
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeanzisha utaratibu wa kuwapa mkono wa heri wanachama wake wanaostaafu, utaratibu ulioanza Julai Mosi, mwaka jana, imefahamika.
Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa watakaopewa mkono wa kwaheri ni waliochangia chama hicho kwa zaidi ya miaka 15.
Alisema katika kipindi cha kati ya Julai Mosi na Desemba, mwaka jana, Sh. milioni 265 zilitumika kutoa mkono huo kwa wastaafu 781 na kwamba mwaka huu zimetengwa Sh. bilioni 1.4 kwa ajili ya kuwaaga wastaafu 4,200.
Aliongeza kuwa kwa kuanzia, wastaafu hao kila mmoja atapewa mabati 20 ya geji 30 yenye urefu wa futi 10.
Oluoch ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CWT, alisema utaratibu huo umetolewa kutokana na kikao kilichofanyika Januari, mwaka jana, na kwamba wanachama waliostaafu kuanzia Julai Mosi, ambao wana sifa ndio watakaonufaika.Alisema mkono huo wa kwaheri unaweza ukaboreshwa zaidi baadaye na kwamba badala ya kuwapatia mabati, inawezekana chama kikatoa pikipiki au hata gari kulingana na uwezo.
“Huo ni uamuzi wa kikao hicho kwa hiyo mwanachama aliyestaafu kabla ya tarehe hiyo mfano Juni 31, 2015, hataagwa hivyo watabaki kuwa wanachama kwa mujibu wa katiba,”alisema.
Alisema chama hicho ambacho ni cha wafanyakazi walimu na si mfuko wa hifadhi ya jamii kulingana na katiba yake, hivyo kitaendelea kuwatetea walimu wote waliostaafu na walioko kazini.
Miongoni mwa haki hizo ni kuhakisha wanapata mishahara stahiki, viinua mgongo na matibabu.
Mwaka 2009, chama hicho kilikusanya Sh. bilioni 1.2 kutokana na kodi ya pango ya kitega uchumi cha Mwalimu House. Kutokana na mapato hayo, kila chama cha kuweka na kukopa cha walimu (Saccos) kutoka kila mkoa, kilipatiwa Sh. milioni 40.
Walimu wanachukua mikopo kwenye Saccos hizo na kurudisha asilimia 50 fedha zote za mkopo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment