Rais John Magufuli, akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete wakati wa Maadhimisho ya Miaka 39 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida, Februari 6, mwaka huu. Picha ya Maktaba.
Kukielewa Chama cha Mapinduzi (CCM) cha sasa, ni muhimu kuipitia historia ya vyama asili vilivyozaa chama hicho kilichotawala muda mrefu zaidi katika Bara la Afrika.
Vyama husika vilivyoungana ni Tanganyika African National Union (Tanu) cha Tanganyika na Afro Shiraz Party, (ASP) cha Zanzibar, vyote vikiwa ni vya ukombozi.
Ilikuwa ni Tanu iliyoasisiwa mwaka 1954 iliyoongoza Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961 huku ASP iliyozaliwa 1957 ikaongoza Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, ambayo hata hivyo yanatazamwa tofauti na Wazanzibar kutokana na matabaka.
Historia tofauti ya vyama vilivyozaa CCM vimeendelea kuifanya CCM Bara na visiwani kuwa tofauti kabisa, kama mapacha wasiofanana.
Tanu ilipata uungwaji mkono na wananchi karibu wote wa Tanganyika wakati wa uhuru.
Kule Zanzibar, ASP kilikuwa ni chama cha tabaka moja kati ya matabaka mawii yenye ufuasi karibu nusu nusu, tabaka la waliojiita Waafrika na la weusi.
Ni tabaka hilo la Waafrika, wenye ASP yao, ndiyo wanaoyaona mapinduzi kama harakati muhimu za kuenziwa, zilizowakomboa Waafrika wanyonge dhidi ya dhuluma kutoka kwa Waarabu.
Lipo tabaka jingine lililochukia mapinduzi na kuyaona kama dhuluma, uonevu uliopanda mbegu ya ubaguzi kati ya wananchi wa Zanzibar. Hawa walikuwa wapinzani wakati ule (ZNP) na ni wapinzani sasa (CUF).
Kutokana na historia mbili tofauti, CCM Zanzibar inajaribu kwenda sambamba na CCM ya Bara, ikijaribu kushinda kwa urahisi kama wenzao wa bara katika chaguzi za kidemokrasia ndani ya mfumo wa vyama vingi. Matokeo ya jitihada hizo ni kubakwa kwa demokrasia visiwani humo mara nyingi CCM ikilazimisha ushindi.
Sura mbalimbali za CCM
Tofauti hii ya CCM Bara na Zanzibar ni kielelezo cha mnyumbuliko kutokana na nyakati na mahali unaokifanya chama hiki kuchukua sura mbalimbali tangu kuzaliwa kwake mwaka 1977.
Kwa mfano, katika muktadha wa Afrika, CCM ni kielekezo cha Muungano wa mfano ambao Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akishawishi na kuutaka kuuona.
Nyerere alipenda Muungano wa taratibu kuanzia katika kanda mbalimbali za Bara hili kabla ya kufikia muungano wa Afrika nzima.
Kwa hiyo, CCM kama chombo cha itikadi ni mfano wa utekelezaji wa falsafa hiyo ambayo ilipingana na ile Kwame Nkrumah na wengine waliotaka Afrika iungane yote, mara moja na kuunda nchi moja.
CCM na ukombozi wa Afrika
Sura nyingine ya CCM ni chama cha ukombozi wa bara la Afrika. Chini ya Tanu na baadaye CCM, Tanzania ilikuwa ni ngome na kambi kubwa ya harakati za ukombozi wa nchi zilizokuwa zikitawaliwa na wakoloni barani Afrika. Nyerere aliamini kuwa uhuru wa Tanzania hauna maana kama ndugu zetu wengine wa Afrika walikuwa wakiendelea kunyanyaswa na kutawaliwa.
Chini ya muongozo wa itikadi wa Tanu/CCM, jukumu la Tanzania lilikuwa kubwa kiasi kwamba makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi za Kiafrika (OAU) ilikuwa hapa nchini ambako kazi kubwa ilifanyika kuzinasua nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini, Msumbiji na Namibia kutoka katika makucha ya wakoloni.
Ikisimama katika siasa za kutofungamana na upande wowote katika mnyukano wa vita baridi kati ya nchi za Magharibi za Kibepari na Mashariki za Kijamaa, Tanu/ CCM ilihakikisha uhusiano wake na mataifa makubwa kama Marekani au China hauathiri harakati za ukombozi zilizofikia tamati mwaka 1994 pale Afrika Kusini ilipopata uhuru wake kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa makaburu.
Ujamaa uliofeli
Sura nyingine ya CCM ni chama cha kijamaa ambapo mwaka 1976, Tanu ilitangaza Azimio la Arusha lililolenga kujenga nchi ya kijamaa kwa misingi ya usawa na uhuru na haki mbalimbali ikiwamo ya kuabudu na kutoa maoni, haki ya kupewa ujira wa haki, kupinga matabaka na unyonyaji, umiliki wa pamoja wa rasilimali za nchi na ukombozi wa bara la Afrika.
