Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, March 24, 2016

Magufuli, Museveni wampelekesha Uhuru

By Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais John Magufuli kukubali haraka mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga umemgutua Rais Uhuru Kenyatta, ambaye sasa anahaha kuishawishi Uganda ibadili msimamo wake.
Rais Yoweri Museveni na Magufuli walisaini makubaliano ya ujenzi wa bomba hilo la urefu wa kilomita 1,120 Machi Mosi, na kuifanya Uganda kuachana na mradi huo wa Dola 4 bilioni kupeleka bomba hilo hadi Lamu nchini Kenya.
Kenya na Uganda zilikubaliana katikati ya mwaka jana ujenzi wa bomba hilo, lakini hazikuafikiana njia ambayo lingepitia kutokana na sababu za kiusalama na hofu ya malipo ya fidia kwa wamiliki wa ardhi.
Uamuzi wa Rais Magufuli kukubali mradi huo utakaozalisha zaidi ya ajira 15,000 wakati wa ujenzi, ndiyo ulioharibu mipango ya Kenya, na sasa Kenyatta amefufua mazungumzo hayo.
Kenyatta alikuwa na mazungumzo na Museveni jijini Nairobi Jumatatu, lakini hawakuweza kufikia makubaliano na hivyo kupanga kukutana tena ndani ya wiki mbili jijini Kampala, linandika gazeti la Daily Nation la Kenya.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo, mawaziri wa nishati wa Uganda na Kenya walitangaza kuwa kikao hicho kilikuwa na mafanikio na kilijikita katika kupunguza gharama za ujenzi na sehemu ya kupitishia bomba hilo.
Mkutano ujao utawapa fursa mawaziri hao kuwasilisha mpango mmoja wa jinsi ambavyo bomba hilo litajengwa ikiwa ni pamoja na gharama za usafirishaji mafuta.
Daily Nation iliripoti mapema wiki hii kuwa utafiti uliofanywa na kampuni za mafuta ndiyo ilikuwa suala kubwa lililojadiliwa na marais hao wawili jijini Nairobi Jumatatu.
Gazeti hilo limemkariri ofisa mmoja kutoka Wizara ya Nishati akisema utafiti wa kampuni za Tullow Oil plc na China National Offshore Oil Company (CNOOC) umeionya Uganda dhidi ya kuendelea na mpango wake wa kujenga bomba hilo kutoka Hoima, kupitia Lokichar (kaskazini mwa Kenya) hadi Lamu.
“Inaeleweka kuwa kampuni hizo mbili zinazofanya kazi pamoja na Total ya Ufaransa zilionya kuwa mkakati wa Uganda kuanza kuchimba mafuta kwa ajili ya kuuza nje ifikapo mwaka 2018, unaweza kucheleweshwa kama itaendelea na njia ya Kenya,” linaandika gazeti la Daily Nation.
Katika kikao hicho, Rais Museveni aliwasilisha matokeo ya utafiti huo kuonyesha sababu za mpango wake wa hivi karibuni wa kuelekeza nguvu kwenye njia ya Tanzania.
Gazeti hilo limekariri vyanzo vinavyosema kuwa Kenya ina historia ya migogoro ya malipo ya fidia ya ardhi, ambayo itachelewesha ujenzi wa bomba hilo kutoka Lokichar hadi Lamu. “Hoja ya Uganda ni kwamba utafiti wa Tullow na CNOOC umesema malipo ya fidia ya ardhi ni suala kubwa litakalochelewesha ujenzi wa bomba kupitia kaskazini,” The Daily Nation limemkariri mmoja wa maofisa waliohudhuria mkutano huo.
Utafiti huo umetoa mfano migogoro mikubwa iliyokuwapo wakati wa kuchukua ardhi kwa ajili ya ujenzi wa bomba wa Lamu Port Southern Sudan-Ethiopia Transport (Lapsset) na ujenzi wa reli ya viwango vya kimataifa (SGR).
Utafiti huo unaonya kuwa migogoro hiyo inaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama kwa sababu wamiliki wa ardhi wana tabia ya kupandisha bei kunapokuwa na miradi.
Uganda pia imedai utafiti umeonyesha maeneo ambayo bomba litapitia hayana barabara nzuri na hivyo hilo litakwamisha ujenzi, hali kadhalika bandari ya Lamu bado haijajengwa na inaweza kuwa haijakamilika ifikapo mwaka 2018 wakati Uganda itakapokuwa tayari kuanza kusafirisha nje mafuta.
Utafiti huo umeishauri Uganda ikubaliane na Tanzania, ambayo bandari yake ya Tanga inahitaji marekebisho madogo.
Lakini Kenya iliihakikishia Uganda kuwa suala la vikwazo vya malipo ya fidia halitachelewesha ujenzi wa bomba na kwamba ujenzi wa reli unaendelea baada ya wamiliki wa ardhi kufidiwa. Kenya pia ilisema ujenzi wa barabara pembeni ya Lapsset unaendelea.
Ujumbe wa Kenya pia ulikihakikishia kikao hicho kuwa mara ujenzi wa bomba hilo utakapokamilika, itahakikisha linalindwa, ikitoa mfano wa bomba la mafuta kutoka Mombasa hadi Eldoret.
“Kuhusu mashambulizi ya kigaidi, hatua za kutosha zimechukuliwa. Kwanza tishio la ugaidi liko kwenye nchi zote za Afrika Mashariki,” ofisa wa Wizara ya Nishati alikaririwa na Daily Nation.
Waandishi wa Kenya wanasikitika mradi huo kutekwa na Tanzania.
“Njia ya Tanzania sasa inaweka ushindani mpya kwa usafirishaji wa baadaye wa mafuta kutoka nchi nyingine za maziwa makuu, hasa mashariki ya Congo DR na Sudan Kusini,” linaandika Daily Nation
Mwandishi wa kujitegemea wa Uganda, Angelo Izama aliandika katika barua yake ya wazi kwa Rais Museveni kuwa kupitishia bomba hilo Tanzania kuna faida kwa Waganda.
“Njia mbadala ya bomba kwenda Tanga itatupa nafasi ya kufikia bandari mpya na kupanua wigo wa biashara na Tanzania,” anaandika Izama katika barua hiyo aliyoichapisha kwenye tovuti yake.
“Hii itajumuisha kuagiza na kuuza nje gesi asilia ya Tanzania ambayo Uganda inaihitaji kwa ajili ya unafuu katika gharama za kupikia.”   

No comments :

Post a Comment