Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Jecha ambaye kuingia na kutoka kwake uwanjani hapo hakukutangazwa kama ilivyokuwa kwa viongozi wa kitaifa, aliwavutia wanachama hao baada ya kuteremka kutoka jukwaa kuu na kuelekea sehemu iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya kumuapishia Dk. Shein.
Mwenyekiti huyo kwa sasa amekuwa kivutio kwa wananchi wengi hususan wanachama wa CCM baada ya kufuta uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Jecha ambaye alikuwa amevalia vazi la kanzu, alionekana mpole wakati akishuka jukwaani na alipofika chini, ndipo wananchi hao walipoanza kumshangilia.Kiongozi huyo tangu alipotangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo mwaka jana kwa madai kwamba ulitawaliwa na kasoro nyingi, amekuwa haonekani hadharani.
Uwanja wa Amani jana ulifunguliwa saa 1:00 asubuhi na wananchi mjini hapa walifika kwa wingi huku wakiwa wamevalia sare za CCM.
Vyombo vya ulinzi viliimarisha ulinzi na kona zote za uwanja zililindwa na askari Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Vikosi vya Maalum vya Zanzibar.
Aidha, katika sherehe hizo wananchi mbalimbali wakiwamo askari, walizimia kutokana na kusimama muda mrefu pamoja na kukaa juani.
Watoa huduma ya kwanza walionekana wakikimbia huku na kule kwa ajili ya kuwabeba wananchi waliokuwa wamezimia ili kuwapa huduma ya kwanza.
Licha ya kuwapo jua kali, lakini wananchi walikaa kwa utulivu hadi mwisho wa sherehe.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment