dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, February 4, 2016

Wabunge CCM: Tutaibana Serikali

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola akichangia mjadala wa mapendekezo ya mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na mwongozo wa kuaandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016 / 2017, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Dodoma. Wabunge wa CCM wamesema hawatakuwa na kigugumizi katika kuibana Serikali ili itekeleze ahadi zake kwa wananchi na tayari hali hiyo imejionyesha katika wiki ya kwanza ya Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi na Moja.
Jumanne, wabunge wanaotoka kwenye mikoa ambayo Reli ya Kati inapita, waliunda umoja wao kwa ajili ya kushinikiza ujenzi wa reli hiyo, wakisema bila ya Serikali kusikiliza kilio chao, watahamasisha wenzake ili wasusie bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Wabunge walioongea na Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita walidokeza mkakati wao wa kutoinyamazia Serikali inapokosea, wakisema hawawezi kukwepa jukumu lao la kuisimamia Serikali.
Wabunge hao walipewa rungu hilo na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana wakati wa semina ya kuwanoa iliyofanyika Januari 19 kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa Bunge mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kwenye semina hiyo Kinana aliwataka kuhakikisha wanazungumza masuala yenye masilahi kwa Taifa na kuibana Serikali pale inapoonekana inalegalega katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu, Kinana alifanya ziara nchi nzima, akiahidi kuwapa meno wabunge wa CCM ili waibane Serikali, huku akiponda mawaziri walioonekana kutowajibika ipasavyo.
Suala la ujenzi wa reli hiyo lilianza tangu wiki iliyopita wakati Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema atashawishi wabunge wenzake kuigomea bajeti iwapo Serikali haitatoa mwelekeo wa ujenzi wa miundombinu hiyo ya usafiri.
Mapema wiki hii, wabunge wao waliungana na wapinzani kuunda umoja wao ulio chini ya uenyekiti wa Ezekiel Maige, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Msalala kwa tiketi ya CCM, akisaidiana na Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, ambaye anakuwa katibu.
Wakizungumza na gazeti hili, wabunge hao wa CCM walisema wataufanyia kazi wito wa Kinana na hawatakuwa na kigugumizi.
“Nimedhamiria kwa moyo wote kuwatumikia wananchi hivyo sitakuwa na kigugumizi,” alisema Mary Mwanjelwa, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mbeya na Mwenyekiti wa Bunge.
“Kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, itakuwa kweli kwa kuwa nitakosoa bila woga na kupongeza inapostahili.”
Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso alisema nguvu hiyo ilikuwapo siku nyingi, lakini tatizo lilikuwa hofu.
“Kitendo cha Kinana kutoa njia kwa wabunge wake kuikosoa Serikali hadharani, ni cha kiungwana,” alisema.
“Kwa lugha nyingine chama chetu kimetupa meno ya kung’ata pale tunapoona Serikali inakwenda kinyume hivyo mawaziri wajiandae,” alisema Kakoso.
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani alisema ni vizuri mwongozo huo sasa upo, ingawa alisema wakati mwingine ulikuwa ukitumiwa vibaya.
Ngonyani alisema kuna wabunge walikuwa wanaacha wajibu wao na kufanya kazi ya kupongeza hata mahali ambapo hapakustahili, lakini kwa kauli ya Kinana lazima watabadilika.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Mbunge wa Urambo Mashariki, Margaret Sitta naye alisema atazungumza kile anachokiamini.
“Siwezi kuficha kitu,” alisema. “Pale penye ukweli nitausema. Siku zote huwa napenda kuzungumza kile ninachokiamini.”
Katika mjadala unaoendelea wa hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa Novemba 20, 2015, wabunge wamekuwa wakiikosoa Serikali na kueleza wazi jinsi wananchi wanavyopata tabu kwa kukosa maji, huduma bora za afya, elimu, barabara, reli, bandari, usafiri wa anga na kuhoji lini kero katika maeneo hayo zitamalizika.

Mawaziri wajibu
 Wakijibu hoja hizo baadhi ya mawaziri walisema wamejipanga kuendana na kasi ya wabunge na hakuna mtu atakayekubali kuaibika mbele ya umma wa Watanzania.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema hana wasiwasi kuhusu kibano cha wabunge kwa maelezo kuwa maelezo yote ya utendaji wa kazi wameshapewa na Rais John Magufuli.
Alisema kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo inayosababisha wao kuwa kifua mbele kwa kuwa hakuna jambo lililoahidiwa ambalo litashindikana.
“Naamini kabisa mle ndani wabunge watakuwa wakali na hii itakuwa kutoka hata kwa wapinzani, lakini pia tukubaliane kuwa tunafuata sheria na kanuni na kazi kubwa tulisharahisishiwa na Rais. Kazi yetu ni kufuata njia tu,” alisema Masauni.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo alisema kitendo cha CCM kuwaruhusu wabunge wake kuibana Serikali yao ni kizuri na hivyo mawaziri na manaibu wanatakiwa kuendana na kasi hiyo.
“Uelewa wa wabunge wa sasa ni mkubwa na huwezi kuwadanganya,” alisema.
“Sina wasiwasi kwa kuwa wabunge watakuwa wakiyasemea matatizo ya Watanzania ambayo hata mimi angependa yatatuliwe na ndiyo dhamira yake. Siwezi kumkimbia mbunge wa CCM.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki alisema Serikali imejipanga vyema na hakuna jambo litakalokuwa na shida.
“Mimi siyo msemaji katika jambo hilo, lakini nataka mtambue kuwa kama Serikali tumejipanga kuwa na majibu yasiyokuwa na maswali na hakuna shida kuhusu wabunge wote kuibana Serikali,” alisema Kairuki.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim analiona suala hilo kuwa gumu kwa sababu litaiweka rehani CCM.
“Mfano nzuri ni sakata la (uchotwaji fedha kwenye akaunti ya) escrow, wabunge wa CCM watajadili kwa juu juu siyo kiundani kwa sababu linawagusa baadhi ya watu waliopo katika chama chao,” alisema Salim.
Alisema jambo jingine kuna baadhi ya hoja zinawagusa moja kwa moja watu wanaodaiwa kukifadhili chama hicho, hivyo hawatakubali kuijadili ili kulinda masilahi ya CCM na Serikali kwa ujumla.
“Nguvu ya upinzani ni kubwa sasa tofauti na Bunge lilopita. Kwa hiyo ni vigumu kwa wabunge CCM kuunga mkono kwani wakifanya hivyo watakiweka chama chao mahali pabaya na hilo hawataki litokee,” alisema Salim.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi,ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Richard Mbunda alisema suala hilo linawezekana kwa kuwa kazi ya mbunge ni kuisimamia Serikali, pia kuikosoa na kuipongeza pale inapofanya vizuri.
Alisema ni wakati mwafaka kwa wabunge wa CCM kujitofautisha na kujiweka pembeni badala ya kuisemea na kuitetea Serikali.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Habel Chidawali na Bakari Kiango.     

No comments :

Post a Comment