Toleo la 445
17 Feb 2016
ALHAMISI wiki hii, wananchi wa Uganda watafikia kilele cha Uchaguzi Mkuu nchini humo.
Watachagua Rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa, watakaoliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki katika kipindi kingine cha miaka mitano.
Uchaguzi huo ni wa tatu tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo, mwaka 2005.
Rais Yoweri Museveni, aliyeongoza taifa hilo kwa miaka 30 sasa, anawania kuongoza kwa muhula wa tano, akikabiliana na wagombea wengine saba katika uchaguzi ambao Waganda milioni 15 wanatarajiwa kupiga kura.
Uchaguzi huo una umuhimu wa pekee kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Uganda ikiwa moja ya nchi waasisi wa jumuiya hiyo ina jukumu la kuhakikisha uchaguzi nchini humo unafikia tamati kwa amani, kwa manufaa ya raia wa Uganda na wakazi wote wa Afrika Mashariki kwa ujumla, kwa kuwa hali tete katika taifa moja mwananchama wa EAC inaweza kuathiri nchi nyingine jirani. Tayari Afrika Mashariki inauguza majereha yaliyotokana na uchaguzi wa nchini Burundi ambapo mpaka sasa, Tanzania inahifadhi wakimbizi zaidi ya 120 kutoka taifa hilo mwanachama wa Afrika Mashariki, huku hali ikiwa bado tete nchini humo.
Amani kwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni muhimu kwa ustawi wa shughuli za kijamii na kiuchumi katika ukanda huu, machafuko katika mojawapo ya nchi hizi hayataziacha nchi zingine wanachama salama. Kwa hiyo wakati nchi za jumuiya hii pamoja na Umoja wa Afrika (AU) zikifanya juhudi za kuweka hali ya mambo shwari nchini Burundi, ni vyema Waganda wakahakikisha kuwa wanakamilisha mchakato wa uchaguzi katika hali ya usalama, wakithibitisha kwamba wao ni kielelezo halisi cha demokrasia.
Aidha, vitendo vya ukiukwaji wa demokrasia na haki za binadamu vinavyoelezwa kuendelea kutokea nchini humo kuelekea siku ya uchaguzi vinapaswa kukomeshwa ili wananchi wa taifa hilo wakatimize haki yao ya kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wao.
Ndiyo maana, wakati tunawatakia Uganda uchaguzi wa mwema, tunawaomba wafanye uchaguzi wao kwa kudumisha amani na umoja wa taifa hilo.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tunawatakia-waganda-uchaguzi-mwema#sthash.XOyskNgx.dpuf
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tunawatakia-waganda-uchaguzi-mwema#sthash.XOyskNgx.dpuf
No comments :
Post a Comment