa kutoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamishna wa Tume ya Uchaguzi, Asina Omary aliwasilisha mada katika mkutano huo akisema asasi za kiraia ni wadau wakubwa katika mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia kwamba NEC haiwezi kuwafikia Watanzania wote.
Pia, aliitaka NEC kutoa elimu kwa Watanzania ili kukuza demokrasia nchini na kuelimisha wananchi juu ya haki na wajibu wao katika michakato ya chaguzi.
Mtu mwenye ulemavu, Fatma Djaa Cheza alisema upigajikura kwa Zanzibar uliendeshwa kwa usiri huku watu wa kundi hilo wakipewa kipaumbele.
No comments :
Post a Comment