Azimio la Arusha lilitaja kuwa fedha siyo msingi wa maendeleo na kuweka malengo ya kujitegemea kwa imani kuwa misaada ingeweza kuhatarisha uhuru wetu.
Katika utekelezaji, njia kuu za uchumi zilibinafsishwa na kisha kuundwa vijiji vya ujamaa huku baadhi ya watu wakihamishwa kwa nguvu kwenda kujiunga.
Miongoni mwa maadili ya viongozi ilikuwa ni pamoja na kila kiongozi kuwa mkulima au mfanyakazi, asiwe na hisa katika kampuni yoyote au kuwa mkurugenzi wa kampuni binafsi, asipokee zaidi ya mishahara miwili, asimiliki nyumba ya kukodisha wengine.
Hatimaye, baada ya jitihada kubwa ya utekelezaji wa sera za ujamaa, sera hizo zilishindwa kwa sababu mbalimbali za nje na ndani. CCM ikalazimika kubadili mwelekeo wa kisera kutoka ujamaa hadi ubepari.
Mnamo mwaka 1991 chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, CCM ikaachana rasmi na ujamaa katika Azimio la Zanzibar lililopindua maadili ya uongozi yaliyowekwa katika Azimio la Arusha. Huu ulikuwa ndiyo msumari wa mwisho katika jeneza la ndoto ya kujenga ujamaa.
CCM ya matajiri
Ukiyasoma vema marekebisho ya Azimio la Arusha yaliyofanywa kule Zanzibar mwaka 1991, utagundua kuwa kimsingi chama hicho kilikoma kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi pekee na badala yake kukaribisha wafanyabiashara na matajiri.
Halikuwa jambo baya ukizingata zama zilishabadilika, lakini udhaifu wa usimamizi wa maadili ya chama ukaifanya CCM kuwa chama cha matajiri pekee huku wakulima na wafanyakazi wakitumiwa. Katika miaka ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa na baadaye Rais Jakaya Kikwete na mpaka sasa, CCM imehangaika na zimwi la rushwa ndani ya chama huku ikidhihirika kuwa matajiri walikuwa wakiiteka kwa kununua uongozi.
Ilikuwa ni baada ya kugundua kuwa umaarufu wa chama unazidi kudidimia, Rais Kikwete alianzisha mchakato mwaka 2010 wa mageuzi yaliyobatizwa jina la kujivua gamba. Ni katika harakati hizo za mabadiliko ndio mwaka 2012 timu mpya ya viongozi ilipochaguliwa wakiwamo Philip Mangula kama Makamu Mwenyekiti CCM Bara na Abdulrahman Kinana kama Katibu Mkuu.
Uongozi wa mpya wa chama ulirejesha kidogo imani ya wananchi katika chama kwa kufanya ziara mikoani ya kuimarisha chama hicho huku wakikosoa Serikali hadharani hadi chama kikaaminika kuliko Serikali yake.
Kwa maoni yangu uongozi wa wakina Mangula na Kinana haukuendana na Serikali ya Kikwete ambayo ilionekana kuchoka na kuishiwa pumzi, ikiandamwa na kashfa za rushwa na ufisadi kila kona na ndiyo maana haikuwa ajabu CCM kupata tabu kushawishi wananchi kuichagua katika uchaguzi wa mwaka jana.
Kwa wafuatialiaji wa mambo wanaweza kukubaliana nami kuwa huenda ni ujasiri wa viongozi hawa Mangula, Kinana na timu yao ndiyo waliowezesha kukatwa kwa majina ya wagombea urais ndani ya CCM walioonekana kuwa na nguvu, lakini wakiwa na madoa ya kimaadili.
Bahati nzuri pia, busara za wazee ziliwezesha kukibakiza chama kikiwa na umoja, pale tishio la mgawanyiko lilipotokea.
Zanzibar kesi maalumu
Kama nilivyoanza kusema awali katika ufunguzi, CCM Zanzibar ni tofauti na bara, ina maadili na misimamo yake inayoongozwa na historia za matabaka za visiwa hivyo. Kwa sababu hiyo, CCM Zanzibar inakabiliwa na changamoto tofauti.
Ni historia hii ya matabaka ndiyo iliyompelekea kiongozi mmoja kushauri vyama uipinzani, hususan CUF, wasiruhusiwe kugombea urais Zanzibar, bali wagombee nafasi za chini. Na ni historia hii ya matabaka ndiyo iliyowaamsha wafuasi wa CCM kubeba bango la lugha ya kibaguzi mbele ya viongozi wao katika sherehe za mwaka huu za Mapinduzi.
CCM Zanzibar inazidi kupata upinzani kutoka kwa CUF na huenda hali hiyo ikawa mbaya zaidi. Kwa sababu wafauasi wa CUF wanazidi kuongezeka kuliko wa CCM, inaonekana huko mbele CCM itahitaji kutumia nguvu nyingi kushinda uchaguzi.
maoni@mwananchi.co.tz
No comments :
Post a Comment