Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, amefariki dunia, baada ya kuugua ghafla.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, alisema jana kuwa Sarah alifariki dunia juzi saa moja jioni, katika Hospitali ya Wilaya ya Njombe ya Kibena, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.
Alisema mkuu huyo wa wilaya aliugua ghafla juzi muda mfupi baada ya kutoka ofisini na alianza kujisikia vibaya alipokuwa akijiandaa kula chakula alichokuwa ameandaliwa.
“Mkuu wa wilaya alipofika nyumbani kwake, alitaka kupata chakula lakini alianza kupata shida ya kupumua na baadaye kuanza kulegea mwili. Alipelekwa katika Hospitali ya Kibena ndipo umauti ukamfika akipatiwa matibabu,” alisema Dk. Nchimbi
Dk. Nchimbi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Wanging’ombe ya Ilembula, ambayo ndiyo ina uwezo wa kuhifadhi maiti.Alisema mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na kwamba leo kutakuwa na ibada maalum ya kuaga mwili wake katika Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini mjini hapa, alikokuwa akiabudu.
Mkuu wa Mkoa alisema baada ya hapo, mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Dar es Salaam, ambako familia yake inaishi maeneo ya Kigamboni, kwa maziko.
Sarah alianza kazi ya ukuu wa wilaya mwaka 2006 katika wilaya ya Kilindi mkoani Tangana baadaye kuhamia Njombe (wakati huo ikiwa katika mkoa wa Iringa) na sasa mkoa wa Njombe, alikotumika hadi kufariki dunia.
Kabla ya kuwa mkuu wa wilaya, alikuwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) sasa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
MAGUFULI ATUMA SALAMU
Katika hatua nyingine, Rais Dk. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, kutokana na kifo cha ghafla cha mkuu huyo wa wilaya.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli alielezea kushtushwa na kifo cha ghafla cha Sarah Dumba, ambaye alisema alimfahamu kwa uchapakazi wake, uaminifu na uadilifu katika utumishi wa umma na uongozi.
"Nimeshtushwa sana na kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba. Kwa mara nyingine, taifa limempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika," alisema kama alivyonukuliwa katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.
Dk. Magufuli alibainisha kuwa Sarah Dumba atakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhimiza maendeleo ya wananchi, hususan katika kilimo na ufugaji, nidhamu ya utumishi serikalini na kuwatetea wananchi wa hali ya chini, wakati wotealipokuwa mkuu wa wilaya.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli alisema anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo, katika kipindi hiki kigumu na pia amewataka wote kuwa na subira na uvumilivu.
TAMWA YAMLILIA
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha mwanachama wake ambaye alikuwa mwanahabari mahiri na mkongwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga, alisema chama hicho kinaungana na familia ya marehemu, serikali, wanahabari na Watanzania wote katika kuombeleza kifo hicho na kwamba ameacha pengo kubwa kwenye tasnia ya habari, hasa wanawake na taifa kwa ujumla.
Sarah Dumba amewahi kuwa mtangazaji wa RTD na wakati fulani aliteuliwa kuwa mwakilishi wa chombo hicho mkoa wa Morogoro kuanzia mwaka 1998 hadi 2006 alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya.
Kitaaluma, Sarah Dumba alisomea mafunzo ya utangazaji Cairo, Misri na baadaye alijiunga na Chuo cha Diplomasia, Kurasini jijini Dar es Salaam.
SOURCE: NIPASHE
No comments :
Post a Comment