Wajumbe hao, Ayoub Bakari Hamad na Khamis Mohammed, walikutana na waandishi wa habari jijini Dar e Salaam na na kueleza kuwa, haungi mkono tangazo la Jecha kuitisha uchaguzi wa marudio kwani ni batili kwa kuwa madiwani na wawakilishi walishatangazwa na kupewa vyeti vya ushindi kutokana na uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
“Januari 21, mwaka huu, tume ilifanya kikao kujadili uchaguzi wa marudio, baadhi ya wajumbe walitaja Machi 20, kuwa tarehe ya marudio. Baadhi walipinga kwa kueleza kuwa ufutaji wa uchaguzi wa awali ulikuwa batili kikatiba na kisheria, hivyo kuitisha uchaguzi mwingine pia itakuwa ni batili,” walisema makamishna hao.
Hata hivyo, wajumbe hao wamependekeza kuwapo kwa mpatanishi wa kimataifa ambaye atazikutanisha pande mbili zinazotofautiana, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) katika meza moja ili kufikia suluhu itakayoridhiwa na pande zote.Walidai katika kuonyesha Mwenyekiti wa ZEC alikuwa anashinikizo la CCM, katika kikao chao cha Oktoba 27, mwaka jana, malalamiko yao yaliwasilishwa lakini aliyatupa.
Walidai Novemba Mosi, mwaka jana, walikaa kikao kingine ambacho ajenda yake ilikuwa ni kuunga mkono tamko la Mwenyekiti la kufuta matokeo ya uchaguzi alilolitoa Oktoba 28, mwaka jana na kwamba kabla ya kikao hicho Jecha aliwaomba radhi na kuwataka kumuunga mkono kwa kuwa amefanya hivyo baada ya kushawishiwa na vyombo vya juu lakini wajumbe waligawanyika na alipiga kura ya kuamua mwenyewe.
Walisema hawaungi mkono uchaguzi wa marudio kwa kuwa Katiba ya Zanzibar haitoi nafasi kwa Mwenyekiti peke yake kufanya uamuzi kwa jina la tume.
Walitaja sababu nyingine kuwa ni, kwa mujibu wa Katiba uchaguzi wa uwakilishi na udiwani ulishakamilika kwa washindi kupewa vyeti na hakuna chombo chochote kinachoweza kubatilisha uchaguzi huo isipokuwa Mahakama Kuu baada ya kusikiliza shauri husika lililopelekwa na wenye mamlaka ya kupeleka wametajwa kisheria na siyo mwenyekiti wa tume.
Wajumbe hao walisema kurudia uchaguzi huo ni kuiweka nchi katika majaribu kwani kuna uwezekano mkubwa wa kutokea fujo.
“Wakati Rais Dk. John Magufuli, anachukua hatua nzito za kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, tuna amini kuwa nchi yenye uchumi mdogo kama Zanzibar kutumia fedha za umma zaidi ya Sh. bilioni saba kwa kufanya uchaguzi uliokwishafanyika ni matumizi mabaya kuwahi kutokea.
Kutokana na utashi wa kisiasa ndani ya tume imepelekea utaratibu wa manunuzi kufanywa kwa kutumia hali ya dharura na hivyo kuondoa uwazi na uwajibikaji,” walifafanua.
Aidha, walihoji kwanini uchaguzi urudiwe kwenye upigaji kura pekee bila kufuata hatua zote muhimu na kwamba huo ni uminyaji demokrasia na iwapo utafanyika viongozi watakaochaguliwa watakuwa batili.
“Tume imeingiliwa mno na kufanya maamuzi yake kisiasa ikiwamo kurudia uchaguzi, ni lazima ieleweke tume inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu,” walisema.
Aidha, walitoa wito kwa wajumbe wenzao kuachana na uchaguzi huo kwa kuwa hauna maslahi kwa nchi badala yake ni historia mbaya.
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuelezea madai ya wajumbe hao, Jecha simu yake ya mkononi iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na alipotafutwa Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Alli, naye simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa ZEC, Khamis Issa, alisema hajui lolote kuhusiana na suala hilo na kutaka aulizwe Jecha.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment