Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, March 27, 2016

JK azidi kupasua anga Ulaya


Wakati Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiendelea kusafiri kwenda mataifa mbalimbali kwa shughuli za kikazi na kufikisha nchi 10 alizokwisha tembelea, Rais John Magufuli leo ametimiza siku ya 143 tangu aapishwe kuingia Ikulu bila kukwea ndege kwenda ughaibuni.
 
Hiyo inaweza kuwa rekodi ya aina yake kwa kuwa haijawahi kutokea tangu Uhuru kwa Rais mstaafu kusafiri safari nyingi za nje ya nchi kushinda Rais aliyeko madarakani.
 
Hadi sasa, Rais John Magufuli ametumia siku zote za kuwa kwake madarakani kusimamia kampeni yake ya kuongeza mapato ya serikali na kukomesha vitendo vya ufisadi kupitia kile anachokiita ‘kutumbua majipu’.
 
Mbali na mataifa mbalimbali aliyokwishatembelea, rekodi zinaonyesha kuwa Machi 21 mwaka huu, Kikwete alikwenda nchini Tunisia kwenye mkutano wa nane wa nchi majirani na Libya ambapo yeye ni mwakilishi maalum wa Afrika wa usuluhishi wa mgogoro wa taifa hilo.Kabla ya kwenda Tunisia, Kikwete alikuwa katika mji wa Salalah nchini Oman alikoshiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya na alishindwa kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Shein kutokana na kuwa nje ya nchi.
 
Katika mkutano wake na viongozi wa Libya, Kikwete alisisitiza kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.
Juzi Rais huyo mstaafu aliwasili Dubai akitokea Tunisia kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa shughuli hizo hizo za upatanishi wa mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Libya.
 
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa tayari JK ameshakwea ‘pipa’ na kufika nchi za Ethiopia, Uingereza, Visiwa vya Comoro, Afrika Kusini, Ujerumani, Marekani, Oman, Libya, Tunisia na UAE huku baadhi ya safari hizo zikitokana na mialiko maalum anayopata.
Wakati Kikwete akiendelea kusafiri kutokana na majukumu mbalimbali yanayomkabili akiwa Rais mstaafu, Rais Magufuli ameendeleza rekodi yake ya kutosafiri. 
 
Mara baada ya kuingia madarakani kufuatia ushindi wake wa asilimia 58.46 katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, Rais Magufuli alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi yasiyo ya lazima kwa serikali na pia kuwabana wakwepa kodi ili hatimaye kuinua mapato na mwishowe kunufaisha Watanzania kwa kuwaondolea kero mbalimbali zitokanazo na huduma za jamii.
 
Hadi sasa, tayari Rais Magufuli ameshachukua maamuzi kadhaa makubwa yaliyookoa mabilioni ya fedha na pia kuongeza nidhamu ya kazi katika ofisi za umma. 
 
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli ni pamoja na tangazo lake la kudhibiti safari holela za nje ya nchi kwa viongozi wa Serikali ambazo sasa ni lazima zipate kibali chake au cha Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu.
 
Wakati akilihutubia Bunge Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli alisema safari holela za nje huligharimu taifa mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo. 
 
Alitoa mfano wa safari za nje zilizogharimiwa na serikali katika mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015 ambazo ni Sh. bilioni 356, huku Sh. bilioni 104 kati ya hizo zikiteketea kwa posho za safari hizo kwa viongozi na maafisa wengine wa juu wa serikali.
 
Pia ameshafuta matumizi ya fedha za serikali kwa ajili ya maadhimisho ya siku mbalimbali za kitaifa ikiwamo Uhuru na Ukimwi, ambazo kwa kawaida huigharimu serikali mabilioni ya fedha. 
 
Aidha, mwendelezo wa utumbuaji majipu wa serikali ya Rais Magufuli umewezesha kufichua ukwepaji kodi kupitia uondoaji mizigo bandarini unaodaiwa ulikuwa ukilikosesha taifa takriban Sh. bilioni 600, zaidi ikiwa ni kutokana na kontena 2,431 zilizopitishwa kinyemela bila kulipiwa kodi. 
 
Mpaka sasa, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi Tanzania, Rished Bade, amesimamishwa kazi kutokana na kashfa ya kontena huku Alphayo Kidata akiteuliwa kushika nafasi yake.
 
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Awadh Massawe ameondolewa baada ya uteuzi wake kutenguliwa na pia iliyokuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA imevunjwa huku maafisa takriban 50 wa TPA na TRA wakifikishwa mahakamani kutokana na tuhuma zinazohusiana na ukwepaji kodi huo.
 
SAFARI ZA MAGUFULI
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa tangu alipoingia Ikulu Novemba 5, Rais Magufuli hajawahi kupanda ndege ili kwenda nje ya nchi na ameonekana akitumia muda mwingi kuandaa mazingira ya utekelezaji wa ahadi zake mbalimbali alizozitoa kwa Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
 
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kuonyesha njia juu ya namna ya kutekeleza dhamira yake ya kudhibiti safari holela za nje, Rais Magufuli hajasafiri kwenda ughaibuni walau kwa ajili ya kujitambulisha.
 
Magufuli alisafiri kwa gari kutokea Ikulu jijini Dar es Salaam hadi katika Ikulu Ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Novemba 17, 2015. Alikaa Dodoma kwa zaidi ya wiki moja na kutimiza jukumu lake la kutangaza jina la Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), kumuapisha (Waziri Mkuu) na kisha kuzindua Bunge.
 
Mara baada ya kulihutubia Bunge Ijumaa, Novemba 20 mwaka jana, Rais Magufuli alirudi Ikulu jijini Dar es Salaam Novemba 26, ambako alijichimbia na kuendeleza kasi yake ya ‘kutumbua majipu’.
 
SAFARI ALIZOJINYIMA MAGUFULI 
Pengine katika kutekeleza agizo alilolitoa la kudhibiti safari za nje, Rais Magufuli hakujihusisha na safari ya kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), uliofanyika visiwa vya Malta Novemba 27, 2015.
 
Badala yake, Magufuli alimtuma Balozi wa Tanzania nchini Uingereza kwenda kumuwakilisha katika mkutano huo, akiwa pamoja na maofisa wengine watatu na hivyo jumla yao kuwa watu wanne. 
 
Inaelezwa kuwa wakati wa utawala wa awamu ya nne, msafara kwenye mkutano kama huo uliofanyika Malta ulikuwa ukimhusisha Rais, baadhi ya mawaziri na maafisa wengine wa juu serikalini ambao kwa ujumla walikuwa takriban 50. 
 
Novemba 29, Magufuli alitakiwa kuwapo jijini Paris, Ufaransa katika mkutano wa kimataifa wa 21 kujadili mabadiliko ya tabia nchi duniani (COP21) ambapo wakuu wa nchi takriban 150 kutoka katika nchi 195 walishiriki, wakiwamo marais Barack Obama wa Marekani na Xi Jinping wa China. 
 
Hata hivyo, Magufuli hakukwea ndege kwenda kuhudhuria mkutano huo na badala yake akabaki nyumbani akiendelea kushughulikia ‘upasuaji majipu’ hasa TPA na TRA.
 
Desemba 5, 2015, Rais Magufuli hakupanda ndege pia kwenda Johannesburg, Afrika Kusini kulikokuwa na mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za Afika na Rais wa China, Xi Jinping, kupitia Jukwaa la Nchi za Afrika na China (FOCAC). Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. 
 
BAADHI YA SAFARI ZA KIKWETE
Siku chache baada ya kuondoka Ikulu, Kikwete alikuwa jijini Addis Ababa, Ethiopia ambako aliwahi kuripotiwa Novemba 26, 2015 akiipongeza timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyokuwa imetinga robo fainali ya Kombe la Chalenji.
 
Novemba 30, Kikwete alikwenda Moroni, Comoro baada ya kuteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kwenda kuhudhuria mkutano ulioangalia namna ya kukabili dalili za mgogoro wa kisiasa visiwani humo kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Aprili, 2016.
 
Baadaye Kikwete alikwenda jijini London, Uingereza ambako alihudhuria mkutano Mkuu wa 20 wa Taasisi ya Ushirikiano wa Usimamizi wa Sayansi na Teknolojia kwa nchi za Jumuiya ya Madola (CPTM) na kutunukiwa tuzo maalum kwa kutambua mchango wake katika ukuaji wa matumizi ya Sayansi na Teknolojia, ikiwamo matumzi ya simu katika utoaji wa huduma za fedha.
 
Alitunukiwa tuzo hiyo Desemba 1, 2015.
Aidha, Kikwete alikwenda jijini Johannesburg, Afrika Kusini, kama mualikwa, kuhudhuria Mkutano wa Tano FOCAC uliofanyika Desemba 4, 2015. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kudumisha maendeleo ya pamoja kati ya nchi za Afrika na China, kuibua maeneo ya maendeleo yakiwamo ya miundombinu na kuimarisha fursa za kibiashara.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment